Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, May 23, 2011

Dawa ya moto ni moto-12 Maua alipofika  kwenye ofisi yao akaingia ndani kwa mwendo wa haraharaka akilini akiwa na mawazo ya kutaka kujua nini kimefungwa ndani ya ile bahasha. Alikuwa kiwaza huenda ni kazi za kiofisi, lakini huo mtindo wa ile bahasha ulimtia wasiwasi. Haiwezekani iwe bahasha ya kiofisi, kwanza huyo aliyenipigia simu kuwa nina ujumbe au mzigo wangu ndiye huyo huyo aliyeweka ile sauti ya ajabu ajabu…na huenda akawa ni Bosi.
 ‘Kama ni bosi tuitaonana…akasema huku anaifungua ile bahasha, mara akakuta santuri ndogo ya DVD, imeandikwa `Part one’. …kwanini `part-one’ akajiuliza moyoni, `part two yake ipo wapi’ akaendelea kujiuliza. Akaitizama kwa makini huku akiwaza bosi wake kahifadhi nini ndani ya ile DVD…na kwanini mpaka aiweke kule hotelini na asiilete ofisini, kama ni ya kikazi! Hii inawezekana isiwe ya kikazi, au ni movie nzuri alitaka kunipa…hawa wanaume bwana huenda ni ya kimapenzi, ya kutaka kunirubuni…’ akacheka na kuikagua…halafu, akaiendea  computa yake  mezani kwake na kuiwasha. Na wakati anasubiri  computa yake iwake, akasimama na kuchungulia nje kwa kupitia dirishani, akaona pikipiki imesimama nje ya geti la ofisi, akakumbuka aliiona pikipiki kama hiyo kule hotelini.
‘Pikipiki hii mbona inafanana kama ili ya mume wangu, halafu kama sikosei, niliiona kule hotelini, na kama vile…’ akasikia sauti ya computa ikiashiria kuwa imewaka, akasahau mambo ya pikipiki na kuiendea computa yake , akaisogelea karibu na kuiingiza ile DVD ndani ya computa, huku moyo ukidunda kwa wasiwasi, akiwa na hamu ya kujua ni picha gani imo mule ndani….
                                                                                      ******
 Maneno alipofika kwa nje, akasimamisha pikipiki yake, na kusema moyoni, `ina maana kweli Maua kaja hapa kwa ajiuli ya  mambo ya kikazi, ‘Oh namuonea sana huruma mke wangu, kazi imemfanya hata asahau kuwa anaumwa na kichwa’, Alimuona mkewe akingia ndani ya ile ofisi, akasubiri kidogo akishindwa kuamua afanyaje sasa, kwani kuna yule mpanda pikipiki ambaye alikuwa keshafika na kusimama mbali kidogo na pale getini, alisubiri mpaka Maua alipoingiza gari ndani ya lile geti, naye akasogea taratibu na pikipiki yake.
 Yule muendesha pikipiki alipofika karibu na lile  geti, alisimama kidogo baadaye aliwaendea wale walinzi akaongea nawo kwa muda mfupi halkafu naye akaingia ndani na pikipiki yake kwa kupitia ule mlango wa pale getini. Hii ilionyesha kuwa na yeye huenda ni mfanyakazi wa humo ndani, `mbona katika kufika kwangu mara kwa mara sijawahi kuiona hiyo sura…inawezekana maana wafanyakazi hapa ni wengi’, akwaza Maneno,
Maneno alikaa pale aliposimamisha pikipiki yake kwa muda baadaye akaona haina haja kusubiri pale alipokuwa kajificha, ngoja ajitokeze akongee na wale walinzi kama inawezekana na yeye aingie ndani, na alipowatizama wale walinzi kwa ule umbali alipokuwa kasimama aliziona zile sura za wale walinzi kuwa ni ngeni kwake. Akalisogeza lile pikipiki lake hadi kwenye ule mlango wanapokaa walinzi, na kulisimamisha pikipiki lake na mara mlinzi akatokea na kuuliza anashida gani.
‘Jamani mimi ni mume wa Maua, nimekuja mara moja, kwasababu aliondoka akiwa anaumwa, sasa nilitaka nimjulie hali mara moja halafu niondoke zangu, natumai yupo ndani..’ akauliza Maneno.
