Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, August 9, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-11‘Hahaha Docta, kumbe ni kweli wanavyosema wewe ni mrembo sana, mmmh natamani kuziibua hisia zangu,… na ukiwa hivyo uchi natamani kufanya kile wenzangu wanachopenda kukifanya, lakini mimi siko huko kabisa, tangu mke wangu anisaliti na kutoa siri zangu kuwa nimeamua kuisaliti nchi,…nikaanza kusakwa kama mhalifu…nilimuona kama …sijui kitu gani… nikawa sitamani mwanamke yoyote…nilimpenda sana mke wangu nikampa kila kitu anachokitaka, lakini mwisho wa siku alinigeuka….hapana…nikaamua kutokupenda mwanamke yoyote, kwani kila nimuonaye namfananisha kama yeye, simuamini tena…na hata nikijaribu kufanya mapenzi na mwanamke yoyote namuona kama ni mke wangu yupo mbele yangu natamani kuua tu….

`Ila kama binadamu ipo siku nashindwa, namtafuta wa kuondoa tamaa za kimwili lakini mwisho wa siku huyo aliyejitolea kwangu anajuta kwanini alikutana na mimi kwani nageuka kuwa mnyama…aah,imefikia hatua naona bora nisiwe na mwanamke, ili mradi siathiriki…ila nakuhakikishia kuwa sipo katika hawo wabakaji nafanya hivyo kwa hiari ya huyo nilyekubaliana naye na akiwa tayari kufanya hivyo kwa makubaliano ya hiari. Na nakuomba uniamini sipo kwa nia hiyo…sipo hapa kama mnavyotuzania kama wanavyotangaza kwa propaganda potofu nipo hapa kwa ajenda moja tu, ya kukupa ujumbe, na ujumbe huu huenda ukauchukulia kirahisi rahisi, lakini nakuomba uuchukue kama ujumbe wa kivita, lolote laweza kutokea…na nakuhakikishia kuwa sisi tuna imani yetu, na nisingependa kuiharibu imani yangu na taratibu zetu za katiba yetu,…’ akaonyesha ishara ya imani yake, halafu akaangalia juu kama anamuomba mungu wake.

`Docta ni kweli wapo miongoni mwetu ambao kwa malengo yao binafsi wamekuwa wakiharibu kile tulichokidhamiria,ili tuonekane wakorofi, lakini sio kweli kuwa tupo hivyo, sisi tuna katiba yetu, tuna mwongozo wetu, na upo wazi kuwa mbakaji, muuaji na yoyote atakayesaliti anafanyiwa nini hilo lipo kwenye katiba yetu, na sio mahali pake kukusomea hukumu zake hapa, lakini zipo hatua kali hazina mchezo, kwani zina mkono wa imani za dini zetu…nakuhakikishia kuwa hatupo kama wanavyotupakazia matope hawo wabaya wake…’ aliongea yule mtu akiwa kajaa madevu, na nguo zilionekana za uchakavu kidogo, lakini alionekana na cheo katika jeshi ambalo Rose hakulijua na jeshi gani.

‘Mimi ni mmojawapo wa kiongozi wa wanaopigania mapinduzi, au siku hizi wapenda kuita demokrasia na karibuni nitastaafu, nisingependa kuendelea na vuguvugu hili tena, kwasababu umri umekwenda na hata hivyo tulikuwa na nia njema, tulikuwa na malengo mema, lakini wamekuja vijana wenye hamasa..siwalaumu, kwasababu damu inawachemka, …kwahiyo wao wanadai sisi wakubwa tunachelewesha mambo…kiukweli wao wameanza hata kuharibu ile katiba yatu yenye nia njema, na ukijaribu kuwaweka sawa wanaona kuwa tunaanza kuogopa, hata wanafikia kusema sisi viongozi wa zamani ni wasaliti, sasa kwangu mimi nimeona ni bora tuwaachie uongozi wao tuone nini walicho nacho ambacho hatuna, ila tunafanya kwa uangalifu mkubwa na tutakuwa nyuma yao kuwaunga mkono…

