Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, May 16, 2011

Dawa ya moto ni moto-9



Bosi wa fedha, alisinyaa kimya, akimwangalia kwa kujiibia mke wake, ambaye alikuwa kashika kiuno huku kasimama katikati ya mlango, na kuujaza mlango wote, macho yakiwa yamemuiva kwa hasira, …
‘Mke wangu sikiliza, kikao kiliisha usiku saaana, kiasi kwamba…’ akaanza kujielezea bosi huku akiusogelea mlango pale aliposimama mke wake ili ampishe aingie ndani, lakini kabla hajamaliza kujieleza na wakati huo mguu ulikuwa umekanyaga kizingiti cha mlango , mlango ulifungwa kwa nguvu usoni mwake na kwa vile bosi alishakaribia kwenye mlango, alijikuta akigongwa na huo mlango  usoni…karibu adondoke! Alijikuna pua huku akiwa katahayari, akalijua leo ehe, kuna mambo. Akatamani arudi alikotoka, au aelekee kazini, lakini alijiangalia nguo alizovaa ndizo alizoshinda nazo  jana zilikuwa hazitamaniki kwenda nazo ofisini tena…
Akajipa moyo `mimi mwaume bwana…’ akauelekea mlango na kuufungua akiwa tayari kwa mapambano…`haiwezekani bwana, mke aninyanyase…hapana tutapambana…tu’ akasema kimoyomoyo, huku akitizama huku na kule kwa woga, akakuta kumbe mkewe hayupo hapo karibu na mlango, akaongoza hadi chumbani, ambapo alimkuta mkewe, akasimama ghafla, lakini alipomuoana mkewe kashika kichwa kainama chini,..akaingiwa na moyo wa simanzi, na majuto akataka kumsogelea na kukaa pembeni, karibu yake,. Lakini aliogopa, `usimchokoze nyoka shimoni..’ akajisemea kimoyomoyo…! Kwa harakaharaka, akachojoa nguo zake huku anamwangalia mkewe kwa kujiiba, akiomba ainame hivyohivyo, akachukua taulo, akavaa haraka, akaelekea bafuni!
Akiwa huko bafuni akioga,  mawazo mengi yakamtanda akilini. Alijiona kama mfungwa fulani, ndani ya familia ya mkewe! Alijiuliza hivi maisha kama hayo yana raha gani, ndio pesa anazo, maisha ya kifahari, lakini kuna raha gani. `Lakini mbona…nitakuwa nakosa shukurani kama nikilaumu hili kwasababu bila hii familia ningekuwa wapi…’ ,akajikuta akisema kwa sauti, Kiukweli kama isingekuwa familia ya mkewe, angelikuwa bado anasota, na huenda angelikuwa mchunga ngombe kule kijijini kwao, lakini familia ya mkewe ilimsomesha, ikamjenga hadi kuwa bosi wa kampuni kubwa. Alikumbuka jinsi alivyokutana na mkewe huyu.
Watoto wa familia ya mke wake kwa wakati huo ilikuwa ikiishi nje ya nchi, na baada ya mkataba wa kikazi kuisha, walirejea hapa nchini. Ni kipindi hicho ambacho baba mkwe wake alipokutana na familia ya bosi, ni katika mambo ya kikazi na majukumu, baba mkwe huyo akawa anatembelea zile familia zisizojiweza. Kati ya familia hizo ilikuwemo ya Bosi, na hapo Bosi akapata msaada wa kusomeshwa yeye na vijana wengine. Kipindi hicho Bosi hana mbele wala nyuma, akachukuliwa hadi Dar, na kukabidhiwa kwa jamaa mmoja , ambaye alikuwa ndugu wa baba mkwe.
