Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, July 5, 2011

Dawa ya moto ni moto-30  Wakati hayo yakiendelea huko kwa Inspecta na Maua, katika chumba kingine walionekana  Wazee wawili ambao katika maisha yao yote wamekuwa mahasimu, lakini cha ajabu leo walikutanishwa katika chumba kimoja, na sio ndani ya chumba kimoja tu, bali katika meza moja wakiwa wameangaliana…Walipokaribishwa na kuingizwa ndani ya chumba hicho, kila mmoja akiwa amefika kwa wakati wake, walijikuta wamekaa, na kujikuta wanaangaliana, kila mmoja akiwa anashangaa, na kila mmoja akijaribu kuinuka akitaka kuondoka, lakini mkaribishaji aliwaomba kuwa watulie kidogo, kwani haitachukua muda wao mwingi…basi wakatulia kistaarabu, lakini kila mmoja akiwa kaangalia pembeni, na kama ilibidi kugeuka, ilikuwa kwa kujificha kuhakikisha mwingine hamuoni mwingine!
 Wakati wanahangaika, mara kipaza sauti kikasikika, na kuwafanya wageuka na kuangalia huko sauti inapotokea, ikawa kila mmoja anangalia kule mwenzake alipokaa, lakini humwangalii mwenzake usoni, kwani sauti hiyo ilikuwa ikitokea mbele kwa kila mmojawapo, lakini kwa juu, na mara ukutani kukatokea taswira ya mtu akiongea, taswira hii ungeiona popote unapogeukia, kwahiyo haikuwapa shida kugeuka huku na kule, na kwasababuu ya taswira hii, ile hali ya kuogopana ikawa  haipo na hawa wazee wawili  wakawa kama wanaangaliana, lakini sio kwa kuangaliana usoni, bali kumwangalia yule mtu anayeonakana ukutani akiwakaribisha kama ada …
‘Karibuni wageni wangu mashuhuri, karibuni wageni waalikwa, nyie ni wageni wangu mashuhuri…kabla ya kujitambulisha kuwa mimi ni nani naomba mlikumbuke tukio moja lililotokea miaka mingi nyuma, kipindi nyie mnatafuta mali, labda baada ya kumuangali huyo mtu nitapenda kuwauliza kama kweli mnafahamu huyo mtu…hebu tujikumbushe kidogo..’ mara ukutani kukatokea sura ya jamaa akiwa kashika kipande cha dhahabu mkononi huku ametabasamu…
Wazee wale wawili walipoiona ile picha, walishikwa na butwaa karibu wadondoke kwenye viti walivyokalia, na mara picha ile ikaondolewa ikaletwa picha ya mwanamke,… naye akiwa kashika vipande vingi vya dhahabu huku akiwa kama anamuonyesha mtu aliye mbele yake lakini alikuwa haonekani vyema. Hutaamini wale wazee wawili waliinuka wakitaka kukimbia kile chumba, na walipofika mlangoni wakawa wanagombea kushika kifungulio cha mlango, …na walipofanikiwa  kukishika kwa pamoja walikuta mlango umefungwa…wakabakia kuangaliana…na haraka wakarudi kukaa kwenye viti vyao, kwani ilionekana nguvu za mwili zilikuwa hazipo, kwa shinikizo la damu , na huenda na kisukari...
‘Naomba mtulie wazee wangu, mbona mna pupa ya kuondoka, mumesahau kuwa nyie ni wageni waalikwa, sasa mukiondoka shughuli hii itaendeswaje…na nawaona mpo katika hali mbaya, nawaombeni sana msifanye mambo ambayo yatawafanya mfe mapema, … nawaomba sana, sana, chukueni gilasi zilizopo mbele yenu mnywe hizo dawa, kwa afya zenu, kwani mpo mbele ya mtaalamu wa matatizo yenu…msipate shida kabla ya wakati wenu haujafiika…’ aliposema hilo wale wazee hawakupoteza muda wakachukua zile gilasi wakanywa vile vinywaji na kweli haikuchukua muda kila mmoja alijiona ana hali njema, halafu wakataka kuinuka kuondoka…
