Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, July 21, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-3



   Ilikuwa saa sita za usiku wa mwezi wa tano mwaka 1996, na pamoja kuwa katikati ya usiku ukitaraji kuwa pilikapilika nyingi zimepungua, bado kulikuwepo na magari yakipita hapa na pale, na hata walionekana watu wachache na baadhi yao wakitembea kwa miguu…na mara kwa mbali ikaonekana taksii ikija na kusimama mbele ya nyumba mojawapo, iliyopo karibu na barabara, na wakateremka watu wawili kutoka kwenye ile taksi, ambao walionekana kama ni wapenzi, kwa jinsi ya matendo yao, walipotoka tu wakawa wameshikana mikono na kukaribiana zaidi na baadaye  kila mmoja akazungusha mkono kwenye kiuno che mwenzake huku wanatembea kuingia kwenye ile nyumba!
‘Kweli hawa ni wapenzi..’ akajisemea mgambo mmoja aliyekuwa akiwaangalia kwa hamu
Wawili hawa walikuwa wametoka kwenye moja ya sherehe za jamii, na walikuwa wameburudika vya kutosha na kila mmoja alikuwa na hamu ya kujitupa kitandani kupumzisha viungo baada ya kurukaruka huko ukumbini, na kuisubiri siku ya kesho yake ambayo wengi wanaitambua kama ni siku ya kazi. Na sherehe kama hizi zilitakiwa zifanywe siku za mapumziko, lakini hii ilikuwa maalumu ilifanywa siku za kazi…! Walipoingia ndani wakawasha taa, na hawakutaka hata kutulia kwenye varanda, au chumba cha maongezi wakafulululiza moja kwa moja hadi chumbani, na kusarura nguo zako kama watu wenye hasira nazo..,
‘Sitamani chochote zaidiya usingizi…’ akasema mwanamama
‘Yaaani hata mimi mumeo hunitamani..’ akasema Mwanaume
‘Yaani wewe nisikutamani, ninaposema usingizi sio maana kulala tu, ni kulala na wewe na najua nikiwa karibu na wewe ni raha tupu…nakutamani sana mume wangu, haya tulale maana hata hivyo nakuonea huruma kuwa ulihitajika kupumzika ili uwahi kesho kwa ajili ya safari yako…’ akasema mwanamama, na mwanamume hakujibu kwani alikuwa akivua viatu vyeka huku akiwa anawaza mengi kuhusiana na safari hiyo, halafu akasema.
‘Safari ya basi hadi Mwanza, nikitoka hapo kuna kazi kidogo pale Mwanza kwenye ofisi yetu ndogo, nikimaliza pale kuna kupanda meli hadi Bukoba, na huko kuna ofisi yetu ambapo natarajiwa kukaa muda kidogo halafu nitarudi tena Mwanza kumalizia kazi kabla ya kurejea Dar, ooh, mbona `nitakumiss’ mahabubu wangu, mwezi mzima …bila kuwa na wewe itakuwa adhabu kubwa sana…’ akasema mwanaume
‘Hata mimi sijui nitaishije, maana tangu tuoane hatujawahi kutengana kwa kupindi kirefu kama hicho, huwa uansafairi unakaa siku mbili na tatu ni nyingi, lakini mwezi mzima, mmmmh, sijui nitaishije, na unasamea unatakiwa kupanda meli, meli yenyewe inaitwaje? Akauliza mwanamke
‘Inaitwa MV Bukoba, ni ya siku nyingi kidogo, kama sikosei iliundwa au ailinunuliwa mwaka 1979 nimeshaipanda mara nyingi, kwahiyo naijua vyema, hata nikiwa mle ndani najua wapi niende, wapi pananifaa, na mara nyingi mimi napenda kukaa nje, nikiangalia samaki…na nikuwa kule sina wasiwasi wa kupata tiketi kwangu pale ni rahisi sana kwani wameshanijua…’akasema mwanaume.