‘Ngoja kwanza, …unasema wewe ni mume wa Maua…’ akasema yule mlinzi huku akimkagua kwa macho toka juu kichwani hadi chini miguuni halafu akarudisha macho kumwangalia usoni. `mbona kaja jamaa mwingine ana pikpiki kama yako, mimi nilijua ni wewe kwasababu kila mara ukija unakuja na pikipiki lako, sasa…hebu ngoja kwanza…’ Yule mlinzi kumbe alikuwa akimfahamu, akaingia kwa ndani na baadaye akarudi,
‘Yule jamaa mwingine mwenye pikipiki kama yako anaonekana anajuana na Maua kwasababu naye kaingia ndani, lakini…nina wasiwasi, ngoja nimpigie Maua nimuulize, maana dunia ya sasa imebadilika’. Yule mlinzi akasogelea simu ya mezani na kupiga namba za mle ndani, akasubiri kwa muda halafu akasema;.
‘Huyu dada inaonekana yupo busy sana hata hapokei simu..’ akasema yule mlinzi
‘Una uhakika kuwa huyu jamaa aliyeingia na pikipiki unamfahamu kuwa ni mfanyakazi wa humu ndani, hukumuuliza kitambulisho …au unamfahamu vyema,..au ina maana hapa watu wanaingia tu na wala huwaulizi hata kitambulisho, huoni inaweza ikaleta matatizo baadaye..’ akasema Maneno.
‘Labda matatizo uyaanzishe wewe,…huyu jamaa sio mfanyakazi wa humu, lakini anafika mara kwa mara kikazi, na mara nyingi anamuulizia Maua… kwahiyo hatuna wasiwasi naye, …unajua ndugu sisi hapa tuna miaka kumi hapa, watu wanaingia wanatoka, lakini hatujawahi kupata tatizo kama unavyodhania wewe. Unasikia, labda kwa vile mkeo anaumwa ndio maana una wasiwasi. Kama unataka ingia kamwangalie, maana sisi tunajua nini tunachokifanya, mtu mbaya utamuona tu…hajifichi..’ akasema yule mlinzi akinadika kitu kwenye daftari lake, na kabla hawajaendelea na mazungumzo yao, mara likaja gari, na kusimama pale mlangoni, na mlinzi akakurupuka na kudondosha lile daftari chini, na haukujali kuliokota…Bosi kaingia, mkuu wa pesa, …Mlinzi alikimbilia geti  akafungua mlango harakaharaka, lakini lile gari  badala ya kuingia likasimama pembeni kwa muda na mara akatoka mwanamke na kuelekea barabarani, na kumuacha mwanaume akiwa ndani…
 Bosi na mkewe walisharuhusiwa na yule traffic na wakawa wanaelekea ofisini, na kipindi hicho mkewe alishakasirika kutokana na tukio hilo…., alikuwa hana hamu na safari yenyewe, alipanga kuwa akifika huko       ofisini mwa mume wake, anachukua taxi na kurejea myumbani, kwani kamuona mume wake ni limbukeni , anaweza kumuingiza kwenye matatizo ambayo kwake anayaona sio ya msingi, lakini akilini alikuwa katekwa na yale maneno ya kaka yake kuwa mume wake anawindwa na kundi haramu ambalo linatafutwa na polisi…Kwanini sikumuuliza kaka zaidi kuwa ni kundi gani hilo…akawaza na kutikisa kichwa kuwa muda ule haukuwa muda muafaka kusikia jambo jingine. Akaahidi akirudi nyumbani tu atampigia kaka yake simu ajue ni kundi gani hilo…
`Kundi gani hili, na kwanini awindwe…’ akajikuta akisema kwa sauti
‘Unasemaje mke wangu…sikukusikia vyema, …nimesikia kama umesema kitu,…?’ akauliza Bosi, huku akigeuka kwa kujiiba kumwangalia mkewe, alipoona kimya akasema `mke wangu nashukuru sana ulivyowaweka vyema wale traffic maana jamaa hawa wakikukuta na kosa, ujue itakutoka mfukoni, la sivyo umeadhirika…’ akasema Bosi huku akitabasamu
‘Mimi naona unishushe hapo, nachukua taksi, narudi nyumbani, naona `unani-bore’ tu, huna lolote la maana, watu kama nyie, hamna la kufikiri kichwanii zaidi ya chupi za wanawake…’hopeless’…’ akasema na kusonya.
