Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, June 7, 2011

Dawa ya moto ni moto-19Hebu turudi kwa Maneno, unakumbuka tulipoishia sehmu iliyopita?...nakumbuka ilikuwa Maneno kamfuatilia yule docta wa viatu vyekundu, akafika kwenye kile chumba, halafu….akawa anamwangalia docta akitoa sindano akiwa na nia ya kumchoma yule mgonjwa aliyelala kitandani, ukumbuke kuwa Maneno  hadi muda ule alikuwa hajui ni nani aliyelala kitandani, ukumbuke kuwa Maneno aliitwa kuwa kuna mgonjwa anamuhitaji hakuwa na uhakika kuwa aliyemuta ni mkewe au ni nani, …akaingia kwenye udadisi, sijui unamhusu au vipi, sasa endelea,
 Maneno akiwa kaduwaa hajui afanye nini kuhusu yule docta wa viatu vyekundu baada ya kusikia sauti ya mtu akija nyuma yake, aliogopa kuyaondoa macho yake kule ndani ya chumba, na pia aliogopa kugeuka na kuonana na huyo anayekuja nyuma yake, kwani hapo mlangoni kuliandikwa onyo kuwa `hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia hapo, ni dakitari tu….’ Sasa yeye kakiuka sheria , lakini kagundua mengine, ambayo yalidhihi kuwa docta aliyemuona ana nia mbaya na yule mgonjwa, sasa atamwmbiaje huyu anayekuja nyuma yake, na je ni nani, asije akawa mshirika mwenza wa huyo aliyepo ndani.
Hebu tuwepo kwenye muendelezo wa kisa hiki, `dawa ya moto ni moto, sehemu ya 19.
                          *********
 Maneno akiwa anaangalia kwa jicho moja kule ndani ya chumba huku jicho jingine likijaribu kumwangalia nani yupo nyuma yake, akiwa na wasiwasi, akasema, kwa kunong’ona, `Jamaa anajifanya docta ili amuue mgonjwa kwa sindano ya sumu, nimemsikia kwa masikio yangu mwenyewe akimtishia mgonjwa kuwa atamuua kwa sindano ya sumu kama hatatimiza matakwa yake,fanya haraka umukoe…’
‘Unasema nini wewe, nani kasema mgonjwa wangu anahitaji sindano…; sauti  ya ukali ikatoka nyuma yake, na mara huyo mtu akampita akiwa na vazi jeupe la kidakitari kama yule aliyeingia ndani, na akasukumwa pembeni na huyo aliyekuwa nyuma yake ilia pate nafasi ya kuingia ndani, kumbe ndiye docta maalumu kwa huyo mgonjwa, haraka akaingia kule ndani, na Maneno naye akapata mwanya  wa kusogea na kusimama katikati ya mlango.
Yule Docta alipoingia ndani akamvaa yule docta mwingine kwa maneno akimuuliza kulikoni, kwanini anaamua kumpiga huyo mgonjwa sindano bila idhini yake, na kwanini ampige sindano. Yule docta wa viatu vyekundu, alikuwa kashaificha ile sindano, akabaki kaduwa kidogo, lakini mara akajifanya anamkagua yule mgonjwa kitandani na kusema, yeye alipata taarifa kuwa huyo mgonjwa analeta usumbufu, kwahiyo akaja haraka kuangalia…na kama anaumbua basi ampige sindano ya kumpa usingizi
‘Mimi ni wanafunzi tunaochukua mazoezi ya vitendo niliambiwa nifike hapa kumwangalia huyu mgonjwa kwani alionekana kuwa anasumbua…samahani sikuweza kukufikia kwanza, niliona ni bora nije nione hali yake kwanza …’ akasema yule docta wa viatu vyekundu.
‘Wanafunzi wa vitendo mbona wameshamaliza elimu yao kwa vitendo, wewe ulibakia kufanya nini, kwanza hebu naomba kitambulisho chako, kwani umeshanitia wasiwasi…, leo sio siku ya wanafunzi kupita huku wodini…’ akasema docta kwa sauti ya kiaskari.
‘Basi aliyekosea ni huyo aliyeniagiza,…sijachukua kitambulisho change,  ngoja tukamuulizie vyema huyo aliyeniagiza…’ akasema yule docta wa viatu vyekundu, akitaka kuondoka
‘Hiyo sindano yenyewe iko wapi, uliyotaka kumchoma mgonjwa…’ akauliza docta
‘Sindano, sindano gani…..oh, unajua nilikuwa nimesahau, nimeiweka?’ akasema yule Docta wa viatu vyekundu akiwa anajibaragua ili apapate mwanya wa kutoka, lakini dota yule mwingine alikuwa kamkinga, …huku kashika kiunoni.
  Maneno alinogewa na kile kinachoendela mle ndani akajisahau kabisa, lakini ghafla,  kwa haraka ya ajabu, Maneno alishikwa na mshangao, kwani hakuona jinsi gani mguu ulivyoinuliwa na jinsi gani ilivyotokea, yeye alishangaa kumuona docta wa yule mgonjwa akpepesuka na kabla hajajitetea vyema, teke na ngumi vikamsindikiza kwenda sakafuni. Ilivyoonekana ni kuwa yule docta alitaka kumkagua docta mwenzake mfukoni, akijua kuwa kaficha ile sindano mfukoni, …akiwa na nia hiyo, alikuwa kama anainama hivi ili aufikie mfuko wa koti wa yule docta mwenzake, na hapo akashitukia teke la haraka lilitupwa na kumpata usoni mwake, na hiyo hali ilimtia mshangao, …alipoinua uso uliojaa maumivu akajikuta anakutana na ngumi, moja usoni na nyingine eneo la shingoni…mapigo yale ya haraka yakamtupa yule docta chini kama mzigo, na kwa haraka yule jamaa akamsogela pale chini kutaka kumumalizia kabisa.