Alikaa hapo huku anasoma, na alipofaulu akaenda kidato cha sita na hatimaye chuo kikuu. Alipomaliza masomo yake, akaajiriwa kwenye kampuni ya kawaida, akapata uzoefu wa kikazi, na kwa bidii yake mwenyewe, akaamua kujiendeleza zaidi. Baba mkwe wake wakati akiwa nje, alikuwa kafungua kampuni yake hapa nchini, ilikuwa  ikifanya vyema, na hata kuwa na matawi . Siku mkataba wake ulipoisha akarudi na kuamua kuiendeleza kampuni yake mwenyewe, na ndipo akakutana tena na bosi, akamkumbuka, na alipomsaili zaidi akagundua kuwa anafaa kuajiriwa katika kampuni yake!
Siku kadhaa, kampuni ikawa inasherehekea kumaliza mwaka, na Baba Mkwe na familia yake wakawa wamejumuika. Na siku hiyohiyo kulikuwa na kikao cha wanafamilia wa baba mkwe, na bahati nzuri, bosi alialikwa kama msikilizaji. Na katika pilikapilika za hapa na pale macho yake yakakutana na msichana mmoja mrembo, ambaye muda wote alikuwa akiongea Kiingereza, …mvuto wa yule binti ukamwingia sana Bosi, na lugha ille ikamwacha hosi kabisa, akajikuta akisema moyoni, huyu ndiye binti ninayemtaka, ukikaa naye utafikiri tupo Ulaya Akawa mara kwa mara anajiiba kumwangalia, na kutamani akutane naye, ili amuonyeshe kuwa naye yumo kilugha, na kulayaulaya ingwaje hajawahi kupafika. Bosi kwa kujikweza ndio mwenyewe!
‘Watokea wapi weye binti’ akamuuliza kwa kiingereza, pale alipopata bahati ya kukutana naye.
‘Natokea wapi, una maana gani kusema hivyo, mimi ni binti wa baba mwenye nyumba hii..’akasema yule binti kwa dharau
‘Ohh, ina maana huyu Mzee ana binti mrembo kama wewe…sikujua hivyo, samahani sana…’ akasema huku akijishusha maana anaongea na mtoto wa bosi wake. Na ile hali ya kujipendekeza na kujibaragaua kwa bosi, ikamwacha hosi binti, akaishia kucheka, na hapo akamwangalia vyema bosi machoni. Mhhh, binti naye akahisi matamanio ya nafsi ya kimteka akilini, akakiri moyoni kuwa kvutiwa na huyu jamaa. Hapo hapo akaamua kumtoa wasiwasi huyu jamaa ili ikiwezekana wawe karibu kimawazo, na mazunguzmo yakaendelea hadi kujuana na hata ikafikia kupeana namba za simu.
Ikawa mara kwa mara wanawasiliana  kwa simu, na hatimaye ikafikia kualikana chakula cha mchana,na baadaye kikawa chakula cha jioni, urafiki ukanoga. Na wazazi wakagundua kuwa binti yao ana mtu anamzuzua, wakachunguza wakagundua ni nani…!
‘Binti yangu, vipi nakuona wewe na jamaa huyu mumeiavana sana, …nakuonya sana, sitaki muwe marafiki na huyu jamaa, sio aina yako, ina maana umekosa watu wa aina yako…usinitie aibu, nataka uolewe kwenye familia za maana, kwani twataka harusi yako iwe ya historia…’akasema mama yake.
‘Acha kuingilia maswala ya watoto, kama wamependana hakuna haja kuwaingilia, swala ni kumshauri tu na hata kumuonyesha ni nani tungefurahi awe naye kama rafiki hadi mchumba.’ Akasema baba wa binti, na katika maongezi, baba akatoa nasaha zake akasema ` Binti yangu, huyo jamaa ambaye naona sasa mumeivana kiurafiki, kiukweli hamuendani kabisa. Huyu anatokea kijijini familia yao tunaijua vyema, …ni ya kimasikini kwa ujumla, na ujue kama ukiolewa na huyo jamaa, huenda ukaenda kuishi huko, je utayaweza maisha ya kijijini…?’ akamuuliza baba yake.