‘Chupi za wanawake? …imekuwa hayo tena mke wangu, mimi hayo sina kabisa, hayo ni mawaza yako tu mke wangu, ungelijua ninavyokupenda usingelisema hayo, …mambo mengine unayohisi hayana msingi kabisa labda…mmmh au ni wivu mke wangu…lakini kama ni wivu ni bora maana najua nina mtu anayenipenda pia…’ akasema huku akisimamisha gari kwenye geti la ofisini. ‘Sasa tmefika, sijui…’ akajikuna kichwa.
Mkewe hakusema kitu, akatoka nje ya gari huku akisonya… , na kabla hajaita taksi, akawaza jambo na kugeuka kumwangalia mume wake ambaye alikuwa akiingiza gari kwenye geti la ile ofisi, akamfuata kwa nyuma, na kuingia ndani ya geti, akatizama na kuona gari jingine limesimama kwenye maegesho ya magari , akatikisa kichwa na kusema `kumbe Malaya wake yumo humo ndani, ngoja nikamshitukizie…
   Maua alikuwa akiangalia ile DVD mwili ukiwa umekufa ganzi kabisa, hakuamini nini kile alichokiona, hakuamini kuwa kweli alikuwa yeye kwenye ile picha, akili yake haikukubali kabisa kuwa ni yeye, lakini kila hatua ilionyesha ni yeye, na jinsi alivyotoka kule sehemu waliokuwa wakifanya karamu na wafanyakazi wenzake, halafu akaombwa na bosi wake waende chumba cha ndani ili wakaongee, na huko ndipo machafu yalipoana kutokea.
 Mkanda ule uliendelea hadi walipofika sehemu akaanza kuvua nguo kama mwenda wazimu, anavua na kutupa huku na kule wakaingia chumbani, na hapo mkanda uaksema unaendelea sehemu ya pili. Maua kwa hasira akaitoa ile DVD kwenye computa na kuiharibu haribu, kwa kuikanyagakanyaga, na kabla hajaondoa yale mabaki ya ile DVD, akasikia sauti kama ya mtu anaingia ofisini, akazima computa yake haraka na kufungua mlango wa ofisi yake na kuchungulia sehemu ya ofisi kuu ambapo hukaa wafanyakazi wengi, akatizama huku na huko, hakuona mtu.
 Alipohakikisha kuwa hakuna mtu akarejea kule ofisini kwake na kuangalia yale mabaki ya ile DVD, akahakikisha kuwa hakuna kinachoweza kuonekana tena, akayaokota yale mabaki na kuyatumbukiza kwenye ile bahasha na kuitumbukiza kwenye kapu la takataka. Huku akiwa akili ikiwa imehamaki, mara akaona kikaratasi kilichonadikwa namba ya simu, …alikumbuka kuwa kilidondoka wakati anaitoa ile DVD akaitizama akaona ngoja ajaribu kuipiga ile namba, akaelekea kwenye simu ya mezani kuanza kuipiga ile namba, na mara akasikia upande wa pili ukipokea na kusema halloh nikusaidie nini..
‘Wewe ni nani …’ akauliza Maua kwa hasira.
‘Wewe ndio umepiga halafu unaniuliza wewe ni nani, jitambulishe wewe kwanza halafu na mimi nitakuambia mimi ni nani..’ ikasema sauti ambayo ilikuwa kama inakwaruza kwaruza.
‘Unajifanya mjanja sio, wewe ndio umetengeneza hii DVD, ili kuniharibia maisha yangu, nini lengo lako..’ akasema Maua kwa hasira.
‘Unanichekesha kweli wewe binti, `eti tunakuharibia maisha yako’ …tumekuharibia au umejiharibia maisha  yako wewe mwenyewe, kwani ulipokuwa unafanya huo ufusuka kuna mtu alikulazimisha, nyie watu namna gani, mpewe nini ndio mrizike umepewa kila kitu, mali mume, na unaishi kwenye familia inayokujali, huko ngoja nikuache…lakini kiukweli hiyo ndio adhabu ya mzinzi! Hebu nikuulize, lakini sitaji jibu, wewe si una mume, na mume ulimtaka mwenyewe,…leo unamwacha mume wako nyumbani unakwenda  kuzini na mume wa mtu…mnzizi kwa mnzizi, …ok huko sitaki maneno mengi, ila nakuambia hivi hiyo DVD ni mfano tu wa DVD ambayo inatakiwa kuingia sokoni, …ile yenyewe utaletewa muda si mrefu, na ukumbuke kuwa kuna sehemu ya pili yake…ikionyesha tendo lenyewe…hahaha,…tendo lenyewe, mchi kwa kinu…aisee kweli wewe binti mkali kweli…unajua mkali basi ukiiona hiyo DVD, utahakikisha hilo’ akatulia na wakati huo Maua alikuwa kama kamwagiwa maji ya baridi hawezi kuinua hata mdomo kuongea