Maneno akaona hapo anahitajika kutoa msaada wa haraka, akasukuma ule mlango ili aingie ndani, kabla hajaweza kuingia ndani akashikwa na mshangao mwingine, kwani,yule mgonjwa aliyekuwa kalala kitandani aliinuka na kuokota chupa ya soda iliyokuwa mezani, ilikuwa haijafunguliwa, na  kwa haraka akambamiza yule docta wa viatu vyekundu kichwani, na kile kipigo kilikuwa kikali kikamshitua docta wa viatu vyekundu na kutoa mguno wa maumivu, aligeuka kutaka kujiokoa lakini akakutana tena na kipigo kingine cha ile chupa, na sasa kikampata sawasawa na kumfanya alale, kumlalia yule docta mwingine, nafikiri alishapoteza fahamu.….
‘Piga kwa nguvu, watu hawa wanavichwa vigumu, ukimuonea huruma atakugeukia tena..’ akasema Maneno kwa munkari kama vile anashabikia yale mapigano. Aalisema huku anamwangalia yule docta wa viatu vyekundu kuwa hawezi kuinuaka tena, akamsukuma kwa mguu wake, ili aondoke juu ya docta mwingine. Akamwangalia yule docta mwingine akamkuta naye kazimia.
‘Madocta wote wamezimia, sijui nani wa kumtibu mwenzake, ilikuwa zinga la shoo…ooh, mgonjwa nashauri utoke humu, maana jamaa huyu akiinuka kutakuwa hakukaliki, hapa dawa ni kuwaita walinzi tu…au unasemaje mgonjwa..’ akasema na kumgeuka mgonjwa, alipomuona akabakia mdomo wazi ….
‘Oooh, Maua ndio wewe….’ Akasema Maneno na kumsogelea Maua ambaye alikuwa kashika mdomo, akiogopa tendo alilolifanya, akilini akijua kaaua.
‘Oooh,…sijui nimefanya nini…Maua ndio nani…ooh, wewe… mfunge kamba huyo jamaa hakikisha unamfunga kiukwelikweli ….oooh, kichwa changu oooh, jamani kichwa changu…’ mara Maua akapepeseuka na kudondoka chini, na hapo Maneno akawa anahaha kumwangalia mke wake kuna nini kichwani, akakumbuka yale maumivu ya kichwa ya siku ile, ina maana bado yapo. Akamsogelea haraka mke wake  kumuwahi asidondoke sakafuni, akamdaka kabla hajafika chini na  wote wakadondoka chini, lakini alijitahidi mkewe asijigonge sakafuni,…!
‘Oooh, mke wangu una nini, ni kile kichwa, tulia hapa ni kamuite docta, lakini..ngoja kwanza akajitahidi kumzuia vyema mkewe pale chini na hatimaye akamwinua na kumweka kitandani harakaharaka…akageuka kutafuta kitu cha kumfunga yule docta kama alivyoshauriwa na Maua, na wakati huo kumbe huyo docta wa viatu vyekundu alishaanza kuinuka,…
‘oooh, shiti, …kichwa kinauma, oooh, wewe …utanitambua….’ Akasikia sauti ya huyo jamaa, huku anajitahidi kuinuka na huku akashikwa kichwa, na alipoona damu ndio akasema `utanitambua..’
 Na wakati huo sauti za watu zilisikia nje wakija kwenye hicho chuma, na huenda ni walinzi …yule docta wa viatu vyekundu akainuka na kuanza mapambano, alikuwa mwepesi wa ajabu, kwani Maneno hakutegemea hilo, alijikuta akipata mateke mawili ya haraka, na ngumi nzito usoni,alianza kupepesuka huku anaona vinyota usoni…lakini akajikaza na kuudaka mguu wa yule docta wakati anarusha teke jingine …na hapa akamuwezea,kwani yule docta alikosa uimara akaanza kupepesuka akitaka kudondoka, chini, na  ile sindani aliyokuwa nayo mfukoni ikamtoka na kuzama chini ya kitanda bila ya yeye kujua, kwani alikuwa akijitahiidi kushika ukuta asidondoke chini… na wakati huo walinzi wakaingia…
‘Kumetokkea nini huku ndanii docta, mbona makelele na vitu vinasikika vikidondoka,….,?’ akauliza mlinzi mmojawapo.
‘Nyie askari mpelekeni huyo wodi ya vichaa, mbona mumemuachia huyu kichaa kuja huku, hamuoni kachanganyikiwa analeta fujo huku wodini…na huyo binti anatakiwa kupigwa sindano ya usingizi haraka, kwani wote wamechanganyikiwa wanaweza kuleta matatizo…’ akasema yule docta wa viatu vyekundu huku akitafuta ile sindano yake mfukoni, na alipoona haioni akasema `nesi yupo wapi, ngoja nikachukue sindani haraka maana hawa watu ni hatari, wamemuumiza docta mwenzangu na sasa wamenigeukia mimi…ooh’ washikeni nakuja…!’ Akasema huku anatoka mlangoni
‘Sio kichaa mimi , mkamateni huyu ni docta wa uongo amempiga docta mwenzake karibu amuue, alikuwa akitaka kumuua mgonjwa hapo kitandani…mshikeni huyo anaondoka…’ akasem Maneno, lakini wale walinzi hawakumsikiliza wakawa wanamshika yeye huku akipata virungu vya kwenye magoti vilivyomfanya achuchumae na kunyosha mikono juu, akisema kwa uchungu…`jamani mnafanya makosa mnamuachia mhalifu, anaondoka…ooh, mnaniumiza..basi basi……

