Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, July 4, 2011

Dawa ya moto ni moto-29



   Inspekta alingalia ukutani na kuona zimebakia nusu saa kama alivyoambiwa, na baada ya hiyo nusu saa kuisha ina maana kutaanza kuingia hiyo gesi iliyopo mle itaanza kuvuja na hapo ndipo itakuwa mwisho wa misha yake, …alitizama huku na kule lakini kulikuwa hakuna hata chembe ya sehemu ya kutokea, …alishindwa kuelewa vyema, kwani alifuata kama alivyoelekezwa na yule docta, mtani wake…lakini kilichomshangaza walipoachana pale alimpigia simu na alipomuuliza kuwa yeye atakuwepo huko, alisikia yule docta akiuliza kwa mshangao kwa kumuuliza wapi ..na aliuliza kama hajui nini alichokuwa akiulizwa, na baadaye alimwambia  kama ni kule unataka tukutane nitakuja, lakini mimi sijaamua lolote, na sina mpango huo…
‘Sina, mpango huo…’ docta aliyarudia yale maneno kwa kujiuliza, na wakati anatafakari haya akaona kweli aliingia mtegoni…ina maana yule aliyekutana naye ufukweni sio docta mtani wake, kwani hata yale mazungumzo ya mwisho alihisi sauti kama siyo yake, alikuwa karibu agundua hilo, lakini kwa vile alitekwa na hamasa ya kuingia ndani ya jumba hilo, hakutilia maanani ile hisia yake…kweli sasa kagundua kuwa sio yule docta mtani, yule likuwa docta-mlipiza kisasi…alikuwa kajibadili sura na kuigiza sura ya mtani wake! Inspecta alijilaumu sana, kwani hisia zake zilishamuonyesha kitu lakini akazizarau….
Alijikuta akisema ‘too late…’ hapo akaanza kumuomba mungu, kwani alijua muda wa maisha yake ndio umewadia, hakuamini kuwa maisha yake yataishia katika kifo cha mateso ya namna hiyo. Alikumbuka jinsi alivyowahi kuwaona watu waliokuwa wakifa kwa kifo cha gesi wanavyoteseka, kwanza unaanza kukosa pumzi, halafu….alipofika hapo kimawazo akainuka pale alipokuwa amekaa…akatafakari jinsi alivyoingia mtegoni, kwani alielekezwa kuwa abonyeze kile kitufe cha `lifti’ namba tisa mara tatu haraka,pale tu hiyo lifti itakapokaribia kusimama,halafu kile chumba cha chini aliposimama kitafunguka na kuwa kama kinazunguka, ina maana atakuwa kasogezwa kwenye lifti ya chini, halafu atabonyeza tena namba hizo mara tatu kwa haraka, ile lifti itaanza kushuka chini..ikianza kushuka, ikionyesha tisa kuwa ipo kwenye chumba namba tisa abonyeze ile namba tisa, na hapo tena chumba cha lifti kitafunguka, atoka haraka mle ndani na atajikuta kwenye chumba….asubiri kidogo na wakati anasubiri  mara akajiona anashushwa kwenda chini kwa haraka...hapo akashangaa alijua kuwa katoka kwenye ile lifti..kumbe yupo kwenye lifti nyingine ya kwenda chini, iliyokuwa ikishuka kwa kasi kwenda chini kabisa…halafu mlango wa ile lifti ukafunguka, akatoka na kujiona kwenye varanda, akafuata mishale inayoonyesha kwenda mbele akaifuata na alipofka mbele chumba kilichokuwa mbele yake kikafunguka, akasita kuingia, lakini baadaye akaona aingie tu, alipoingia mlango ikajifunga ghafla, na hapo akasikia kicheko…..
‘Hahahaha umejileta mwenyewe Inspekta, sikujua kuwa ningekupata kirahisi namna hiyo…lakini nakuomba ndugu yangu soma maelezo hapo mbele yako ukikubaliana nayo weka sahihi yako, na kama hutakubalina anayo basi…utayaona yatakayofuta…aliangalia huku na kule, halafau akasoma yale maelezo ambayo yalimtaka ajiunge na hilo kundi na kuahidiwa donge nono, mshahara..na vitu vingi..na kwanini anatakiwa kujiunga, ni kuwa anahitajika sana kwa ajili ya utawalka ujao ambao kiongozi atakayechaguliwa atakuwa na utaratibu utakaowawezesha watu wawe huru, hata kutumia madawa ya kulevya…na mambo mengi ambayo Inspekta yalimtia kichefuchefu akalifunga lile faili na kusema hataki hata kusoma, afanye analotaka kufanya…