‘Docta utashangaa kwanini nimekuja hapa kwako leo hii, na kukuelezea haya yote, au kwanini nisiende kwa bosi wako moja kwa moja…’ akasogea yule mtu hadi dirishani na kuangalia nje , labda alikuwa akihakikisha usalama wake au ndio mbinu zao,…akawa anaongea huku kaangalia nje, hakujali kuwa Rose anaweza kumuvamia kwa nyuma, labda alihakikisha kuwa Rose hana silaha…Rose akapata muda wa kupumua, kwani alikuwa akiyaogopa yale macho yenye kutisha, yalikuwa na sijui ni makengeza au ni kitu gani kile…akapumua na mara akajiangalia na kushangaa, kumbe yupo uchi…akasogea taratibu na kuchukua khanga yake na kujifunika haraka haraka,…akangalia mlangoni, akitaka kutoka na kukimbia, lakini mwili ukawa mzito kufanya hivyo….
‘Sisi ni wana uvuguvugu la msituni tunaodai haki zetu, tangu raisi yule wanayemuita Nduli kuondoka, tulianza kutengwa na kunyanyaswa, na kutokupewa haki zetu,wakasahau kuwa tulikuwepo madarakani tulikuwa pamoja katika mstari wa mbele kumuondoa huyo nduli,…alipoondoka wakagawana madaraka wao wenyewe , na sisi tuliojitolea hadi hata wengine kupoteza maisha na hata kuwa vilema, wametuweka pembeni,…unaona hili jicho langu, hapa ni risasi ilipita…sasa fikiria uchungu gani ninaoupata…tukajaribu kudai haki zetu…hakukufanikiwa na hapo tukaona haiwezekani tukaasi jeshi na kuingia msituni, na lengo ni kudai haki zetu…tuliona bila mtutu wa bunduki hatutaweza kusikilizwa,…tukawa wanamapinduzi, tunadai mabadiliko…’ akageuka na kuangalia mlangoni, halafu kama aliyekumbuka muda akaendelea kusema

`….Sio kwamba tulikimbilia kutumia nguvu, kwamba tunapenda kumwaga damu…kuwa hatutaki kufuata utaratibu, hapana tulifuata taratibu zote za kudai haki zetu, lakini hatukusikilizwa,…yakawa yanakuja madai kuwa hatuna elimu, hatu…ooh, hatuna elimu wakati hawo wenye elimu wanaajiriwa hawajui lolote tunaambiwa sisi tuwape mafunzo…elimu gani wanaitaka….ndipo baadhi tukaamua kusaliti jeshi na nchi yetu... Lakini hatujaisaliti nchi yetu, kwani nia yetu ni ili tupewe haki yetu, tuweze kuijenga nchi yetu kihalali…tunataka tuijenge nchi yetu kwa pamoja kwa haki sawa., bila dhuluma, bila ubaguzi na…’ akageuka kumwangalia Rose, halafu akasogea mlangoni.

‘Sasa kwanini nimekuja kwako, naona nisikupotezee muda wa kujipumzisha, wewe ni dakitari na katika hospitali ambazo zimekuwa zikisaidia watu bila kujali ni nani ni hospitali yenu, hili tunawapa hongera sana, licha ya kuwa mpo katika hali ngumu ya kusakamwa na jeshi, nalijua sana jeshi hilo kwasababu nimetokea huko, huwa kuna watu wanachukulia mambo juu, kwa juu tu bila kuangalia undani wake,..uzoefu wetu katika jesh umetuonyesha hivyo…wao ilimradi wana cheo , basi akisema lala ni kulala tu hata kama kuna hatari…lazima kila jambo liende kisayansi kiuzoefu, nan i vyema kuwa na malengo yenye mafanikio sio malengo ya kutesana, na jeshi sio sehemu ya kutesena, wao wanafikiria hivyo, sio kweli, jeshi ni sehemu ya kuweka amani, usalama, lakini watu wameharibu lengo hilo…hilo nalijua sana …sasa nakupa ujumbe huu…’ akageuka na kumwamgalia Rose kwa yale macho yanayotisha na Rose akawa nanatetemeka mwili mzima, na kama ingekuwa haja ingeshatoka bila yay eye kujijua.