                                                         *************
Tuwepo kwenye muendelezo, sio kusudio kuleta kipande hiki kikiwa kifupi hivyo, ndio kama nilivyowaelezea.  Mambo baaado yanatokota, nini, na kwanini inatokea hivyo?

Ni mimi: emu-three

13 comments :

Swahili na Waswahili said...

Kaka kazi nzuri nakuaminia mtu wangu!Pamoja kaka.

Anonymous said...

Tunazidi kuwemo humu pamoja sana m3

Yasinta Ngonyani said...

Asemacho Rachel ni kweli kwamba m3 kwa kwali ni kazi nzuri sana na tupo bega kwa bega. Swali:- Rachel Umejuaje kama m3 ni MKAKA?

Goodman Manyanya Phiri said...

Ndiyo, katika mapigano au mzozo wa wawili, yule wa kwanza kulalamika kwa wakubwa ndie anaaminika kuliko wa pili.

Lake Maneno halipo tena kwa walinzi, aiseee!

Candy1 said...

Hata ingekuwa sentensi moja bado story inaendelea au sio? Haya tuone Maneno kajiingiza kwenye kasheshe gani tena...mi nipo

Anonymous said...

Swali limeulizwa na dada Yasinta, M3, ni mdada au ni mkaka? Mimi naamini kama alivyosema yeye mwenyewe awali, ki-uandishi, kama mwandishi anasimama popote,...mdada, mkaka, m-vyovyote, ila hali halisia inabaki pale pale, au sio, sasa M3 ni mkaka au ni mdada, nyinyi mnaomuita hivyo mumegundua wapi, hebu tumchimbe kidogo?

Anonymous said...

Huyu M3 ni mdada kwasababu ya visa vyake vingi vinawatetea wanawake, pili ana aibu, kwanini haweki angalau picha yake, au jina lake kamili...ni maoni yangu tu, kama sio asinielewe vibaya~eti nyie mwamuonaje huyu mdada?

Anonymous said...