‘Napenda sana watu kama nyie..alipofikia hapo kimawazo aliangalia kule juu na kuona muda unavyokwenda haraka akasogea pale alipokuwa na kuruka juu, ili kutafuta uwezekano wa kufikia sehemu ya juu, aliigusa lakini, kulikuwa kugumu sana, na kila tendo alilofanya alisikia jamaa akicheka, ina maana huyo jamaa alikuwa mahali anamuona kila tendo analolifanya huko alipo….akayaangalia yale matundu ambayo aliambiwa ndipo gesi itakapopitia muda ukiisha, aliona vitundu vitundu kwa juu, ambapo ndipo hiyo gesi itakuwa ikipenya  na kuingia mle ndani kwa kupitia juu, kwahiyo hakuna sehemu ya kuikwepea, akajaribu kugonga gonga kila mahala akaona kuwa ni chumba kilichosiribwa kabisa, na kama isingekuwa ile hali ya hewa iliyowekwa mle ambayo nayo kama wataizima basi unakufa kwa hali nzito ya hewa, akatizama hapo kama kuna sehemu yoyote anaweza kubomoa ili apate kupita lakini hakuona hiyo dalili na saa zikawa zinazidi kwenda.
Akakumbuka maneno ya yule jamaa…`inspecta kwanini wewe umekuwa mgumu kiasi hicho, unafikiri ujasiri wako huo utakufikisha wapi , angalia wenzako waliokuwa majasiri kama wewe wameishia wapi kama sio kuitwa tu mashujaa, ..waliokuwa mashujaa…na sasa watoto, au wajukuu zao wanasota maisha ya taabu, kama wangeliwekeza , kama wangelichuma na mali hizoo zikawekezwa, saa hizi wajukuu zao wangelizikuta wakaziendeleza, lakini ipo wapi, …wamekufa na wanzao waliokuwa wajanja wanafaidi nchi….mnaishia kuwaita `mafisadi..’ ndio ni mafisadi, lakini wanaishi, watoto wao wansoma, na mwisho wa siku ndio watakaoshika taifa…wewe utaishia kuitwa `shujaa..’ lakini upo wapi…kama sio udongoni ..!
‘Nimekuwa nikikutafuta kila mara wapi nitakuondoa , maana wewe ni kikwazo kwangu, kila nikipanga mipango yangu nashindwa kwa kuchelea watu kama wewe…sasa angalia hapo ulipo, huwezi kutoka bila ya mimi kufanya mambo yangu huku, ni chumba ambacho hakijulikani kabisa na yoyote zaidi yangu mimi, ni chumba ambacho kila mbaya wangu aliyekataa kutii amri zangu ameishia hapo na ameshasahaulika…sio kwamba mimi ni mbaya kiasi hicho,…cha kuwamaliza watu kama nyie…ila ubaya huo nimepandikizwa na watu wabaya zaidi ya ubaya, na hakuna sheria iliyoweza kuwaadhibu, eti kwasababu ni watu wakubwa, watu wenye pesa, …pesa zenyewe za dhuluma…na uuavyo dhuluma haidumu, sisi tumeamua kuchukua sheria mikononi mwetu, kulipiza kisasai…na wale wanaowatetea hawo wabaya…lazima tuwafagie…
‘Nimekupa dakika nyingi za kufikiri, nimekupa muda wa kutosha wa kuamua sina muda wa kupoteza na wewe,…nina mambo mengi ya kufanya, kuna mambo mengi ya kupanga, ….sasa  na kuaga kwaheri ya kuonana…hapo juu kama unavyoona hiyo mishale ya saa, na dakika zinavyojiandika hapo, hiyo nusu saa ikiisha gesi itaanza kuingia toka juu, na unajua mateso ya gesi,  kesho ikifika  tutakuja kusafisha chumba chetu na kama kuna masalia tutayatuma kwa jamaa zako ili wasikusahau kwenye daftari la mashujaa wa nchi…sina jinsi, …inaniuma sana mtu jasiri kama wewe kufa kwa kifo cha aibu kama hicho..nakumbuka sana tulivyozoeana …lakini nitafanyaje, kama wewe unakuwa kikwazo cha kufanikisha kisasi changu nitafanyaje..kwaheri..’ na mara kukawa kimiya na Inspekta akawa anahagaika huku na kule kutafuta upenyo wa kutokea, lakini alikosa, …na kila dikiak iliyopita ikawa mateso kwake, na hata ikafika muda akaona ni heri atulie ili kutunza pumzi yake ya mwishoi ya kukatia roho…