‘Kama ni ya zamani ina usalama kweli, maana ya zamani ilitakiwa upumzike au ifanyiwe marakebisho ya mara kwa mara, lakini nijuavyo watendaji wetu wanaweza kuzarau kufanyia ukarabati wa mara kwa mara…na kwa mfano mkiwa kwenye maji inakuwaje maana mimi sijawahi kusafiri ndani ya maji, ikatokea balaa, mnajiokoaje kama huwezi kuogelea itakuwa vipi…’akuliza mwanamke.
‘Kuna makoti(majaketi) ya kuvaa, lakini kwenye meli kama yetu hiyo kama yapo ni machache, ukiyavaa yale huwezi kuzama, tatizo ni watu wengi wanaopanda mle, …kama sikosei wanaweza kufikia hata mia sita hata na mia saba…sasa fikiri hayo makoti ya kuwatosha …sijui kama yapo, inatakiw yawepo, lakini mle sizani…cha muhimu ni kuomba mungu mfike salama…hata kama unajua kuogelea vipi kama limetokea la kutokea utaogelea vipi mfano ni katikati ya ziwa, uanze kuogelea hadi mwisho mmh, sijui kama mtu utaweza…labda wapo wanaoweza maana unazungumzia eneo la umbali wa kilometa elifu 60 na zaidi…sina mahesabu sahihi, lakini labda ni hivyo au zaidi..sasa ikikukuta hata kama unajua kuogelea, utahitaji uokozi wa haraka, kabla hujachoka……hayo ya safari tuyaaache tuwaze yetu mimi na wewe …au sio, nakupenda sana mke wangu, ….nakumbuka nimekuambia nataka Baraka zako…’akasema mwanaume.
‘Baraka mbona nimeshakupa nimeshakuombea sana, na nikasema nakuombe safari njema, au unataka Baraka ya namna gani…..hahaha, na wewe bwana…hiyo mbona ni kawaida, kumbe nayo ni baraka…’akasema mwanamke huku akicheka kimahaba na kuwamgalia mume wake machoni,
‘Hiyo ndio Baraka ya ndoa, sio kuomba tu, baraka ya ndoa ni ile uliyofundwa kwa wazazi wako, ile aliyotuagiza mola…hebu sogea huku univue hili shati maana hivi vifungo vinanipa shida na kunichelewesha…mmh, ina maana hata kuoga hatuogi leo maajabu maana wewe kila siku lazima mtu aoge kabala hajalala, leo unanishangaza kidogo…., lakini nitaoga  kesho asubuhi…’ akasema mwanaume, ha hapo yulei mwanamke akaja kumvua shati, na kusema  ‘ukipanda kwenye meli hakikisha unaliwahi hilo koti la kuogelea, usilete mazaru yako,…usiseme kuwa umezoea kusafiri…na kwa leo unahitajika kupumzika ili uwe na nguvu ya safari..’
‘Hayo ni ya safari , ya leo ni mimi na wewe, …ni kweli mke wangu nahitajika kujipumzisha kiukweli lakini pia nahitaji baraka zako, unajua mke na mume wakiwa pamoja kwa mapenzi ya raha ni baraka na kila utakalolifanya likiwa ni kwa mapenzi, mnakuwa mnapata thawabu…na ni vyema mmojawapo akiwa kwenye safari kupeana baraka za mapenzi ya ndoa , kwasababu safari ni hatua…’ akasema mwanaume.
‘Nawe umeanza sipendi hii kauli yako ya kila mara ukisafiri, unapenda sana kusema `safari ni hatua..’ unajua kauli hii mimi inanitia uwoga fulani…’akasema mwanamke.