M3, KISA HIKI KIPO JUU SANA. TUPO PAMOJA MKUU. WE NI MKALI DAIMA MI NAPENDA SANA STORY ZAKO.

WADAU WEZANGU, MIMI NGOJA NISEME, M3 NI ........AAAH!! HAPANA. BASI NAONA SITOMTENDEA HAKI NIKISEMA, NITAKUWA NA KIMBELEMBELE. KWANI MWENYEWE KAWEKA FUMBO. SIJUI ANA MAANA GANI? LABDA KUTOKANA NA HADITHI ZAKE AU KWA SABABU ZAKE MWENYEWE. LABDA PIA KWENYE KUNONGESHA STORY ZAKE TUSIELEWE JINSIA YAKE, KAMA HAPO JUU WADAU WASEMAVYO, MDADA AU MKAKA?

KWA KWELI M3 WEWE NI KIBOKO, UPO JUU. BIG UP MY BOSS. NAKUAMINIA.

BN

Anonymous said...

Mimi namfahamu kabisa,tulisoma naye ni mdada,ila anapenda sana kujifamnanisha na wanaume, anacheza fotbal...jina lake ni miriam, ndio kafupisha ili lionekane kiume

samira said...

mambo yamenoga sana maneno nae heshi umbeya halafu mwisho matatizo
wadau mimi na nahisi ni mdada ila kwa vile mwenyewe hatuweki wazi basi tuendelee kusoma mikasa yetu
tuwachane na haya
just maoni tu msinielewe vibaya

Swahili na Waswahili said...

hhahaaha dada Yasintaaaa!!!!Mimi nahisi tuu hata sina uhakika, Nikisomasoma maoni yake pale kwangu na kwawengine naona kama mkaka kaka hivi!!!
Pia ukiingia pale SwahilinaWaswahii,Kwenye jikoni leo kwa mama Kamala umo ndani alichangia nami nikamswalika swali, Akanijibu na kunifundisha kupika Chakula cha kwao kinaitwa [KISHUMBA] sasa unaweza kuchungulia alivyokuwa ananifundisha na maelezo aliyotumia.kama wewe utawazaje?.

Anonymous said...

Wengi wanahisi ni mdada,yeye mwenyewe anasemaje kwani kama ni dume uitwe mdada inahitaji subira.Tupe uhondo hizi ni changamsha kijiwe.Mimi nafurahi ukiwa hivohivo mafichoni!

emu-three said...

Yeye mwenyewe anasemaje?
Emu-three ndio jina langu au kama wasemavyo wengi AKA, yangu na kama nilivyoelezea awali kwenye blog,hapo pembeni ni ufupisho wa herufi za majina yangu matatu.
Nia na mdhumuni yangu, sio mimi kama,kujulikana, sio mimi mnijue kuwa ni jinsia gani, kama wengi wanavyotaka. Nia yangu ni kutoa kile nilichokuwa nacho kichwani kwa siku nyingi, kuwa nataka niwe mtunzi wa vitabu,...mnijue kwa maandishi, kwa visa, kwa hadithi kwa diary hii... lakini kila nilipojaribu kuandika viatabu nilikutana na vikwazo vingi.
Basii nilipogundua kuwa kuna kitu kinaitwa BLOG, na unaweza ukaandika watu wakasoma ...nikashukuru mungu sana, na hapo nikaanza kuandika kidogokidogo...mwanzoni hakuna aliyekuwa akinijua, nikawa naaadnika tu kujifurahisha, na baadaye watu mmoja mmoja wakaanza kuijua blog hii...sio haba nashukuru mungu na nawashukuru wale walionisaidia kuirekebisha hii blog nakuwa kama mnavyoiona.
Kama mnavyoona, blog hii iliwekwa hewani tangu 14-7-1999, lakini ilikuwepo toka awali, nilikuwa nashindwa jinsi gani ya kuiweka ionekanae hewani. Nawashukuru wengi waliobahatika kunisaidia kwa hili. Hapo sio mahala pa kuwataja hawo walionisaidia ipo siku nitafanya hivyo kwa wakati muafaka, mungu atawalipa kwa wema wao huo.
Je mimi ni nani na jinsia yangu ni ipi, na huenda nitaulizwa zaidi na sura yangu ikoje. ...Mmmh, hebu kwanza nikaendeeleze kisa chetu cha `dawa ya moto ni moto' halafu nitawaelezea...au vipi kila kitu kwa mahala pake, ....!
TUWE PAMOJA KWENYE SEHEMU YA 20, YA `DAWA YA MOTO NI MOTO'