Maua alipofika kwenye ile hoteli ambapo alitegemea kumuona baba yake akakuta anapokewa na mtu asiyemjua na kuambiwa amfuate huyo mtu, bila ajizi Maua akamfuta, akijua kuwa hoteli hiyo ni ya kimataifa , hakuna wasiwasi, wakaingia kwenye lifi ikabonyezwa namba kwa haraharaka wakajikuta wanazama kwenda chini akashangaa, kumbe kuna eneo la chini kwa chini…na baadaye ikafika mahala ikasimama, lifti ikafunguka na wakatoka na kuingia kwenye chumba,  ambacho aliambiwa kuwa asubiri hapo …akauliza baba yake yupo wapi, akaambiwa asubiri kidogo, ataonana na huyo baba yake  na akakaribishwa vinywaji, lakini hakuwa na hamu kabisa ya kunywa hivyo vinywaji, na akaishia kusoma magazeti yaliyokuwepo humo, na wakati anaangalia ukurasa mmojawapo mara akasikia sauti kutoka kwenye kipaza sauti, na ukutani mwa hicho chumba ikaonekana mwanga kama vile mwanga wa kuangalia sinema, na mara  ikatokea taswira ya mtu kakaa kwenye kiti huku anatabasamu, akasema kwa sauti…
‘Salamu binti mwema, salamu Maua , sina haja ya kujitambulisha maana mimi ni kinyonga, hutaweza kunifahamu, ila kwa matendo huenda ukanikumbuka, najua  mengina utakuwa umeyasahau na hungependa kuyakumbuka, lakini sio mbaya, kukumbushana, kwanza hembu tuanzie hapa, samahani kwa hili…mara ile sura ikaondoka na mbele yake ikaletwa sura…oooh, akashituka na kutaka kudondoka, kwani ulikuwa ule uchafu ambao hakutaka kabisa kuuona, …ile DVD, ….kumbe ni hawa watu, ndio walishirikiana na mume wake…akaangalia pembeni lakini hakuweza, kwani sura ile ilikuwa kama imejaa chumba kizima kila unapogeuka unaiona..na akasikia kicheko kikubwa, labda ni kutoka kwa yule mtu…
‘Usijifanye kuwa una aibu, mbona siku ile hukuona aibu…usijifanya wewe ni mtakatifu kwani habari zako tunazijua kuliko hata wewe mwenyewe unavyofikiria, na zipo zimehifadhiwa…nilishangaa sana ulipoamua kuolewa na yule masikini wa watu…ukamfanya baba wa nyumbani, ni sawa,… hilo ni jambo jema, kwasababu mumetoka naye mbali, lakini ungemheshimu basi…anyway, hayo hayana msingi kwa hapa, usijali sana Maua, kwani licha ya yote hayo, uliogopa sana kuwa utaabika, baada ya tendo hili…haya ni mambo katika kuwekana sawa, ili ujue kuwa upo wapi na watu walio nyuma ya hilo wana uwezo gani…
 `Maua  nakuhakikishia kuwa hakuna baya litakalotokea kama utakuwa binti mwema, kwani wapo watu wanaokujali, wapo watu walio na uchungu sana kuhusu maisha yako zaidi ya huyo unayemdhania na kumuogopa kuwa akiona huu uchafu atakuumbua na kukutupa jalalani..labda umemsahau mama yako…’ mara ikatokea sura ya marehemu mama yake, hapo alionekana akiwa kalewa bwii, na pembeni yake yupo jamaa kasimama pembeni yake, huku kavaa taulo tu…….,baadaye hiyo picha ikaondolewa..
‘Hapa nataka kukumbusha kuwa kuna jamaa mmoja alikuwa anahudumia bustani yenu, huyo alikuwa anahudumia hata kazi za nyumbani, natumai unamkumbuka, huyo alikuwa mlezi mkubwa wa mama yako na wewe, ulipenda sana kumuita `uncle’…huyo ndiye alikujali na maisha yako wewe, kwani kuna siku wazazi wako walikuwa wanagombana sana…wewe ulikuwa ukikimbilia kwa huyo jamaa, …na ugomvi wao  ulifikia  hata wazazi hawa kutamka maneno ambayo nazani kuna siku uliyasikia kuwa huenda wewe sio binti wa baba aliyekulea…hilo ni moja ya mateso ambayo yalimtesa sana mama yako…
