Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, May 31, 2011

Hujafa hujaumbika



 Leo wakati nakuja kazini nilikuwa nikiwaza mengi kuhusiana na maisha, nikawa nasikitika moyoni kuwa nateseka na usafiri, maisha magumu nakadhalika,. Pembeni ya kilti nilichokaa kwenye daladala ambalo huwa tunajazana kama magunia, …alikuwepo dada mmoja, alikuwa katulia na uso ulionyesha dhahiri kuwa alikuwa na machungu fulani.  Nilitamani nimsemeshe lakini nikachelea, maana hujui mtu kaamukaje, hujui nini kilichomsibu unaweza wewe ndio ukatolewa uvivu na hasira zote zikaishia kwako.
 Ilipofika kituo cha mbele yule dada akashuka, alikuwa akitembea kwa shida, lakini ilikuwa haionyeshi kuwa ana matatizo gani, alipofika mlangoni akalipa nauli yake akaishia, na mara watu wawili wakagombea kukaa sehemu ile aliyotoka yule dada na akabahatisha kukaa mwanamama mmoja. Alipokaa tu akaanza kuongea, na kusema,;
‘Jamani dunia hii kuna mambo,…wanasemaje vile, hujafa hujaumbika, su sio… huyu dada aliyekuwa amekaa hapa, sikuzania kuwa angeliweza kuja kupanda daladala. Masikini wa mungu, mume wake kafariki miaka mitatu au miinne iliyopita. Katika maisha yao waliishi kifahari, unajua kuishi kifahari, nyumba nzuri, na wala sio moja, magari ya kubadili kama nguo!...siunajua maisha ya namna hiyo?’ akawa kama ananiuliza nami nikamwangalia tu.
‘Basi walikuwa na gari mbili ya mume na mke, mke na biashara zake mume kazini, watoto wanasoma shule ya kimataifa. Walikuwa wakitupita kama radi mabarabarani, maana wanapenda kuendesha magari yao utafikiri wapo mashindanoni., hawatoi `lifti’ hata siku moja, mtachafua magari yao, mtawatia kinyaa na mijashojasho yenu…jamani huwezi amini. Hata nyumbani kwako ukifika, ukisalimia wanakuitikia kwa shida, nasikia eti ukiingia ndani kwako, ukitoka wanapuliza `pafume’ umaharibu hali ya hewa!..’
Nakumbuka watoto wangu waliwazoea sana watoto wao, wakawa wanafika nyumbani kwao kuangalia runinga, haikupita muda wakapigwa marufku kiaina, basi mimi nikalijua hilo na kwa vile najua tabia yao, nikawapiga marufuku watoto wangu kwenda kwao, lakini watoto ni watoto, wakawa wanajiiba wanafika huko, hasa kuangalia picha, kwani wao wana `ungo’ dunia yote wanaiona!. Siku moa nikakutana na huyo mama akanipasha kuwa nijaribu kuwachunga watoto wangu kwani wanakwenda mara kwa mara kwake , na kusababaisha watoto wake wasiende kwa ratiba waliyopangiwa… wao wanaishi kwa ratiba, kizungu-kizungu, siunajua kuishi kizungu-kizungu?’akawa kama ananiuliza, lakini mimi nikawa kimya, namsikiliza tu!
‘Unajua watoto usiwaachie hivi hivi, wachunge, wapangie ratiba, ..lalalal…maneno mengi, akaendeela kusema hivi, sasa wanakuja kwangu, makocho furufuru..kelele mtindo mmoja, sio vyema, nakushauri tu, ili tusionane wabaya…’ akasema wee, na mimi kimya,  wala sikumjibu kitu’.
‘Basi ajali ikatokea, ajali mbaya kweli maana siku hiyo walitoka harusini,wakati wanarudi , walikuwa ngari moja tu familia nzima ilikuwa humo ndani, ilikuwa ajali mbaya kwelii, baba akapoteza maisha hapohapo, mama nyang’anyang’a  kaishia Muhimbili, bahati nzuri watoto hawakuumia sana
 Mama alikaa sana Muhimbili sijui mwaka, au mwaka na nusu, maana alivunjika sehemu nyingi, mbavu, miguu…yaani kaponea kudura ya mungu, alipotoka kutibiwa, na mgongo, na kigari cha kusukuma, biasahara ikawa imekata, na kwa vile alikuwa hayupo siku nyingi, watu wakawa wamemuibia, na alijikuta kama anaanza upya maisha. Wanandugui wakiume wakagawan kile walichokiona bila kujali kuwa jasho jingine ni la mke. Angefanyaje naye yupo ICU. Waliokuwa wakimuhangaikia ni rafiki zake aliokuwa akifahamiana nao, matawi ya juu,kwani hata ndugu zake wakuzaliwa tumbo moja, alikuwa hapatani nao, …wanamtilia kiwingu!
‘Basi akaishi kwa shida, hata marafiki zake wakaanza kumkimbia, kwani hana pesa tena, hana mbele wala nyuma, watoto wakafukuzwa shule ile ya kimataifa ikabidi wakasome shule za kawaida..inasikitisha, kwani watoto walikuwa mara kwa mara wakilia na kulalamika, kuwa kama baba yao angelikuwepo wasingepata taabu, lakini hayupo, na baba wadogo wamekomba kila kitu…hawana habari nao tena, dunia hii kuna dhambi jamani…’ akasema yule mama huku anainua mikono juu
‘Sasa ndio huyo mama unamuona hapo anakwenda kusikiliza moja ya kesi zake za madai kwa ndugu wakiume ambao walichukua nyumba na shamba wakidai ni mali yao. Kesi imechukua muda kweli, naona hata mama mwenyewe alishakata tama, lakini kuna mama mmoja wa ustawi wa jamii ndio anamsaidia vinginevyo asingeweza…’
‘Lakini mbona anatembea vizuri kidogo, siulisema alikuwa anatembelea magongo..?’ nikamuuliza
‘Anajikongoja tu, kuna  siku hawezi hata kutoka nje…’ akasema yule mama.
‘Kweli hujafa hujaumbika, hata mimi namfahamu yule mama..’ akasema jamaa mwingine
 Mwisho wa safari ukafika, kila mmoja akaelekea njia yake, je wewe wasemaje kuhusiana na kisa hiki?

