Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, July 18, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-1



 ‘Nilikuwa kwenye chumba nikiwa navaa gauni la harusi, gauni mbalo thamani yake siwezi kuielezea, sio thamani ya kipesa, bali thamani ambayo haielezeki kwa maneno’ alianza kunisimulia kisa chake huku machozi yakimlengalenga.

Alisema kuwa aliliinua lile gauni na kuliangalia tena, …na kukumbuka siku ile alipoletewa, sio kwamba, hakulipenda, sio kwamba ilikuwa mara ya kwanza kuliona, ila alishangaa, siku ya leo imekuwaje…siku ile lilipopendekezwa kuwa ndilo linamfaa, alitaka kulikataa,…lakini alikosa hoja ya msingi, kwani ndilo lililokuwa linampendeza, na kufanana na sura yake, na kila mmoja aliona hivyo…

 Lakini yeye aliona zaidi ya wanavyoona wao…hakutaka ubishi, hakuwa anataka kukosana na watu tena, alishachoka, alishaona hakuna jinsi, bora tu akubali, yaishe….akajiuliza akilini  kwanini ikatokea, kila kitu siku hiyo kinafanana na ile siku, hata gauni la harusi lipo sawa sawa na lile gauni la harusi yake ya kwanza, utafikiri waliamua kufanya hivyo, lakini alipodadisi aligundua kuwa imetokea tu hivyo…akaliangalia kwa moyo wa hamasa sana, huku akili ikiwa bado haiamini kuwa kweli siku kama hiyo imefika tena…na cha ajabu, ni siku kama ile, hata masaa yanaendana…akaguna…hata tarehe, haiwezekani…! Ndoa ya pili…inafanana na ndoa ya kwanza karibu kwa kil kitu,…

 Akaliinua lile gauni juu, na kabla halijajitandaza kitandani, taswira ya ndoa yake ya kwanza ikamjia kichwani, na kuanza kusikia vigelele na shangwe nje…ilikuwa siku ambayo hataweza kuisahau maishani, kwani akiwa katika hali ile ile nayoiona leo, mlango uligongwa na aliyekuwa ameingia siku ile alikuwa shangazi yake, huyu ndiye aliyemlea, na alimuona sawa na mama yake…alichukuliwa akiwa mdogo na shangazi huyu, akalelewa kiukwelikweli na kumsomeshwa kadri ya hali yao…na wanasema alijengwa kitabia ambayo shangazi huyu aliitaka…

‘Wewe hebu vaa hilo gauni, usinitie aiabu, muda ni kitu muhimu sana…’ akasema shangazi yake akiwa na mpambe wake pembeni, alianza kulivaa lile gauni kwa aibu, hakupenda kuvaa nguo akiwa anangaliwa na watu,lakini kwa ile aibu ya siku ile, na fikira za siku ile akiwaza kuwa ndio siku imefika anaondoka kwenda kwa mume, hatamuona tena mama yake  kwa karibu, hatamuona shangazi  yake kwa karibu, hatawaona ndugu zake kwa karibu…akawa anataka kama kukataa, lakini moyoni  mmmh!

‘Jamani kwani lazima nivae mkiwa humu ndani…tokeni kidogo nikivaa mtakuja….’ Akasema Maua

‘Wewe Maua, hivi unatufanya sisi watoto kama  wewe, ina maana ukiolewa utakuwa unamwambia mume wako atoke nje uvae kwanza, hapa tunataka kuanza kukuonyesha kuwa , mwili wako kwa mume wako utakuwa wake….kumbuka nilivyokuwa nikikufunda, aibu kwa mume wako hapa ndio mwisho wake…usiende kuniletea aibu huko…’ akasema shangazi yake. Akasema kiakili lakini huyo si mumee…hata hivyo sitakubali kufanya kuvaa nguo au kuvua mbele yake….

‘Ilikuwa sababu ya utoto au sijui vipi…’, akasema Maua kwani kwa kisirani alilivua lile gauni na kulibwaga chini na kusema kama ni hivyo hataki kuolewa tena, ina maana anakwenda kuishi na mtu ambaye atakuwa anamchungulia hata akioga, hata akivaa…hapana, …kumbe ndoa ndivyo ilivyo hapana, ….anasema alitaka kutoka nje huku akisema kwa sauti `kama ni hivyo sitaki kuolewa tena …’

Alishitukia kibao cha nguvu kikitanda usoni, hajakaa sawa kibao kingine kikatupwa, na kabla hakijatua usoni mpambe akakizuia kwa mkono wake, na isingekuwa huyo mpambe  kuwa karibu yake  siku hiyo uso ungelivimba kwa vibao..woga ukamshika na harakaharaka akaanza kutetemeka na kwa aibu akalivaa lile gauni…alimjua shangazi yake kuwa hana mchezo pale panapohitajika kuwajibika, ….