‘Huo ndio ukweli…mke wangu, hata kama kwa udhaifu wetu kama binadamu hatupendi kauli hiyo, lakini hebu tujiulinze  kwa dhati hivi kweli tuna mamlaka gani mbele ya Mungu, yeye ndiye muamuzi na anajua ya mbele yetu sisi hatujui zaidi yetu na hatujui yeye kapanga nini kitokee, hata leo hata kesho hata lini, na kwa vile mtu unasafiri mbali, kwa kutumia vyombo vya moto, unatakiwa ujiandae kwa hilo…sina nia mbaya ya kukutisha, ila ninachosema nataka Baraka za penzi lako…’ akasema na kumvuta mkewe karibu yake miili yao ilipokutana walijisahau kabisa kuwa walikuwa wamechoka na hata usingizi haukuhitajika tena.
‘Namshukuru sana mungu, …’ Maua akasema maneno hayo baada ya baraka kutolewa ,na sasa wakiwa wapo tayari kwa usingizi  huku moyoni akisema sasa ameridhika kuwa kweli kaeshampatia baraka zote mume wake
‘Nikuulize mke wangu kwanini mara nyingi unapenda kutamka maneno hayo kila mara tunapokuwa pamoja na kila baada ya raha hii uliyonipa..’ akauliza mume mtu huku akiwa kainua kichwa akimtizama Maua usoni.
‘Kwasababu nina uhakika najua kiukweli kuwa nakupenda, kwasababu wewe ni kila kitu kwangu, kawasababu..sijui nisemeje, na sijzanii kuwa kuna mwanaume mwingina moyoni mwangu zaidi yako, na sijui kama huo mwezi nitaweza kuvumilia bila kuwa na wewe,  na sijui, sijui….nashindwa kujua jinsi gani itakavyokuwa nikibakia peke yangu, lakini kwa vile yote ni kazi na sisi tunahitaji kula , na asiyefanya kazi hatakiwi kula, …na kwa vile tunahitaji maendeleo, haina jinsi, nakubali usafiri, na nakuombea Mola akulinde uende salama na urudi salama…’ akasema mke mtu huku machozi yakimtanda machoni, hakujua ni kwanini leo itokee hivyo.
‘Maneno akageuka akilaza kichwa kitandani na huku keshaanza kuutafuta usingizi na macho yaliyoanza kusinzia yakamwangalia kwa pembeni mkewe na kusema `Amina’, na kabla usingizi haujamjia vyema kumbukumbu kama ndoto zilimtanda kichwani akiwaza jinsi alivyofanikiwa kumpata huyu mrembo, huyu mke mwema, na kumbukumbu hizo zikawa zinakwenda kama ndoto ya matendo utafikiri ndoto ya kweli, zikianzia siku ya kwanza alipokutana na huyu binti, ambaye alikuja kuwa mke wake wa kweli…..
                                                                         ***********           
Mvua ilikuwa ikinyesha, na mvua hapa Dar-es-salaami inaogopwa kuliko magari, basi watu wakaanza kukimbizana kuwahi kwenye vibanda vichache vilivyopo kwenye vituo vya mabasi na hata yule aliyewahi bado alijikuta akipata shida, kwani mvua ile ilikuwa ya upepo na ilikuwa ikiingia hdi kwenye hivyo vibanda.
Katika kimbizana hii, akaonekana binti mmoja mrembo, naye akiwa kaitika heka heka hizo za kukimbia, lakini vile viatu alivyovaa vikawa vinampa shida, na mkononi alikuwa na begi la kisichana na mkono mwingine alikuwa kabeba daftari na kitabu ikionekana kuwa labda alikuwa katokea kusoma maktaba, na hapo Posta Mpya alipitia tu akiwa kwenye office zinazota mafunzo mbalimbali …na katika kuikimbia mvua, kakijitabu kidogo kakamtoka na kudondoka bila ya yeye kujua na jamaa aliyekuwepo nyuma yake akakiwahi kukiokota kabla hakijalowana, lakini alipoinuka kumpa akakuta huyo dada akwa nagombea kuingia kwenye basi…!