‘Nataka nikumbie kuwa mama yako aliteseka sana, lakini alisahau kuwa yeye na mume wake walimtesa mama mmoja zaidi ya mateso aliyoyapata yeye…labda wewe hukuwahi kusimuliwa hayo…ni kuwa baba yako mali zote alizo nazo, alizipata kwa dhuluma, alimwibia baba mmoja, na hata kusababaisha kifo chake..utasema hayo yanakuhusu nini na ilihali yamepita, ila ninachotaka hapa ni kukufahamisha jamii ambayo inaitwa wazazi wako ikoje kuwa baba huyo na mama yako walitenda zambi kubwa sana, kwani mama yangu alikufa sawa sawa kama alivyokufa mama yako…na kitu kilichomtesa zaidi ni pale alipokuwa  akikumbuka kuwa yeye alihusika katika kifo cha mumewe kwa vile aliambiwa mumewe anatemba na kimada, akaamrisha auwawe..akauliwa na  watu wa baba yako ..na hutaamini kimada aliyetegeshewa ni mama yako…
 ‘Usimuone mama yako hivyo ulivyomkuta, alihangaika sana kumfikisha baba yako hapo alipo, ametokea mbali, toka ujanani kujirusha, akaingia mikononi mwa baba yako, na kujifanya mpole, na baba yako alipogundua kuwa anaweza kumtumia, kwasababu hakumuoa kwa upendo ule wa dhati…aliamua kumtumia…hata hivyo hata pale alipomtumia na kufaidika , baba yako alikosa fadhila, akamhujumu,…na haya yote ni malipo ya watu wabaya. Mama yako alikuwa akigombana sana na baba yako hasa alipokuwa akimkumbusha jinsi mama yako alivyojitolea kwa hali na mali kuwezesha, hata kujizalilisha, hata kuua ili  huo utajiri upatikane,….kwasababu biashara ya madini, inagubikwa na ushirikina mwingi, usio na maana, mama yako na baba yako walipitia huko,  lakini baba yako mwisho wa siku alimsahahu mama yako akawa mtu wa tamaa,…
 ‘Maua nakuambi ukweli baba yako alikuwa hata na yumba ndogo ambayo baada ya mama yako kuondoka ndiyo ilishika usukani…hutoamini hilo kwani kila mara ukikutana na baba yako alikuwa akikumbia kuwa eti `hataki kashifa’ kwenye nyumba yake…lakini alikuwa akifanya hivyo  akikumbia maneno ya laana `aliyo achiwa’ kuwa nyumba yake itasambaratika kwa kashifa …kashifa za nini za ngono…akasema yeye atajitahidi kuhakikisha kuwa familia yake haiteketei kwa kashifa kama hizo…kwasababu ana pesa, …ana utairi…, alitamka hayo moa kwa moja kwa mama yangu, pale alipokuwa akimdhihaki baada  ya kumtegeshea  huo ushenzi wao,… walimunyesha mama madawa, wakamtumia wanaume wakamfanya walichotaka kumfanya ili ionekane kuwa ana tabia hiyo, na kumchafulia kwa jamii, kama hatakubalina na matakwa yao…..’ mara sauti ile ikawa kama imepotea.
‘Kila nikiwaza hayo hasira inanijia na ndio maana nawafanya yale yale waliyowafanyia wazazi wangu, na hata hivyo nashindwa  kukibuni kifo cha wazandiki hawa kiwe cha namna gani….lakini mama yako alikufa kwa mateso makubwa, kama ulivyoshuhudia wewe mwenyewe siku ile ya mwisho wake…lakini kabla ya hapo mara nyingi mimi nilikuwa naye bega kwa bega kuhakikisha hapati shida sana…hahahaha..hakuwahi kujua kuwa shida nyingine nilikuwa mimi namtegea kiaina..mimi ndiye niliyekuwa nikimchukua picha zake akiwa kalewa akiwa anahangaika…na kwa picha hizo zikawa zinatumiwa kumtishia kuwa kama asipotoa pesa picha hizo ataonyeshwa mume wake….!
  ‘Kama nilivyokuambia kuwa mama yako alijitolea wakati mwingine ili kufanikisha matakwa ya baba yako…sasa yale tuliyapata tuliweza kuyafanyia ujanja mwingine ikaonekana kama vile vile alivyokuwa akifanya enzi hizo za ujana wake.., na tukamtishia kuwa hayo mabaya waliyoyafanya yeye na mumewe asipotimiza masharti yetu tutayapeleka kwenye sheria na anajua nini kitafuta baadaye , kwa kuogopa, na kwa kumpenda mumewe ambaye alikuwa hana mapenzi naye, akawa anayameza yeye mwenyewe hayo machungu na kuhangaika kutoa pesa, hata kwa kumuibia mumewe ili hayo yaishie kienyeji …yakawa hayaishi, ..of-course sio mimi nilikuwa namuamba moja kwa moja ila watu wangu walimuonyesha hayo…mama yako alipoona vile presha juu, akafuata masharti yetu, akawa anata pesa nyingi…mpaka baba yako akamshitukia na kuhakikisha kuwa hapati tena nafasi hiyo ya kuchukua hela zake ovyo!