‘Baba mbona mumeenda mbali sana huko, kwani nani kawaambia kuwa tunataka kuoana, sisi ni mrafaiki tu, na sio urafiki kama mnavyozania nyie, ni kwa vile tumezoeana, basi…lakini sijafikia uamuzi huo, na kama ikifika huko kwani ni lazima niende kuishi kijijini na wazazi wake, kwani wazazi wake ndio wamenioa mimi…mimi na mume wangu tutaishi hapa hapa mjini, kama nikuwatembelea wazee wa mume tunaenda mara moja, tunasalimia tunarudi mimi sioni ubaya…’ akasema binti.
‘Sawa, sisi tunachotaka ni kukuweka sawa, kwa ujumla hatupo radhi na huyo jamaa …hatupendelei kabisa urafiki wenu, kwani mwisho wa siku itishia kubaya…na …tunakushauri tena, kuwa tafuta rafiki wa kukufaa maishani, usivutike na vitu vidogovidogo, mvuto wa sura siju, angalia mbali zaidi,..tumekusomesha ili uwe na upeo wa kufikiri…’ akasema baba wa binti.
 Binti hakuwaelewa wazazi wao kwa muda ule, alijua kuwa wanaongea kama wazazi na binti yao, lakini mwisho wa siku maamuzi ni yake mwenyewe. Ikawa kila mara akikutana na Bosi anajisikia raha ya ajabu, na kuomba kuwa ipo siku atakuwa mume wake. Na siku moja ikafika Bosi akamtamkia kuwa anataka wawe wachumba, na Binti akakubali, kwa masharti kwamba hata iweje, wasije kwenda kuishi kijijini.
‘Kwnini unasema hivyo, mimi maisha yangu nimeyajenga hapa Dar, kijijini ni kwa wazazi wangu, …kama nikwenda kusalimia ni mara moja kwa bahati…’ akasema Bosi. Na taarifa hii iakfika kwa wazazi wa Binti.
‘Tulishakuambia unapokwenda ni kubaya unaoana sasa, …unataka kusema kuwa sisi nii wajinga tulipokushauri kuhusu hili…hilo halipo na hatutakubaliana  nalo…’ akasema mama mtu
‘Mimi nipo na mama yako…hatutaki kusikia kauli kama hiyo, unasikia?’ akasema baba mtu.
Binti akapingana na wazazi wake kuhusina na msimamo wao na alipoona kuwa hawabadiliki, akawaambia ukweli kuwa yeye keshampenda huyo jamaa awe mume mtaraiwa kama wanataka , au hawataki, hajali kuwa yeye anatokea familia ya kimasikini au kitajiri. Wao wakae na utajiri wao, yeye yupo tayari kuishi kimasikini…akayatamka maneno haya na kuwaacha wazazi wao wakiwa hawaaminikuwa ndiye yule binti yao ambaye alikuwa akiongozwa na wazazi wake hukubali bila ubishi.
Baba mtu akaona mtoto sasa anampanda kichwani, akatoa hitimsiho kuwa hataolewa na huyo jamaa, kama kamuona yeye ndio kila kitu basi atabakia hapo nyumbani bila kuolewa. Wazazi walipogoma kabisa, binti akawa mgonjwa, akakataa kula, akawa hayupo karibu  na wazazi wake tena, mpaka wazazi wakaona binti kweli kaamua, ikawa haina jinsi, wakamuita Bosi na kumhoji kiundani …hatimaye wakakubaliwa kwa masharti makubwa.
‘Wewe umeamua kumtaka kumuoa binti yetu, ina maana unakuwa sehemu katika familia hii. Tunakuomba sana, sio kukuomba ila tunakupa onyo kuwa siku hatutapenda manyanyaso ambayo tunayaona kule kijijini, wanaume wanawafanya wake kama punda, kama bidhaa, tunasema, utakapokwenda kinyume na ndoa, ukamuumiza binti yetu kimwili, kimawazo, basi..ujue utapambana na familia hii…unamuona alivyo, kalelewa kiadabu, kielimu …ana afya yake njema, sasa, wewe umuharibu, tutaonana..’ akasema baba mkwe bila mzaha.