‘Kuna watu wetu wameamua kuja huko hospitalini kwenu na wengine hujifanya wanaumwa, na mwisho wa siku wanatutoroka na kutusaliti na hata kutoa siri zetu kwa wabaya wetu, na hili tumeliona baada ya uchunguzi mkubwa, na tumeona kuwa upenyo wanaoutumia ni kwenye hospitali yenu, na kama nilivyokuambia awali kuwa hospitali yenu ni moja ya hospitali tunayoiunga mkono na kama lengo letu lingefanikiwa tungeifanya iwe moja ya hospitali kubwa, lakini bado tuna safari ndefu….ila tunaiunga mkono kwa hali na mali…hamlijui hilo na haina haja kulijua hilo…

‘Twawataka hawo watu ambao baaadhi yao bado wapo kwenye matibabu yenu , tunawahitaji haraka warudi kambini, nyie watibieni, msijali cha gharama, tutawalipa…na nasikia kuwa wengine wameingia mikononi mwa jeshi la serikali na wameteswa sana, hili twalijua, lakini ndio vita, tutawakomboa muda si mrefu…sasa ni hivi…’ akawa kama anamsogelea karibu lakini hakumkaribia sana akaongea kwa sauti ya chini `…. kama tutahakikisha kuwa nyie mnawachukua watu wetu na kuwakabidhi kwa serikali kwa jeshi hilo la serikali , kituo hiki tutakisamabaratisha mara moja, najua mnatujua…hilo’ akatoa macho na upande mmoja, uliokuwa na kovu kubwa ukawa unaonekana umemega sehemu ya jicho na kuliweka jicho lionekane kubwa kupita kiasi...!

‘Najua mnatujua , ingawaje sivyo tunavyotangazwa, ila , tukiamua tumeamua, tunawapa muda kulitafakari hili,…hasa kwa watu wetu hawo…nakuomba sana ujumbe huu ufikishe kwa bosi wako…kama kuna mtu kaja kutibiwa hamumjui katoka wapi , msikimbilie kuwakabidhi kwa hawo wanajeshi, mtibieni na akiwa kapona haina haja ya kumdadisi sana kuwa yeye ni nani na watu wetu wanajulikana, hawajifichi…mtibieni na mwachieni…na mumekuwa mukipokea hela bila kujua zimetoka wapi, hizo ni gharama za watu wetu waliobahatika kurudi kambini….kama hawakurudi, hatuwezi kulipa…’ akanyamaza kama anatafakari kitu

‘Najua utasema kwenu itakuwa kazi ngumu, kuanza kufanya hivi au vile, wakati mpo kwenye kazi zenu, nakuhakikishia kuwa sisi tupo nanyi kuliko mnavyodhania, kila linalofanyika hapo hospitalini kwenu tunalijua, tunaliona…na kwa taarifa yako yupo jamaa yetu mmoja ni mtaalamu wa silaha, tunamtafuta sana,kachanganyikiwa kiajabu,…kawa kama zezeta fulani, haelewi na hajielewi, tunaogopa huenda akawa ni hatari kwa maisha ya watu,…tunamtafuta,… na baada ya uchunguzi tumegundua kuwa yupo kwenu…ole wenu mkimkabadhi kwa hawo askari…ole wenu, kama akipona…tutakuja kumchukua,…sisi tutakuja kumchukua, usiulize namna gani, hiyo sio kazi yenu…lakini ole wenu kama ataishia mikononi mwa maaskari, samahani kwa kukuharibia mapumziko yako…’ mara akatembea hatua mbili hadi mlangoni, na akafungua mlangona dakika chache kukawa kimiya, yule mtu aliyeyuka kama upepo…

Rose alitafakari yale maneno kutoka kwa yule mtu anayejiita mwanamapinduzi, hakuamini kuwa keshaoandoka mle ndani,…kilichobakia ni harufu yake ya majasho… alijilaumu kwanini hakumuuliza kuhusu yule mgonjwa wao ,huenda wao wamemchukua …akatoka nje haraka akiwa na maana ya kumuwahi ili amuulize, lakini hakuweza kumuona mtu..akaangalia huku na kule bado akiwa na wasi wasi, kulikuwa kama hakukuwa na mtu aliyetoka mle karibuni, alikuwa mwepezi kama upepo, akaanza kuogopa, akijua anaweza akarudi tena, na akiwaza jinsi gani alivyoweza kufungua mlango wake…hapo akatamani arudi hospitalini haraka amfikishie Docta Adamu huo ujumbe, lakini kutokana na hali aliyomuacha nayo bosi wake asingeweza kueleweka akaona ajipumzishe kwanza, akaoga na kujaribu kulala kidogo , lakini usingizi haukuweza kumjia akainuka pale kitandani akiwaza mengi…lakini alishangaa badala ya kuwaza tukio hili la karibuni la huyu anayejiita mwanamapinduzi, akajiona anazama kwenye mawazo ya mtu mwingine…sura ngeni kabisa ikawa anamjia akilini...