‘Mnakwenda wapi wazee, hamtaki hata kusema ahsante…mnajua gharama ya hiyo dawa, dawa kama hiyo ni milioni mbili, kwa dozi, mnaikumbuka sana,…kwani mumeshaitumia kabla, au sio… lakini …hayo tuyaache kwanza…turudi kwenye mazungumzo yetu ya awali...kwani mkumbuke kuwa mumealikwa kwa ajili ya mazungumzo muhimu sana, kama mnakumbuka vyema, hilo lilianishwa kwenye kadi zenu za mialiko …sio kwamba mliitwa kienyeji, nikijua kuwa nyie ni watu wa heshima, waheshimiwa, …je hayo mazungumzo yameshafanyika…na pia hapa mnatakiwa kukutana na familia zenu…kama sikosei..’ na mara kukaonekana upande mwingine kwenye chumba kingine, akaonyeshwa Maua akiwa  amekaa akiwa anawaza, na upande mwingine akaonekana mke wa Bosi akiwa na mumewe, lakini  wote wakiwa wamekaa bila ya kuaangaliana kama walivyokuwa wamekaa hawa wazee mwanzoni….
‘Niliwauliza swali moja awali je mnawakumbuka hawa watu niliowaonyesha awali, achilia mbali hizi familia zenu…?’ kukawa na ukimya, halafu sauti ikatokea na kusema, huyo mzee mliyemuona kwenye picha mnamjua vyema, na kama mungekuwa wacha mungu mngewaombea Baraka kwa mungu, lakini mioyoni mwenu mnashukuru kuwa hawapo dunia hii, kama sikosei ndio wao waliosababisha nyie muwe watu, ndio wao chanzo cha utajiri mllio nao,…je mnakumbuka  mlichowafanyia hawa wazee?...na picha hiyo ya huyo mwanamama alikuwa mke wa huyo mzee, hebu angalieni marejeao hayo tena…’ mara ukutani kukatokea mapicha ya hawo wazee na matukio mengine, ambapo sehemu nyingine walionekana hawa wazee wawilii kwa wakati tofauti wakiwa na hawo jamaa walio-onyeshwa kwenye hizo taswira,…na baadaye kabisa ikaonyeshwa mazishi ya watu….,  kwanza mazishi ya yule mzee mwanaume, halafu ikafuata mazishi ya mwanamke na huku kwa upande wa pili kukaonekana picha  za hawa wazee wawili waliopo humo  kwenye hicho chumba wakisherehekea kila mmoja kwa wakati wake….
‘Hebi niwaulizeni kwanini mlikuwa mnasherehekea, ilikuwa ni siku ya kuzaliwa au? …kama sikosei mlikuwa mkisherehekea kufa kwa hawo wazee niliowaonyesha hapo kabla, nawaita wazee, kwasababu ni watu wa makamo yenu, je inakuwaje watu washerehekee vifo vya wengine…kwani kama mnavyoona ni tarehe ile ile ya mazishi ya hawa wazee, ndipo mlipokuwa mkisherehekea?… najua ni kwanini, na nyie mnajua zaidi yangu kuwa mlikuwa mukijipongeza kuwa kile mlichokitaka mumekipata, nacho si kingine ni utajiri…utajiri wa dhuluma…ingawaje hamukupata ule mzigo ambao mlikuwa mkiutafuta sana, lakini kwa kiasi kingine, kama migodi na vitega uchumi vingine vilikuwa mikononi mwenu……! Kitu kikubwa ambacho mlikikosa ni ule mfuko wa hazina, labda niwakumbushe vyema ule  mfuko  ulikuwaje …’ mara picha ikatokea kijana mmoja akiwa kashika mfuko, na mara picha nyingine ikaonekana akiwa anaufungua ule mfuko na kumimina vito vya thamani, kama dhahabu na alimasi…
Wazee wale walipoona vito vile vya thamani kubwa sana wakajikuta wakihema kwa tama…..hata angekuwa nani angetamani…maana vilikuwa vingii na vinametameta..kuonyesha uzuri wake. Na bila kujijua wakawa wote wameshika midomo yao, nafikiri mioyoni mwao walikuwa wakilaani kuwa kumbe ule mzigo ulikuwepo na walitamani kujua nani anao na ikiwezekana umri urejeshwe kidogo wafanye vitu vyao, ….
‘Najua mna hamu sana ya kutaka kujua nani aliyewahi kuuchukua huo mzigo…labda niwakumbushe kidogo, kuwa mnamkumbuka mtoto pekee wa mzee huwo kwenye hizo picha nilizotangulia kuwaonyesha awali…mnakumbuka kuwa walikuwa na mtoto mmoja, huyo mtoto aliwapotea siku ile, mama yake alipokufa kwa sumu, ambayo mlimtegea nyie wenyewe, nani kati yenu wawili mnajua wenyewe…na mlifanya hivyo ili ionekane kuwa kajiua mwenyewe…basi mtoto huyo kijana  mliyemuona akimimina hizo dhahabu na alimasi ndiye yule mtoto…aliywatoroka siku ile, huyo ndiye aliyekuwa mrithi halali wa mali ile pamoja na mali mliyokuwa nayo sasa,…na sasa anahitaji mali zake ambazo mlizichukua toka kwa wazazi wake, mnatakiwa mumrudishie…lakini kwa vipi, tutayajua haya baadaye…