Sisi tulimtishia kuwa asipotoa mabilioni ya hela mkanda huo utaonyeshwa dunia nzima, na hata kwa hawo wanaomuheshimu kama mama wa upendo. Unakumbuka mama yako alipata sifa ya mama wa upendo, analea mayatima, anajenga mashule…sasa fikiria picha kama hiyo ionyeshwe  dunia nzima, unafikiri ange-elewekaje…alitamani dunia ipasuke amezwe, lakini wapi…ilibidi ateseke kama alivyoteseka mama yangu …yule mama waliyemfanyia vile ili wapate mali yake na mumewe…na kisasi kikamfuata nyuma nyuma…mpaka akaamua kunywa kupitiliza…
Mara picha ya mama wa Maua ikaonyeshwa jinsi alivyokuwa akilewa, na mara anaonekana mwanamue mmoja akimbeba na kumpeleka hadi chumbani, na mara anaonekana jamaa huyo akiwa na taulo…hili lilimpa mawazo sana Maua kwanini jamaa huyo mara kwa mara mwishoni anaonekana akiwa pembeni yake akiwa na taulo tu…
‘Nafikiri utashangaa sana kila mara unamuona huyo jamaa anakuwa pembeni mwa mama yako, ni kuwa huyo jamaa ndiye aliyehakikisha kuwa kila kitu kinakwenda safi…na nikuambie jambo moja mama yako alipokuwa akilewa, alikuwa anakuwa na hisia kali sana, …hahaha hisia hizo aliyeziwezea  ni huyo jamaa anayeonakena na taulo…hapo anaonekana akiwa na taulo baada ya kazi nzito…hahaha…hebu mwangalie viuri sura yake…utamua ni nani…na baada ya hilo kesho yake mambo hayo anaonyeshwa mama yako na watu wangu, …nini kinachofuata, kama sio kunywa zaidi na zaidi na hata siku moja alitaka kujiua, lakini hatukutaka afe haraka kwani tulikuwa tunahitaji mali ile waliyoiba irejee kwa wenyewe…sio siri alitoa hela nyingi,..hata baba yako alipomshitukia na kuhakikisha kuwa hampi hela tena, …sisi tukabuni mbinu nyingine, tulipandikiza watu wetu kwenye makampuni yake…!
`Maua sitaki kukumiza sana, ila kila mara tulikuwa tunakulinda , kwasababu wewe hukustahili kupata mateso ambayo hayakuhusu…’  Hapo Maua aliwaza, kwanini yasimhusu naye ni familia ya watu hawo wanadaiwa kuwa walikula hela za watu…
‘Wewe ulizaliwa hapo kwa bahati mbaya…bahati mbaya…nitakuambia baadaye kuwa ulizaliwaje hapo kwa bahati mbaya…, subiri kwanza tukamilishe mambo mengine….mara ule mwanga ukazima na kukawa kimiya, na Maua akajikuta anahema, …karibu apoteze fahamu huku akilaani kuwa kama atabahatisha kukutana na huyo shetani, atahakikisha anamkata kichwa chake…lakini kwa vipi, kwani alipojaribu kufungua mlango wa kile chumba alikuta kimefungwa..

NB, Nimeona niishie hapa kwa leo katika muendelezo wa hitimisho la kisa hiki,  ili tuapte muda wa kutafakari zaidi,...mambo yanakuja bambam...tuzidi kuwa pamoja, na kama kuna sehemu nimesahau, naomba tukumbushane ili hitimisho likusanye kila kitu!

Ni mimi: emu-three

4 comments :

Simon Kitururu said...

MKU lete tu mambo bambam!
Mie nipo!

samira said...

mambo mazuri m3 uhondo

EDNA said...

Kazi nzuri jirani yangu,usione kimya wakati mwingine huwa tunapita kimyakimya.Pamoja.

Anonymous said...

Jamani kwanini usitoe kitabu ili tununue na kufanidi huu uhondo moja kwa moja Best!!!!!!!!!!!!!!!!