Ilikuwa na ufukweni mwa ziwa, wavuvu walikuwa wakitembea huku na kule, baada ya lile tukio lilotokea upende wa pili wa lile ziwa samaki wamekuwa wakipatikana kwa wingi, lakinii walikuwa hawana soko…hisia na maneno ya watu kuwa samaki hawo watakuwa wamekula nyama za watu zilikuwa zimeenea sana …lakini wavuvi hiyo ndiyo kazi yao, wasipopata pesa kwa kazi hiyo ina maana hawana zaidi ….

Rose alikuwa na mazoea ya kuja hapo ufukweni kuchukua mazoezi na hata baadhi ya wavuvi walishamzoea, na akipita utasikia wakimuita `docta..docta…docta…’yeye huwapungia mkono na kuendelea na mazoezi yake, watu walikuwa wakimpenda sana kwa matibabu yake, alikuwa docta wa watu na watu walimkubali. Leo alifika hapo akawa anatembeatembea tu akiwa na mawazo mengi. Leo alikuwa na lengo moja kumtafuta jamaa mmoja ambaye ndiye inasadikiwa alimleta yule mgonjwa, ….alitaka kujua tu kama anajua lolote kuhusiana na yule mgonjwa.
‘Docta, docta….mbona leo huchukui mazoezi…?’ akawa anaulizwa na wavuvi
‘Leo najisikia hali sio shwari, ila nilikuwa namuulizia mzee wa samaki, lao kaja kweli huku ufukweni?’ akaulizwa yule mvuvi.

‘Mhh, tangu watu waanza kususia samaki kutokana na lile janga lililotokea kule Tanzania, haonekani mara kwa mara …na hata sisi tunafika tu, samaki wapo wengi ajabu, lakini hawana soko, kwani ile ajali ya kule Tanzania ya kuzama kwa ile meli, imeleta kizaa zaa hadi huku, watu hawataki kununua samaki wakidai kuwa samaki hawo wamekula nyama za watu…tumejaribu kuwaambia kuwa kule ni mbali sana hakuna maiti zinaweza kufika hadi huku na hata hivyo kipindi sasa kimepita…’ akasema yule mvuvi

‘Poleni sana, kwani yeye anaishi wapi..na nikuulize siku moja mlimuokota mgonjwa mmoja akiwa kalala ufukweni , ilikuwaje…?’akauliza docta Rose.

‘Yule inaonekana alijaribu kuogelea akazama, au alikuwa mlevi akawa kazidiwa na kulala ufukweni, kwani walevi mara nyingi tunawakuta maeneo ya ufukweni,…tatizo la huyu, alikuwa pembeni kabisa ya ziwa, akiwa kama kakupwa …na alikuwa mfu kabisa…wataalamu walimshika shingini wakasema kafa…na sote tulijua kafa….tunashangaa kusikia yupo hai, haya maajabu ya mungu..’ akasema yule mvuvi.
‘Haiwezi ikawa ni mmoja wa hawa wapiganaji wa masituni, …?’ akauliza Rose
‘Aaah , haiwezekani kabisa, mpiganaji wa msituni awe kama yule, laini laini namna ile, wewe uliwahi kukutana na hawa watu, mikono yao imeshupaa, wana minywele kama wanyama wa porini..ukimuona mmojawapo utafikiri umekutana na mnyama wa porini…hapana haiwezekani akawa mpiganaji wa msituni…hata hivyo …alionekana kama mtu wa ofisini…sijui lakini…sikumataka kumchunguza sana, kwani mimi nilimuona kama maiti tu….” akasema yule mtu akiwa na mashaka mshaka.