 Mara kwenye ile simu ikasikika sauti ya mlio wa picha au DVD iliyokuwa ikichezwa upande huo …Ilikuwa sauti ya Maua, dhahiri kabisa… akiwa kama analalamika au kulia kimahaba…halafu sauti ile ikanyamazishwa na huyo jamaa. Jamaa huyo upende wa pili wa simu akahema kwa nguvu, na akasema `Duuh, mimi mwenyewe hapa nipo hoi,…Maua wewe mkali…hivi hayo ulishindwa kuyafanya kwa mume wako. Kiukweli sehemu hii ya pili imekamilika ipo mbioni kuingia sokoni,…kama…narudia tena kama…’ akatulia na baadaye akaendelea kwa kusema,`…sikiliza kwa makini Maua, ujue mimi ni sehemu ndogo tu ya wahusika, mimi natumwa kuchukua picha kama hizi, kama tenda, wao waliniagiza kwasababu nakujua…kwasababu naijua kazi yangu, kwasababu sifanyi makosa,…’ akanyamaza halafu akakohoa
‘Maua, binti mrembo, unayejua kazi yako vyema, unaweza ukawa muuigizaji mzuri wa mambo haya, kiukweli una kipaji, lakini sio hulka yetu Waafrika, au sio, sasa Maua,…mimi nina uwezo wakuwadanganya hawa walionituma kuwa haikutoka vyema,…au uwongo wowote ninaoujua mimi nikaizima kia-aina, sio mara ya kwanza kupewa tenda kama hii nikaizima kia-aina, kwanza tunaomba,  uinunue hiyo sehemu ya kwanza,…ili kuwalipa washiriki…’ akasimama kidogo na kuhema, halafu akakohoa.
‘Unajua kazi kama hii ina washiriki kadhaa, ili kukamilisha hii kazi, hawa watu wanatakiwa kulipwa….wapo washikaji walioshiriki hapa na pale, natakiwa niwafumbe mdomo, hiyo ni kazi rahisi sana kwangu…lakini siwezi kuwalipa kwa pesa zangu, pesa zenyewe nitapatia wapi…wasiwasi wangu ni wewe kama ukichelewesa, ikawafikia wadau, sina jinsi, sina uwezo wa kuwazua hawo bwana wakubwa, hawaambiliki, hawasikii kitu, hawajali…wamkubuhu kwa kazi hiyo…kwao pesa kwanza, mengine baadaye…wapo tayari hata kuchukua picha za wazazi wao wakaziuze Ulaya…sembuse wewe mtu baki. Sasa twatakiwa tufanye haraka kulinyamazisha hili,
 Sasa Maua ili taarifa hii isisambae zaidi, hadi kufika kwa waandishi wa habari, kwasababu hawa jamaa wakiamua wanaipeleka kwanza huko kwa wadaku ili soko lipande zaidi…unajua wewe ni mtoto wa wakubwa, taarifa kama hii ikifika kwa waandishi wa habari wa udaku…mungu wangu….oh, masikini Maua…nakuonea huruma, lakini ndio hivyo, sikupenda kabisa kushiriki kwenye kazi hii, lakini nililazimishwa kwanza na njaa, pili na hawa wadau…na kiukweli na mimi nataka kula, kuishi kama wewe….!Kwa ujumla kwa  mahesabu ya harakaharaka kama nitawapelekea wadau hatutakosa milioni ishirini hivi, kwa bei ya jumla, na kama ni bei ya rejareja hutaamini mahesabu yake, na hii nakuambia ukweli inauzika…kazi hii nimeifanya sana, picha hii imetoka bomba…inauzika kiukweli…’ akanyamaza kama anahema.
Alipokohoa ilikuwa kama radi iliyopiga sikioni mwa Maua, ikawa imemzindua kutoka kwenye kuganda kwa mwili, akatizama huku na kule, kuhakikisha kuwa kweli hakuna mtu mwingine, hakuamini kuwa yupo peke yake…alihisi kuwa kuna mtu mwingine  anasikia kile anachokisikia. Mara akasikia tena jamaa akikohoa halafu …. !Na hapo Maua alitamani dunia imu-meze asisikia yale tena yale Maneno ya huyo jamaa, alitaka kuikata ile simu, lakini nguvu hizo zilikuwa bado hazipo, utafikiri kashikwa uwezo wake wa kufanya chochote