 Tukio hilo lilitokea siku kama ya leo miaka miwili iliyopita, na leo tukio hilo linatokea tena na mambo yake yanafanana  sawa sawa…alipofika hapo akaguna akasema ‘haiwezekani  nipigwe vibao kama siku ile…leo najua nini ninachokifanya, ila….’ aliwaza kwa makini, kwanini itokee hivyo hivyo, kwanini kila kitu kiwe sawa sawa na siku ile,…hapo machozi yakaanza kumtoka…hasa ilipomjia ile taswira…  baada ya kufunga ndoa na bila kujijua uso ukatandwa na tukio la siku ile,…

 Mara kwa mbele ya lile gauni ilitanda sura ya yule aliyemkosesha raha….akamuona akiliondoa lile gauni mbele yake na akatoa lile tabasamu….mmmh, lile tabasamu, ambalo hataweza kuliona tena… , na hapo akawa anasubiri kusikia ile kauli ya kipenda roho chake…kauli aliyoitoa siku ile…lakini hakuisikia, akawa kama anafumba macho huku akiisubiri, na kumuomba mungu aisikie tena ile kauli… lakini haikutokea,…na mara akasikia vigelelgele vilitanda hewani kwa nje…kama siku ile , lakini ile kauli aliyoisubiri kwa hamu haikutokea …haikutokea, akafumbua macho yake, na kujikuta akilitizama lile gauni la harusi!

 Mara akasikia nje vigelele nje..tena na tena, na hapo akazindukana rasmi na kujikuta yupo kwenye siku nyingine, sio siku ile tena, ingawaje ki tarehe , saa na mwezi zinafanana…, akalibwaga lile gauni kitandani kwani hakuamini kabisa ingelikuja ndoa nyingine,…hakuamini kabisa baada ya tukio lile angelidiriki kukubali kuolewa na mtu mwingine…alishaapa kamwe hataolewa tena maishani mwake, hakutamani kabisa kuolewa tena, hakumtamani tena mwanaume yoyote hapa duniani, lakini mungu ana mitihani yake, leo hii yupo, kama siku ile ile, tarehe na masaa…anasubiri kama siku ile, baada ya ndoa mume ataingia na kumchukua waondoke pamoja …alipowaza hili akajikuta machozi yakimtoka, …ina maana kweli nimeamua kuihini ahadi yangu, kuwa sitaolewa tena na mwanaume mwingine, ….kuwa sitapenda mwanaume mwingine, ….kweli ni mimi naivunja ile ahadi, hapana siamini hilo…akajikuta machozi yakimtoka kama mvua, na badala ya kulivaa lile gauni, akawa analia hadi kichwa kikaanza kumuuma..

 Baada ya kulia sana ikafika mahala akaanza kujilaumu, kwanini alichukua uamuzi huo, kwanini alilangaiwa mpaka ….akainama na kuliangalia tumbo lake…mpaka…oh, kama kweli nilidiriki kukubali siku ile tendo likafanyika…iweje leo akatae….akabetua mdomo na akaona akubali matokeo na kuwaza kwa kusema  `hivi leo ni siku ya kulia tena au ni siku ya kufurahi, kama nikulia nilishalia sana, hadi kutaka kujiua, na ikafika mahala ndugu jamaa wakamuona kama mwehu, kama punguani kama mtu asiye na imani na mungu…

Haya metokea na yeye asingeliweza kuyapinga..akasema basi,…haya ni mapenzi ya mungu, tuyakubali, huwezi jua, …kwani hujafa hujaumibika, kwani ilishaandikwa iwe hivyo, …na hata kama angelilia hata kama angelijiua hata kama….isingebadili kitu..yote ni mapenzi ya mola, ….akachukua leso na kujifuta machozi.

‘Wewe Maua umeshamaliza kuvaa, twataka kuja kukukagua, kwasababu na wewe hukui tu, usinifanye nifanye yale nisiyoyataka hebu fungua mlango nataka kukaangalia jinsi ulivyovaa, usije ukatutia aibu, tangu uingie humo, subirisubiri …muda unakwenda utafikiri ni mara yako ya kwanza…’ alisikia sauti ya shangazi yake  ikiita na kumfanya azindukane kwenye mawaza mazito, na haraka akalichukua lile gauni lake la harusi na kuanza kulivaa kwa haraka,…

 Mara akatulia na kuwaza kwanini huyo aliyemwambia avae haraka, ambaye ni shangazi yake, alikatiza maneno kama vile kanyamazishwa na mtu…akatega masikio na kwa mbali alisikia kama anaongea na sauti kama ya mwanaume, ina maana bwana harusi kaona wanachelewa kaamua kuja hapo au katuma mtu, kwani watu wao walikuwa wapo upande wa pili wa nyumba, na hadhani wangelikuja kuingilia mambo yao ambayo hayawahusu…sasa ni nani huyo!