 Kwa taarifa tu kijana huyo alipata bahati ya kuupata huo mzigo, na hakufanya ajizi , kwa vile mtoto wa nyoka ni nyoka, naye akawekeza, na huo mzigo ukafanya kazi…’ na mara taswira ya jumba kubwa ikaonyeshwa na nyumba nyingine zikaonyeshwa.. ` Na zaidi ya hapo nitawaambia nini zaidi kilifanyika kutokana na mzigo huo…lakini kuna jambo moja kubwa, ambalo nawataka kuwaomba, kama mnavyoona hapo mbele yenu kuna karatasi za mikataba ya hiari, ambayo inataka kurejeshwa mali iliyoibiwa kutoka kwa waporaji kwenda kwa mrithi halali, mkumbuke mliipora kinyume na matakwa ya wenyewe…kwa mhusika,…huo ni mkataba wa hiari, hauhitaji kutumia nguvu, ni kiasi cha kuchukua kalamu na kuandika jina lako na sahihi yako, mengine tutawaachia watu wa sheria…nawaomba sana mfanye hivyo ili kukubaliana na haya niliyoyasema, vinginevyo…mnaona huko juu kuna vitundu vidogo vidogo, hivyo tukivifungulia kutatokea hali ya hewa ambayo haipatani kabisa na hali zenu…mtakufa kifo cha aibu…
Kwanza kabla ya hapo hebu angalieni uchafu wenu wa maisha yenu..’ mara ukutani kukaonekana video za picha za aibu yakiwahusisha hawa wazee, na video nyingine zikionyesha…vikao vya kufanya njama mbali mbali, na hayo kama yatafika serikalini ingekuwa ni matatizo kwao…na wakati yanaonekana hayo huyo jamaa akawa anaendelea kuongea kwa kusema `kwanza angalieni huo uchafu wenu, angalieni hizo njama zenu za kujiunga na kundi hilo , ambalo linajulikana sana hapa duniani…je serikali ikijua hilo mtasemaje, kuwa mnataka kupindua nchi au… na mengine mengi yataendeela kuonekana hapa mbele yenu, ambayo mkikaidi itabidi mengine wayaone familia zenu…hasa huo uchafu wenu, mtasemaje kwa familia zenu, wakati nyie mnajiita watakatifu hamtaki kashifa… sasa jamani tusipotezeane muda, wekeni saini zenuu hapo mkimaliza kuwaka saini zenu …aaa, taratibu milango itafunguka na taratibu mtaondoka zenu na hayo mliyoona hapo yataishia hapa hapa….
Wazee wale kama ilivyo asili yao ya ubishi waliinuka kutaka kuondoka lakini walipofika mlangoni…haakufunguki,…wakaangaliana, wakawaza,  wakajaribu tena kufungua kwa pamoja wakakuta milango imefungwa kama vile awali…na hata  walipojaribu kusaidiana kuuvuta ule mlango kwa pamoja, haukuonekana kusogea ilikuwa kama ukuta umeungana na huo mlango , walijikuta wakianza kuishiwa nguvu, na shinikizo la damu  kuanza kuleta mtafaruku…na hapo wakaisikia jamaa akiwaambia kama wanaleta ukaudi basi,…kwanza kabisa italetwa familia zo ili waoene huo uchafu na baadaye wataonedolewa na adhabu nyingine itakayofuta ni ya gesi ….
‘Mnasemaje wazee….?’ wakaulizwa na wao wakaangaliana, na kugeuza kichwa huku na kule, mara washike kichwa kwa hasira...

NB. Hebu tuishie hapa kidogo kwani huu ulikuwa muendelezo kidogo wa makaribisho ya wageni kwenye jumba hilo,... hoteli hiyo kubwa, ambayo...mmmh, tususbiri tuone, nini kitafuta baadaye, katika mfulululizo wa hitimisho la kisa hiki...
Ni mimi: emu-three

2 comments :

Swahili na Waswahili said...

Moto wawaka mama mootooo wawaka!!Pamoja ndugu yangu ni moto wa kuotea mbali!!!!

samira said...

m3 leo ni ? mambo yamenoga kweli dawa ya moto ni moto m3 umejiunga na facebook hiki kisa kizuri
cant wait