Ni mimi: emu-three

8 comments :

Anonymous said...

Ujumbe murua kweli, mimi napenda kukuuliza, mbona kwenye blog yako huweki matangazo, hili lingekusaidia kuondokana na matatizo ya kutegemea ofisini kwako, ni wazo tu. ILA KWA KWELI UNAFANYA VITU VYENEYE HEKIMA SANA

Simon Kitururu said...

Ama kweli kabla hujafa hujaumbika!:-(

Yasinta Ngonyani said...

Mimi nasema ya kwamba hata kama ukiwa tajiri au maskini binadamu wote katika dunia hii wana UMUHIMU sawa kabisa. Ukiwa na mali usijione wewe ni mtu zaidi kuliko wengine ishi kama wewe na shirikiana na wengine kama kawaida...

emu-three said...

Hiyo ni kweli ndugu zangu ,liotoa maoni hapo juu, mkuu S.Kitururu, Yasinta na asiye na jina!
Huwa mtu unapokuwa katika njema, unajisahau kuwa sote ni mavumbi tu uchafu ndio jadi yetu, kwahiyo tuthaminiane, na kuvumiliana.
Kuna jamaa mmoja anatoa harufu ya mwili wanaita kikwapa, yeye kila akienda mahali hata kama hajafika, hata kama kwa muda huo ile harufu haijaanza kutoka, wanaziba pua!
Well ni sawa, hiyo harufu inakera, lakini thamini ubinadamu wake, sidhani kama kaiomba hiyo!
Maisha ni kupanda na kushuka, leo unacho kesho huna, kwahiyo tujiandae kwa vyovyote vile, kwa kuwakubali wanajamii wote waliojaliwa kuwa nacho na wale wasiojaliwa kuwa nacho!
Shukurani kwa kuwa nami,TUPO PAMOJA!

EDNA said...

Tupo pamoja kaka,asante kwa hadithi zenye mafunzo.

samira said...

ni funzo sama jamani mgongo wa dunia una mafunzo

Goodman Manyanya Phiri said...

...Pamoja kabisa! Na "maringo ni mwanzo wa kuanguka".


Saizi yake yule mama kwenye hadithi yako, Mkuu...lakini sisi binadamu hatujifunzi kamwe!!!

Faith S Hilary said...

Ndio maisha, kuna mitihani, hiki na kile na sote binadamu. Aliyefika juu hakuruka kimaajabu, alianza chini kwanza na kuna sababu mbali mbali kubaki chini ama kurudi chini...It's life as they say.