Ni wakati anapanda hilo basi, na kwa vile mvua  ilikuwa bado inanyesha watu walikuwa wakigombea kuingia ndani ya basi ili wasilowane, yule dada aliyedondosha kile kijitabu cha kumbukumbu naye alikuwa miongoni mwao akiharakisha aingie ndani ili asiendelee kulowana, na ikiwezekana apate kiti, nab ado akiwa hana habari kabisa kuwa kapoteza kakijitabu ambacho kwake kilikuwa na thamani kubwa , kwani ni kitabu cha kumbukumbu(diary) ,na kama angelijua ingebidi akatize safari kukitafuta, na wakati yupo kwenye pilika pilika za kusukumana ili aingie ndani ya basi mara akashituka  mtu akimshika bega…
‘Nani huyu tena ananishika began i kabaka nini….’akasema kimoyomoyo, kwani huku Dar-ukishikwa begani ni lazima uwe mwangalifu kwani ni mtindo watumiao baadhi ya wezi, hasa kwa wanaume wanaopenda kuweka pesa au simu kweny mfuko wa shati, ukiguswa begani ni lazima utageuka kumwangalia huyo aliyekushika bega, ukigeuka tui mtu mwingine aliyepo mbele yako au upende mwingine wa bega lako ambapo ndipo kwenye mfuko haraharaka anatumbukiza mkono kwenye shati lako na kutoa kilichopo, kwahiyo hata huyu msichana alishasikia hadithi hizo na kwa vile alikuwa kavaa shati ambalo lilikuw lina mfuko, na mfukoni hakukuwa na kitu cha muhimu zaidi ya leso yake aliyokuwa kaiweka baada ya kujifuta majimaji ya mvua, hata hivyo hakuwa anataka kugeuka, ili asionekane hajui hizo mbinu….
‘Samahani dada Maua nina mzigo wako…’ akasikia sauti ikiita jina lake nyuma yake ambapo watu walikuwa wanamsukuma aingie ili na wao wapate nafasi ya kupenya, kuingia ndani…na wakati huo huo anaitwa jina lake alikuwa kaeshapata nafasi ya kuepenya ndani ya basi hakutaka kabisa kurejea nyuma tena, kwahiyo hakumjali kabisa huyo anayemuita, hasa baada ya kugoma kugeuka pale aliposhikwa bega  kwa kujihami, lakini sasa aliona huyo kama ni mwizi kazamiria kweli na kaja mbinu nyingine za kumuita jina, `hilo limegonga ukuta  pia’ akasema kimoyomoyo , kwani alishaambiwa pia na shangazi yake kuhusu hizo mbinu za kuitwa majina, lakini hata kama ni mtu anayemfahamu asingediriki kurejea nyuma tena na mvua ilikuwa inanyesha kwa wingi nje na ina maana akalowane…  hapana….
Ni wakati keshapata kiti ndipo wazo la kumtafauta aliyemuita lilipomjia akawa anachungulia nje ya lile basi kama atagundua sura ya mtu anayemfahamu, huenda ni mmoja wa jamaa zake, kwani itakuwaje mtu huyo amtaje mapaka jina lake, kwahiyo lazima ni mtu wa karibu kama sio kibaka aliyebahatisha jina lake. Alikumbuka maonyo ya shangazi yake kuwa akiwa mjini asibabaishwe na watu, kwani wapo wengi wanaoweza hata kukusia jina lako, na akikuita ukiitika tu, basi kila ulichonacho mfukoni kimeibiwa…akacheka akisema hawataniweza mimi, hizo kama ni mbinu zao nimezigundua mapema mimi ni mtoto wa mjini, na kama ni imani za watu tu, na zishindwe kabisa!