`Unasikia dada yangu wabongo wanapenda sana kanda kama hizi, hutaamini kuna tenda tumaifanya wiki mbili zilizopita tumeshaingiza milioni 30, tena hapo hawa wadau zetu wametuingiza mjini…lakini hela hiyo tulipogawana, na …kufanya machafuzi, starehe…wiki mbili tukabakia mikono mitupu, kazi hii haina Baraka, najua hilo…lakini ukionja asali basi tena, watamani kuonja tena….bei kama hiyo ni hapa bongo tu, lakini kama tunataka dola nyingi …huwa tunatuma huko majuu, wao wanajua jinsi gani ya kuitafutia soko, wapo mawakala wetu huko…’ akahema huyo jamaa kama vile anatua mzigo mzito.
‘Lakini dada yangu nakupenda sana, hasa mimi nakujali sana…najua …huenda haikuwa nia yako…huenda….kuna namna zimefanyika, lakini ndio kazi ilivyo…ni tendo linalohitaji ujasiri…na mtu kama wewe ukiwa kamili huwezi kulifanya,….hutaamini kama ni wewe, hutaamini ulipata ujasiri wapi wa kufanya hivyo…na hata ukiangalia hii kanda, haionyeshi kuwa uli…pata kitu kuongeza munkari, inaonyesha kabisa ulikuwa ukitamani, na kuifurahia kazi yako…, inaonyesha kabisa ulimkamia jamaa….
‘Sasa mimi sitaki uazirike kiasi hicho, kwahiyo, tuzungumze kibiashara, mimi nina shida ya pesa na wewe unazo pesa ambazo …mmh, ndio hizo mnazifuja ovyo kwenye mahoteli,…ok,hainihusu matumizi yako, lakini…hali ngumu, naomba tusaidiane kwa hili…toa hiyo hela tufunge hiyo tenda, na tutasahau kabisa kama kilikuwepo kitu kama hicho…kiukweli nakuomba sana…tena sana, …hivi sasa naongea kiurafiki, lakini ikifika muda wa matendo, hutaamini kuwa ni mimi… nisingependa kabisa tenda hii iingie sokoni kwa hawa jamaa,  …’ akakohoa tena
`Dada yangu , hiyo ni sehemu ya kwanza, toa hizo gharama, elifu ngapi vile, …sio nyingi sana kwako, 20 tu  kwa sehemu za million millioni, ili tuongelee sehemu ya pili, ambayo ….oops, hata wewe mwenyewe usingepedna kuiona…inatisha, na hata mimi siamini kuwa ….nisiongee mwengi, kazi ni kwako… tutaongea sehemu ya pili utaipataje hapo tutakapoona ushirikiano wako na sisi upoje…na kumbuka pia huenda baba sio baba…swala la urithi, …baba akiiona hii unafikiri atakukubali wewe kuwa ni mwanawe tena…kuna swala la kuaibika…hebu fikiria utaficha wapi macho yako kanda kama hii ikisambaa dunia nzima…nakuomba ufikirie sana hili….tunakupa masaa 24! Njia ya kuipata hiyo hela ni rahisi, utaipata ukiipata weka kwenye bahasha , itume kama ulivyotumwa hiyo DVD, hakuna shaka sisitutaipata bila wasiwasi…kumbuka masaa 24, baada ya hapo tusilaumiane’ ile sauati ikasema na kutulia
 Mara nguvu zikamjia Maua na kuinuka huku kaishikilia ile simu kwa hasira, mwili ulimtetemeka, na kama huyo mtu angekuwa karibu naye angemharibu…na kama angekuwa na silaha asingesita kuitumia, akaitizama ile simu…na kwa hasira akasema ‘Wewe mtu….Mwanaharamu mkubwa wewe, kumbe ndio nia yako,…mnaishi kwa kazi za haramu kama hizo, wewe …eti unasema baba sio baba , wewe unamjua baba gani wewe, na sizani kama una wazazi…’blackmailer’ mkubwa wewe…Nakuambia hivi mimi sinunui huo uchafu wenu, na wala sifanyi kitu chochote,…sikia wewe mwanaharam, ibilisi shetani mkubwa wewe… hupati hata senti moja toka kwangu… wewe fanya utakalo…’ Maua akaibamiza ile simu sehemu yake ya kuwekea aliposikia kicheko kikubwa kikitoka toka kwa yule mtu. Alibakia katoa jicho la hasira huku akihema na mwili mzima ukitetemeka kwa hasira…’ Na mara akasikia mlango wa ofisni kwake ukifunguliwa…na kitu kama bahasha ikarushwa kwa ndani na mlango ukafungwa.Na akasikia mtu akikimbia na mlango wa nje ukafunguliwa na kufungwa….
Je ni nani huyu kaingia, kuna nini kitaendelea, na Maua atachukua hatua gani? 