‘Hamjakuta chochote, hamkuona kitu cha kuweza kumtambua huyo mtu kama jina lake…na…na chochote cha kumtambusha….?’ Akauliza docta Rose

‘Hapana, kwanza nani alikuwa na hamu ya kuushika mwili wake, …tulichofanya ni kuhakikisha kuwa yupo hai au kafa, na bahati kukawa na askari walikuwa katika doria, tukawaita wakaja wakamchukua, ila nimekumbuka...ndio Mzee wa samaki aligundua karatasi imejitokeza, akaichukua …ilikuwa imechokachoka,…tuliikagua baadaye ilikuwa na namba namba tu…na ile karatasi aliichukua mzee yule, hakuwapa wale maaskari…kwasababu haikuwa na maana yoyote, wengine tukadhani kuwa nii hundi ya banki…lakini sio hundi…na kwasababu ilikuwa imechanika na kuchokachoka, hatukuona umuhimu wa kuwapa wale maaskari, ila yule mzee aliichukua, hakutka kuitupa...
Rose aliposikia hivyo akaondoka hadi kwa huyo mzee wa samaki, alipofika alimkuta akifanya bishara ndogondogo akasalimina naye halafu akamuomba kuwa ana mazungumzo naye;

‘Umesema unahitaji kuona ile karatasi niliyoichukua kwa yule mtu tuliyemuokota, nani kakuambia kuwa nilichukua karatasi…duh, watu bwana wana macho makali…ni karatasi iliyochokachoka, niliichukua tu na sikukumbuka kuwapa wale maaskari, na nakumbuka niliitumbukiza hapa juu…’ akasema na kukagua kwenye makaratsi aliyoyaweka juu ya paa la bati la banda lake la biashara., akaiona halafu akaikagua kuhakikisha kuwa ndiyo yenyewe na kumpa docta Rose.

‘Hii hapa… chukua kabisa hiki kikaratasi, kisije kikanileta zengwe , maana kama umeshaambiwa hivyo,kuwa nimechukua kikaratasi mwisho wa siku polisi watanijia mimi na kudai mengine…siitaki tena, kwanza haina maana yoyote kwangu…na hatukuona kitu kingine, zaidi ya kuonyesha suruali yake imelowana…na kama kulikuwa na kitu laini ni lazima kitakuwa kimelwoana pia…’ akamkabidhi docta, na docta alijaribu kumuuliza maswali mengi kama yale aliyomulizia yule mvuvi kule ufukweni na majibu yake yalikuwa yale yale,…

‘Huyu sio mpiganaji kabisa, hilo sikubaliani nalo Docta, sisi wapiganaji tunawajua, sura zao uvaaji wao…hawajifichi…huyu labda useme ni mlevi ….lakini hata dalili ya ulevi haipo…sijui imekuwaje maana ukimchunguza sana anaonekana ni mtu wa ofisini….lakini hata majambazi siku hizi wapo hivyo, hutaamini , majambazi wanakuwa kama mameneja ofisini, yeye anacheza na kalamu na silaha….’ Akasema yule Mzee wa samaki

Docta Rose aliichukua ile katarasi na kuikagua vyema, na akagundua kuwa ni kitu kama tiketi ya kusafiria, ilikuwa haionyeshi vyema kwani sehemu ya jina ilikuwa haipo imachanika…ila kwa nyuma aligundua kuwa kuna namba ambayo ilionekana kama namba ya simu…akaukunja vyema na kuitumbukiza kwenye pochi yake akaondoka na kurudi nyumbani kwake…alipofika kwake ilikuwa ni usiku na kwa vile ilikuwa siku ya mapumziko kwake akaona ajisomee kitabu chake kupoteza muda…lakini wazo likamia kukikagua kile kikaratasi tena…na kabla hajatulia vyema, mara mlango ukagongwa, alikurupuka haraka akalitafuta lile panga lake kama silaha, akijua yule jamaa karudi tena au jamaa zao wengine.

Alisogelea mlangoni na kuchungulia kwenye kitundu maalumu kilichowekwa mahsusi kwa kuangalia nje, kwa ajili ya usalama, kwani maisha yao yamekuwa ya wasiwasi, wapiganaji wa msituni wamekuwa tishio, kila siku kuna taarifa za kukamatwa kwa watu, mara kubakwa, na hata kuuwawa, kwahiyo hakuna aliyekuwa na amani..hasa ikifkia usiku, nan i vyema kuwa wawiliwaili, kuliko kubakia mwenyewe, lakini zamu zao hazikuwa zimapangwa hivyo, siku nyingine wanajikuta wanatofautiana. Alitizama nje kwa kupitia kile kitundu lakini hakuona dalili ya mtu…akatulia kimiya kusikiliza tena, mara mlango ukagongwa tena, safari hii kwa fujo, akajua ndio hawo hawo …akatizama kwenye kile kitundu hakuona mtu, ina maana huyo mtu alikuwa akigonga na kutoweka…haiwezekani!
‘Wewe nani na unataka nini kwangu..? akauliza Docta Rose lakini hakupata jibu!