Sasa ni nani huyo…akavaa lile gauni haraka na kuinuka kuelekea pale mlangoni, ili kufungua ule mlango,kwa kukilegeza kibano cha ndani , ili shangazi akifungua mlango uweze kufunguka kirahisi na akarudi pale kitandani, akiwaza afanyaje sasa asimame atulie amsubiri shangazi yake na mpambe wake waingie, au akae kitandani, lakini aliogopa  kuwa akikaa kitandani anaweza kulifanya lile gauni lijikunje kunje, …akatamani aendelee kusimama hivyo, hivyo mpaka waingie, na wakati anawaza hivyo, akahisi mlango umeshafungulia na mtu, na alihisi kuwa aliyeingia ni shangazi yake, akasubiri asikie kauli yake ambayo haishi kutoa kasoro…lakini alihisi dalili nyingine isiyo ya kawaida, …..au ni kule kumuogopa sana shangazi yake ndio maana mwili unasisimuka kwa woga..kwani ingawaje anampenda shangazi yake, lakini inapofika mahala pa kuogopa kufanya uzembe, mwili humcheza kwa woga…anamjua vyema shangazi yake,…hataki makosa, na yupo tayari hata kukuzaba kibao mbele za watu…

 Mwili ulianza kumsisimuka, nywele zikawa zinasimama na mapigo ya moyo yakaongezeka, akajikuta akiogopa, akajikuta akipatwa na msisimuko usio na wakawaida, msisimuko ambao hakuweza kuuelezea, ni kama chumba kilikuwa na ubaridi na mara joto la ghafla likaingia…au kulikuwa na joto kali na mara ubaridi wa ghafla ukaingia…na kuleta uwoga mioyoni mwa watu…kwanini iwe hivyo, ina maana leo anamuogopa shangazi yake kama kuogopa shetani au jinni au kiti cha kutisha, hapana,….na kwanini shsngazi yake aingie na kukaa kimiya, haiwezekani sio kawaida yake akaona ageuze uso amwangalie, lakini akajiona mzito, akaogopa kabisa kugeuka, ….kwanini aogope…

Akahesabu moja mbili tatu,…ili ageuke na kumuonyesha shangazi yake kuwa yeye sio mwoga kiasi hicho, sasa kakua yupo tayari kwenda …yupo tayari kuolewa na mwanaume wa pili…yupo tayari kuyasahau machungu yaliyopita, na shingo ikawa inageuka taratibu, na uso ukaelekea mlangoni, na…macho yalipotua kwa huyo aliyeingia, akajikuta akifungua mdomo kutaka kupiga yowe…na macho yakamtoka pima kwa woga, ……

Je nini kilitokea, …jamani hii ni onjesha onjesha tu ya kisa hiki, sijui kitakuwa na urefu gani,… hiki ni kisa ambacho ni maalumu kwa kumbukumbu za lile tukio la kuzama kwa MV Bukoba, ni kisa cha ukweli kilichotokea.... ni siku nyingi na huenda wengi wamelisahau hilo tukio au wanalisikia tu, lakini maandishi hayasahauliki…nilikiandika hiki kisa na tukio hilo kwa lugha ya kigeni katika diary yangu ya mkononi, na nimeona leo niliweke hewani kwa lugha yetu… kwanza kwa kukitukuza Kiswahili, pili kwa kulikumbuka lile tukio na kuwapa pole wale waliopoteza ndugu zao na tatu kama zawadi kwa wapendanao ….Naomba tuwemo pamoja!



Ni mimi: emu-three

6 comments :

Fadhy Mtanga said...

....sikudhubutu kukinyanyua kikombe changu cha chai hadi nilipomaliza kuisoma simulizi hii....ahsante sana kwa simulizi tamu asubuhi hii...nasubiria sehemu ya pili hadi ya mwisho.i nilipomaliza kuisoma simulizi hii....ahsante sana kwa simulizi tamu asubuhi hii...nasubiria sehemu ya pili hadi ya mwisho.

emu-three said...

Mkuu Mtanga, hapo nimedonoa kidogo tu, kama kianzio, maana katika utunzi kazi ni jinsi gani ya kuanza,na jinsi gani ya kumalizia...kwangu mimi lakini...TUPO PAMOJA KARIBU SANA

samira said...

m3 shukrani kwa simulizi mpya ambayo inaonmyesha ni nzuri
tupo pamoja

malkiory matiya said...

Mkuu m3 kisa hiki kinasisimua.

Anonymous said...

ni kisa kizuri ila kwa ushauri tu ili kuleta uhondo punguza maneno mengi (too much detailed hadi inapoteza ladha) kwa roho safi ni ushauri tu.

emuthree said...

Nawashukuruni sana, kwa ushauri na kuwa pamoja nami, na mshauri wa 10.30 am, nakushuru kwa ushauri wako, nitaufanyia kazi Insha-Allah