Alipoona kwa nje hakuna mtu anayemfahamu akageuza shingo kwa ndani na kukagua sura za watu kwa macho ya kujiiba kama atangundua mtu yoyote anayemfahamu, lakini wote aliowaona humo ndani walikuwa na sura ngeni kwake, akaona labda kuna Maua mwingine aliyekuwa akiitwa sio yeye, kwahiyo hana muda wa kuchunguza chunguza watu ngoja ajitulize kwenye kiti chake na wakati anainama kupekua kitabu chake alichokuwa kakishikilia awali na kuangalia `diary’…akiwa na lengo la kuweka hiyo kumbukumbu…huwa mara nyingi haachani kabisa na hichoo kijitabu chake kwa ajili ya kuweka kumbukubu za matukio…, mara akasikia sauti ya mtu nyuma ya kiti akimgusa tena bega..hehehe, huyo tena,..mungu wangu mbona ninaye…akajikuta akisema kimoyomoyo
‘Samahani dada natumai hiki kijitabu ni chako…’sasa hivi akibidi ageuza kichwa kumwangalia huyu mtu na hicho kijitabu anachoambiwa kuwa ni chake, ….haa, alishituka kuona ni kile kijitabu chake, kwani pamoja na kumbukumbu za matukio anayoandika hapo, pia kulikuwa na kumbukumbu zake binafsi ambazo hakutaka mtu mwingine azisome, akakichukua haraka mikononi mwa huyo mtu, kama vile anambekua, na harakaharaka akakitumbukiza ndani ya lile daftari lake kubwa, halafu akageza kichwa kumwangalia huyo aliyempa hicho kijitabu..
Sijui kwanini alijisikia vile, ilikuwa kama mshituko ambao hajawahi kujisikia kabla, akawaza moyoni ni kwanini, mbona kajisikia kama moyo ukimlipuka, na imetokea pale macho yake yalipokutana na huyu jamaa, ina maana labda hiyo sura alishaiona kabla, na hapo alikuwa akimfananisha,au ni kitu gani kimemshika hadi kushituliwa kiasi kile , akageuka haraka na kujifanya hakuna lolote, na alipotulia akiwaza akaona ageuke tena ili ajifanye anamshukuru, na ikiwezekana amwangalie vyema ni nani huyo, au alishawahi kumuona kabla…
Alipogeuka macho yake yakakutana tena na yule jamaa, kwani hata huyo jamaa alionekana kama kashikwa na mshangao fulani, na Maua aliposema anashukuru kwa kumuokotea kijitabu chake, na yule mvulana hakuchelewa kumuuliza; `mbona nahisi nimeshakuona mahali, au ninakufananisha tu?’
‘Labda, ..mimi sikujui kabisa…labda kama umeniona mahali, lakini mimi sikumbuki kabisa, au nikumbushe uliniona wapi….? ‘ Maua akajitahidi kuongea, akijua hizo huenda ni mbinu za wanaume kuanzisha mazunguzo yao, kwani sio mara ya kwanza kusikia kauli kama ile….lakini wakati ule moyo wake ulikuwa ukienda mbio sio kawaida.
‘Maua ni jina lako hasa au ni a.k.a yako, nimeona hilo jina hapo juu ya kakitabu kako, kuna picha yako pia nzuri kama wewe mwenyewe na hilo jina linaendana sawa sawa na wewe, …!’ akasema kama anauliza yule jamaa
‘Yote mawili ni sawa tu kwangu, …’ akasema Maua na akashangaa yule mvulana akihama kiti cha nyuma alichokuwa kakaa na kuja pale alipokuwa  Maua, kwani abiria aliyekuwa kaka naye alikuwa kateremka, na kiti  kilibakia wazi, na hapo mazungumzo yakaanza na kuanza kuzoeana, kidogokidogo na Maua alishangaa,kwanini aliweza kumzoea yule mwanaume kwa muda mfupi sana, wakati mara nyingi hana tabia ya kuzoeana na wavulana akaanza kuogopa, kuwa sasa anaanza kuingia kwenye mitego ya wanaume na kama akijua shngazi yake atafinywa masikioo mpaka yavimbe…shangazi yake hajali kuwa sasa yeye ni msichana, ukikosea unafinywa kama mtoto mdogo, hata kuchapwa..