Ni mimi: emu-three

6 comments :

Mfalme Mrope said...

kisa kinatisha na kusisimua!! Usichelewe basi kuweka sehemu inayofuata. Can't wait!!

emu-three said...

Mkuu Mrope hata mimi hapa kichwa kinawaka moto, maana muendelezo wake ushapangiliwa kichwani, lakini mmmh, ....ofisi za watu hizi, nahangaika watoto wapate choo kwanza, ...kwa ujumla nitajitahidi iwezekanavyo...kwanza naomba maoni ya watu kuhusu sehemu hii, niende kihivyohivyo au niongeze kidogo...!

Anonymous said...

dah! nenda hivyo hivyo miram3 yani kisa hiki kinatisha. maskin maua.cant wait either

samira said...

m3 nenda hivyo hivyo jamani mauwa nimeipenda hii
thanks m3

Yasinta Ngonyani said...

nanukuu "‘Wewe mtu….Mwanaharamu mkubwa wewe, kumbe ndio nia yako,…mnaishi kwa kazi za haramu kama hizo, wewe …eti unasema baba sio baba , wewe unamjua baba gani wewe, na sizani kama una wazazi…’blackmailer’ mkubwa wewe…Nakuambia hivi mimi sinunui huo uchafu wenu, na wala sifanyi kitu chochote,…sikia wewe mwanaharam, ibilisi shetani mkubwa wewe… hupati hata senti moja toka kwangu… wewe fanya utakalo…’ Maua akaibamiza ile simu sehemu yake ya kuwekea aliposikia kicheko kikubwa kikitoka toka kwa yule mtu. Alibakia katoa jicho la hasira huku akihema na mwili mzima ukitetemeka kwa hasira…’ Na mara akasikia mlango wa ofisni kwake ukifunguliwa…na kitu kama bahasha ikarushwa kwa ndani na mlango ukafungwa.Na akasikia mtu akikimbia na mlango wa nje ukafunguliwa na kufungwa….
Je ni nani huyu kaingia, kuna nini kitaendelea, na Maua atachukua hatua gani?" mwisho wa kunukuu:- ni kisa kinasikitisha pia kinachekeshe kidogo yaani kusisimua. Nimependa kipengele hicho nilichonukuu kuona Maua kapata nguvu na kujibu hivyo. Khuhusu vipi uendee napendekeza andelea vivyo hivyo.....

Candy1 said...

Duh!! nimekaa kwenye kiti huku nasoma hiki kipande yaani nahisi kama kiti kinataka kuwaka moto! Jamani jamani "blackmailing" sio kitu kizuri oooo..mtu hata haoni huruma kisa njaa...M3 mi nipo kama kawa macho hayaondoki hapa...maskini Maua :-(