Hakupata jibu kulikuwa kimiya tu… na Docta Rose, akaogopa kabisa kufungua mlango…akasema kimoyoni sifungui mlango hata kwanini…akasubiri na ukapita muda, akatamani kurudi kulala, lakini moyo wake haukumpa ujasiri huo akawa bado anasubiri, lakini kulikuwa kimiya…baadaye sana akaona afungue ule mlango kwa tahadhari. Alipofungua ule mlango na panga mkononi akaangalia huku na kule, hakuona mtu, akaurudishia mlango wake kwa nyuma, akiwa kasimama akiangalia huku na kule, alihakikisha ameufunga vyema, lakini sio kwa ufunguo, akasogea mbali na ule mlango, huku bado akiangali huku na kule,…karibu na nyumba yao kulikuwa hakuna mtu , ila barabarani watu walionekana wakipita wengine wanakwenda huku wengine kuelekea kwingine, lakini hakuona mtu aliyemuonea shaka, na wala hakukuwa na mtu karibu na eneo la nyumba, kila mtu alikuwa mbiombio kuwahi kwake...

Baadaye akawa karizika kuwa huyo mtu huenda alikuwa mpita njia tu na alikuwa na shida ya kupita, kwani ukiwa unaishi karibu na njiani, utapata wageni wa aina mbalimbali, wengine wanahitaji maji ya kunywa, wengine wanataka kujisaidia, wengine wanauliza njia, ilimradi shida za dharura zipo nyingi tu,inabidi kama binadamu uwasaidie wenzako…baada ya muda akaona afanye utafiti wa ziada akasogea kidogo kule kwenye mlango wa rafiki yake ili kuhakikisha usalama, akajaribu kuufungua mlango wa rafiki yake akakuta bado umefungwa,…akaangali huku na kule hakuona kitu cha kutilia shaka, halafu akaamua kupita nyuma na nyumba kukagua hakuona dalili ya mtu,… baadaye akaona arudi kwake, na alipofika mlangoni akahisi nyewele zikisisimuka, moyo ukawa unanmwenda mbio, vipi kulikoni …akahisi wasiwasi, na mwili ukamlegea,....oh mlango upo wazi, mlango ambao alikuwa kahakikisha ameufunga sasa upo nusu wazi..!

Jamani ngoja niishie hapa nitayarishe sehemu inayofuata. TUPO PAMOJA


Ni mimi: emu-three

5 comments :

Precious said...

Yaani mwili umenisisimka as if me ndio Dr. Rose...tupe uhondo M3 tuko pamoja yaani natamani kila nikiingia huku nikute mwanzo hadi mwisho wa story nzima, ila ndio haiwekani lazima kuwe na episode ili story iwe nzuri zaidi.... Keep it up una kipaji sana.

emu-three said...

Ahsante sana Precious kwa kuwa pamoja nami na kunipa moyo nafarijika sana kwani ingawaje naandika kama hobby lakini kwa wakati mgumu sana ! Hutaamini naandika hii meseji kwenye giza hakuna umeme,natamani kesho niamuke saa kumi ili niwahi ofisini nikaendeleze sehem inayofuata lakini kuna mtihani wa usafiri wenye mafuta wamegoma

Candy1 said...

Tanzania haiishi balaa...mara hamna umeme sasa wenye mafuta wanaringa...mmmh...anyway kwenye story mmmh, mbona wanamuandama docta Rose jamani..ila part hii imenisisimua pia, I can't wait for the next part..

hansom said...

Mkubwa stori tamu sana hii, vp umewahi kuwa askari nn, au upo jeshini hadi leo!!!? Hongera sna kwa burudani zenye mafunzo hasa ya ujasiri.

emu-three said...

Candy Tanzania ni ule usemi wa kufa hatufi lakini cha moto tunakipata! Hansom ukiwa mwandishi wewe ni mpiganaji na kwahiyo unatakiwa kujua kila nyanja.akini cha moto tunakipata! Hansom ukiwa mwandishi wewe ni mpiganaji na kwahiyo unatakiwa kujua kila nyanja.