‘Hilo jina lako ni zuri linafanana kabisa na wewe nafikiri wazazi wako waliamua kukuita hivyo baada ya kukuona sura yako…’ akasema yule mwanaume, na mara basi likafika sehemu ambayo yule mwanaume alitakiwa kuteremka, na akaagana na yule msichana baada ya kumwambia wapi anaishi na sasa anasoma kozi ya komputa mjini. Maua hakukumbuka kumuulizia yule mvulana jina lake,  akasema moyoni kama atakutana naye siku nyingine atamuulizia…na kweli siku ya pili yake walikutana tena, na ikaanza kujenga mazoea a kukutana mara kwa mara….
‘Muhuja, kwanini wamekuita jina hilo, na sikumbuki kulisikia kabla…’akasema Maua
‘Labda nipo tofauti na wengine, lakini kwa kikwetu,Mhuja ina maana ya `mpole’ nahisi wazazi wangu waliniona kuwa nitakuwa mpole ndio maana wakaniita hilo jina…’akasema Mhuja.
‘Hivyo wewe ni mpole, na huo upole utakuwaje…maana mimi nakuona mchangamfu tu…’ akasema Maua.
‘Kuna tofauti ya upole na uchangamfu, mtu unaweza ukawa mpole, lakini inapokuwa ni wajibu wa kuongea, unaongea, lakini sio kwa uchakaramu wa watu ambao sio wapole….’ Akasema Mhuja.
 Siku moja Mhuja alipofika kazini akaambiwa kuwa atapewa gari la kazini kwa ajili ya kazi na usafiri wake wa kwenda nyumbani, alifurahi sana, kwani aliona amelipata hilo gari wakati muafaka, na alipokabidhiwa ufunguo jioni yake, na kwa vile ilikuwa jioni wakati wa kuondoka, akaona ampitia Maua pale anaposomea kozi yake ya komputa. Alipofika akaambiwa Maua katoka kidogo , ikabidi asubiri, na baadaye kidogo akamuona Maua anakuja huku kashikana mkono na jamaa mmoja na walivyokuwa wakiongea, ilionyesha moja kwa moja kuwa wale wanaojuana na jinsi walivyoshikana ni kama wappenzi wa siku nyingi…
‘Oh, ina maana Maua ana mchumba wake, na nilidhania kuwa atakuwa wangu,…kweli sina bahati, kumkosa huyu binti ninauta sana, akasema Mhuja na kurudi hadi pale aliposimamisha gari lake na kuanza kuingia ndani ya hilo  gari ili waondoke na hakutaka kukutana na Maua tena, na mle ndani ya gari alimuacha mmoja wa wafanyakazi wa ofisni kwao ambaye wanaishi njia moja, na alishamuelezea kuwa anakwenda kumchukua msichana mmoja.
‘Mbona umerudi peke yako na ulisema kuwa kuna msichana unakuja kumchukua..?’ akauliza yule mfanyakazi mwenzake.
‘Aaah, achane naye, nilizani nimepata ndege kumbe ndege ana mwenyewe, ngoja tuondoke zetu maana ..’ aliguna akiwaza alivyowaona Maua walivyoshikana na yule jamaa ilionyesha dhahiri ni wapenzi wa siku nyingi, akakumbuka kuwa  aliwahi kumuuliza  Maua kuwa ana rafiki yoyote wa kiume na Maua alimwambia kuwa hajawahi kujiingiza katika mambo ya urafiki na wavulana, ingawaje wengi wanamfuata fuata…hivi ile kauli yake ilikuwa ya uwongo…mbona aliongea kuonyesha kuwa ni kweli…, au…akatikisa kichwa na kusema kama ndio hivyo, basi huenda ana tabia ya uwongoo na mtu kama huyo hatamfaa katika maisha yake, na kabla hajakaa vizuri kwenye gari , mara akasikia jina lake likiitwa, na alipogeuka akamuona Maua akiwa na yule jamaa.