‘Baba huyu tuachie sisi, kama kaamua kuingia ndani ya familia hii, ni lazima afuate masharti ya familia, hatutaki kashifa, hatutaki kunyanyasana…unasikia …’ akasema kaka mtu siku ya kikao maalumu, akamgeukia shemeji mtarajiwa na kumuasa akisema `mimi ni kaka mmojawapo wa dada yetu, wapo wengine lakini wapo makazini, ipo siku utakutana nao, wote lengo letu ni moja, …kwa kifupi hatukuwa radhi sana na wewe, kwasababu tunakujua vilivyo, lakini kama dada yetu, mdogo wetu kakupenda, …tunakubali shingo upande, ila…chunga sana…’akasema kaka mtu.
Kwa kipindi hicho Bosi alikuwa kazimia kwa binti, hakujali hayo maneno, akawaambia wasiwe na wasiwasi, yeye kampenda kiukweli binti huyo na ataishi naye kwa amani na upendo. Na binti akafurahi na uchumba ukakubaliwa na hata harusi ikapangwa, na siku ya siku ikafanyika harusi kubwa ya aina yake.
 Bosi alipowaza haya na kukumbuka wapi walipotoka na huyu binti mwili ukazizima, akaogopa na kuogopa, akikumbuka kuwa jana alifanya kwa mara nyingine kile alichoonywa na familai hii asifanye, akajiuliza kwanini anatamani wanawake wakati anaye mke nyumbani, akashika kichwa huku maji yakimiminika kichwani, …na wakati anawaza hili akakumbuka kuwa wakati anatoka pale hotelini alikutana na mmoja wa kaka za mke wake, na huenda keshaongea na mkewe kuwa alikuwa kalala kwenye hiyo hoteli na huenda imejulikana alikuwa na nani.
‘Hebu niambie ukweli jana ulikuwa na nani huko ulikotoka, usinifiche kwa sababu najua yote yaliyotokea huku, ile kampunii anaimiliki baba, ingawaje kastaafu, lakini mengi yanayotokea mle nayajua, na huenda hata wazazi wanajua, …wewe unafikiri kitu kimeanzishwa na wanafamilia, watakosa kuwepo watu wanaotoa taarifa za kiofisi kwa wenye kampuni, unajidanganya,…yote nayajua toka mlivyomaliza kikao chenu na hatimaye kijimwaga sehemu za siri, kule mlienda kufanya nini….sema haraka kabla sijakubamiza..’ akasema mkewe kwa hasira. Bosi alivyosikia neno kubwamizwa akatabasamu na kutikisa kichwa, akakumbuka siku ile alivyoinuliwa juu kwa juu hadi kwenye meza ya ofisini…kweli mkewe ni kibonge, anaweza hilo, lakinii yeye ni mwanaume…akamwangalia mkewe, sasa hivi kwa dharau
Ila yale maneno ya mkewe, yalianza kumtia woga, inavyoonekana mkewe anajua ziaidi ya jinsi anavyofikiria , akajiumauma, akishindwa kujitetea, na kabla hajasema kitu simu yake ikaita, Akaitizama na kukuta ni namba ya Maua…akamtizama Mkewe kwa kujiiba, mkewe kwa muda ule alikuwa kalala kitandani katizama juu, ilionekana mkewe kuwa na mawazo mengi, au ndio alikuwa anasubiri jibu la swali alilouliza.
‘Mbona hupokei hiyo simu, …huoni inatupigia kelele tu, au ndio huyo hawara wako anayekupigia, umesahau kumuachia hela ya matumizi nini, ongea naye nataka kusikia nini anachokuambia, weka sipika…kama kweli sio hawara wako’ akasema mkewe akiinuka vile alivyolala na kukaa kitandani.
Bosi aliingalia ile namba mara mbili huku anajiuliza moyoni, kwanini Maua kaamua kumpigia simu, na anajua fika saa kama ile yupo na mkewe, na hata hivyo, wakati waliapoachana kwa hasira, hakutaraji kabisa kuwa atapata simu ya Maua. Hii iliashiria kuwa kuna jambo muhimu…au kuna kitu kimetokea kati yake na mumewe, je kulikoni…
‘Nipe hiyo simu nipokee kama unaogopa kupokea…’ akasema mkewe akinuka kuichukua.