‘Vipi nimesikia kuwa umekuja kunipitia , …nimeangalia huku na kule sikuoni, bahati nzuri yule mlinzi kanielekeza kuwa kakuona ukiingia kwenye hili gari, leo umekuja na gari..?’ akasema Maua huku akiwa kashikana mkono na yule jamaa, na Mhuja alitarajia kusikia akitambulishwa kuwa huyu ndiye mchumba wa Maua na hapo angelifunga kitabu cha kumjua huyo binti …
‘Huyu ni binamu yangu, wanaelekea Zanzibar na mkewe, mkewe anafanya `shopping’ kidogo, binamu huyu ni rafiki yangu, na….’ akasita kuendelea na yule binamu akamnyoshea kidole  Maua na kusema, `acha utani wako, ina maana sasa unataka kunikimbia mimi, …sikubali…rafiki rafiki rafiki gani huyu, mbona hujatutambulisha…..’ halafu wakacheka, inaonekana walizoeana sana.
‘Sikukimbii binamu mimi na wewe tena binamu nyama ya hamu…’ akasema Maua, na ghafla akatokea mwanadada mmoa akiwa kashika mifuko miwili ikiwa na vitu, kuonyesha kuwa alitokea dukani, akamkabidhi yule binamu yake mfuko mmoja halafu mwingine akampa Maua na kwambia hiyo ni awadi yake, Maua akashukuru na maongezi kidogo yakatokea na yule mwanadada akasema wao wanaondoka kwani wanaweza kuchelewa, ikawa nafasi ya kuagana kwa wanandugu hawa, na kabla hajaondoka yule binamu akageuka na kumsogelea Mhuja akasema
‘Bwana, umesema nani vile, …Mhoja au mhuja, vyovyote iwavyo, nakuomba sana unitunzie hii ngoma yangu’, akamshika Maua begani kama kumkumbatia vile, `maana ni mtu wangu, nampenda sana, sasa usije ukajitia unampenda kwa lugha za kiujanja, mimi ni mkali wa watu kama hawo, ila nauliza urafiki wenu ni rasmi au ni wa njiani tu, sitaki kabisa tabia  ya urafiki wa njiani, unasikia Maua’ akamwangalia Maua kwa macho ya ukali utadhania sio yule waliyekuwa wakitaniana kabla, halafu akamgeukia tena Mhuja na kusema, `huyu ni binti yetu tunataka akulie katika mazingira ya heshima, …’akaongea kama mtu mzima, halafu akatabasamu na kugeuka kuondoka na Mhuja alielewa hilo akatabasmu tu, kwani hawakuwa wameongea lolote na Maua kuwa wao ni marafiki wa namna gani , ila ilikuwa ipo moyoni ikitafutiwa siku.
‘Usiwe na shaka  Maua, hata mimi nafahamu hilo, nakuhakikishia kuwa mimi sio muharibifu..’ akasema Mhuja na akamshika Maua mkono kumpandisha kwenye lile gari, akimfungulia mlango wa nyuma, yeye alikaa mbele na yule mfanyakazi mwenzao hawakuongea mengi ndani ya lile gari, na kama waliongea ilikuwa mazungumzo ya kawaida tu…
 Walimshusha yule mfanyakazi alipofika eneo lao na Mhuja akabakia na Maua na Maua likuwa wa kwanza kuongea kuhusu wao akasema ‘Binamu yangu yule bwana ni mcheshi kupita kiasi anaweza akakuumbua mbele za watu maana atakutania weee, atakushika, yaani  familia yetu tumemzoa sana kwa ucheshi wake , lakini wakati mwingine sipendi tabia yake ya kushikana mbele za watu…’akasema Maua!
‘Mimi nilishaaanza kuona wivu na kiukweli nilipona mlivyokuwa mumeshikana nilijua kabisa huyo ni mchumba wako, na nilishaamua kujiondokea nikijua ndege alikuwa na mwenyewe, maana mimi sipendii kuingilia kabisa mapenzi ya watu wengine, siunajua tena mimi ni `mpole’ sijui kugombana na watu…’ akasema Mhuja.