‘Halloh, nani mwenzangu..’ Bosi akaipokea na kujifanya hajui nani anayepiga. Na kabla hajasema zaidi akasikia sauti za ajabu ajabu, kwanza ilianza kama mziki laini na baadaye, sauti ya mwanamke akilalamika kimahaba, na mara akasikia…alijihis mwili mzima ukitetemeka kwa woga, akajikaza kiume, lakini…na baadaye akasikia ujumbe kuwa ana mzigo wake hoteli ya maraha, aliousahau..afike haraka, la sivyo mzigo huo utamfikia mkewe….’
Bosi nguvu zilimusihia kwani wakati huo mkewe Alishamkaribia akitaka kusogeza kichwa kusikiliza nini kinachoongewa, kwa haraka bosi akafanya la kufanya, alisogeza kidole hadi sehemu ya kuzimia simu akaminye…tiii, simu ikazimika.
‘Ni nani huyo kakupigia…nimekuambia uweke sehemu ya spika,… halafu inaonekana kuna kitu kwanza umesita kuipokea na sasa unasikiliza tu, huongei kitu…mbona sisikii sauti..hebu nipe hiyo simu…’akasema mkewe, na Bosi bila ubishi akijua simu imeshazima akampa mkewe. Mkewe akaipokea na kuiona imezimika, akamwangalia mumewe kwa hasira, …halafu akaiwasha. Alianza kubonyeza bonyeza, na hatimaye akaipata sehemu inayoitaka, akatizama halafu akauliza
‘Huyu Maua ni nani wako…’akauliza Mkewe kwa hasira. Bosi alishangaa, kwani ukizima simu yake, simu zilizopigwa kabla hazionekani tena, akasahau kuwa mkewe nimtaalamu wa mitandao, anaweza akacheza na simu na kujua wapi imetokea….
‘Ni mfanyakazi mwenzangu…’ akajibu bosi kwa kujiamini.
‘Sasa kwanini alipokupigia hukupokea na baadaye ukazima simu kiujanja..’ akauliza mkewe
‘Najua huyo , ….anataka kuniluliza maswala ya kazi na hapa sio mahala pake, …na sikuizima, ilizimika yenyewe, labda chaji iliisha..’ akajitetea bosi.
‘Chaji iliisha wakati inonyesha hapa imejaa kabisa…usinifanye mimi ni mtoto katika mambo kama haya, ulipolala, mimii ndipo nilipoamukia, maswala haya ya mitandao na mawasiliano nayafahamu sana, na naweza kuyavuta na kujua nini mlichoongea …lakini kwanini niandikie mate wakati wino upo, ngoja nimpigie huyu hawara wako nijue nini alichokuwa akitaka kukuambia…sio kawaida yangu lakini hili limezidi mpaka…samahani kwa hilo’ akasema huku akiangalia ile namba, ili aipige.
Bosi jicho likamtoka, alijua kabisa mkewe akipiga ile simu labda ile sauti aliyoisikia , ataiskia pia mke wake, je ina maana Maua kafanya hivyo kumkomoa, au ana maana gani kufanya hivyo, au alitaka kufikisha ujumbe gani kwake, akaapa kuwa akikutana na Maua atamonyesha kuwa yeye sio kama anavyofikiria, hata hivyo akili ilikuwa sio yake tena alikuwa kachanganyikiwa, akitafuta jinsi ya kuhakikisha kuwa mkewe hasikii hayo aliyoyasikia…sasa afanye nini…..

Ni mimi: emu-three
Enhanced by Zemanta

2 comments :

Simon Kitururu said...

Usione kimya ! Tupo na fulu kufuatilia stori!

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli usione kimya tunafuatilia...hapo naona za mwizi zinakaribia... ngoja niendelee nijue ni nini kinaendelea....