‘Mhhh, eti wivu, kwanini wivu…acha utani wako usiseme umeshaanza kuwaza hayo,…wewe kwanza  hunijua zaidi kama nisivyokujua wewe, hayo ya …wivu yametoka wapi, mbona umeenda kasi sana.. kukutana siku mbili tatu hizi, wewe usiniletee balaa kwa shangazi yangu…hataki kabisa mambo hayo…’ akasema Maua.
Hapo ndipo ambo yalipoanzia na hata kumpa Mhuja nafasi njema ya kujieleza na kutoa ombi, kuwa wakutane siku ya kesho yake ili waongee kwa mapana. Na kesho yake Mhuja akamuomba Maua kuwa anataka wawe zaidi ya mrafiki yaani wawe wachumba Maua alimwambia anahitaji muda wa kufikiri ombi hilo, lakini moyoni alikuwa keshamkubali kuwa kama ni kuwa na mpenzi huyo ndiye anayemfaa, kwani kwa siku hizo walizokutana naye na jinsi alivyomuona alijua kabiisa huyu mwanaume ndiye anaye mfaa, hakutaka kumfahamisha shangazi yake mapema, hadi familia ya Mhuja ilipokuja kujitambulisha, na kweli mambo yakaiva na baada ya miezi sita hivi ndoa ikapangwa na watu wakaoana…
                                            ************
  Mhuja akiwa wametoka kwenye ndoa, na bint I mrembo, ambaye hakuonekana vyema, lakini alipomtizama kwa makini akagundua kuwa ni Maua, wakawa wamesshikana mikono kuelekea nyumbani kwao,, lakini cha ajabu walipofika nyumbani, mara akamuona Maua akirudi kinyume nyume na yeye akipeperushwa na upepo, hata kila walivyojaribu kusimama ili wakutane ikawa haiwezekani…ikashindana na wakawa wananyosha mikoni ili ikutane lakini upepo huo ulikuwa mkali sana…hee sasa vipi mtu nimemuoa tunataka kuingia ndani upepo unatuzuia, akajikuta akisema na kabala hajapata jibu akafumbua macho kumbe ilikuwa ndoto, kumekucha, akainuka pale kitandani na kuangalia saa, akaona ni muda wa kujiandaa kuondoka.
Mkewe naye akaamuka wakafanya maandalizi yote na hatimaye wakaagana, hapo ilikuwa haizuiliki , Maua alijikuta akitoa machozi, na hakutaka kumwachia mume wake aondoke, lakini haikuwezekana mwishowe akaubali akisema `Oh, ina maana ndio unaondoka, ukae mwezi mzima,…haya ukifika usisahau kunipigia simu…’ na ukumbuke siku hizo simu za mikononi zilikuwa hazijaenea sana, kwahiyo alitaraji simu za kibandani, na Mhuja akasema, haina shida nikifika nitapiga simu kwa Maneno, na kama utapata nafasi unaweza kufika pale kazini, ili tuongee, kwaheri , na Maneno najua ni rafiki yangu mwema, atakusaidia kila liwezekanavyo nimeshaongea naye, usijali mwezi mmoja sio mbali sana, na…ukae salama ..’ akasema Mhuja huku naye akijizua alishangaa kwanini leo kajisikia hivyo, mzito kuondoka na hakutaka kumwacha mkewe, aliwaza kwanini hangeshauri wakaondoka naye, lakini akijipa moyo kiume…akamtizama Maua wakati keshaingia kwenye gari na kumuona akiwa kashika shavu huku machozi yakimtoka…na kumbe ndiyo ilikuwa safari ya kwaheri ya kuonana…buriani


Ni mimi: emu-three
Enhanced by Zemanta

2 comments :

samira said...

m3 inasikitisha kweli huyu dada yamemkuta na inaonekana inavutia kweli
mimi sichezi mbali

Pam said...

pole Maua mwezi mzima ni mwingi kwa wapendanao kuwa mbali mbali huona kama mwaka!!