Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, April 29, 2011

Dawa ya moto ni moto-5



Maua alijikuta anatetemeka mwili mzima, hata hakujua kwanini, akawa anaogopa kabisa hataki kuangalia huko mlangoni, mawazoni mwake alikuwa akimuonea  huruma mama yake, alijua nini kitafuta baadaye. Kwa jicho la kujiiba, aliona mkono wa mama yake ukificha kitu kwa haraka, naye akajisogeza pembeni ili kumkinga mama yake kwa lolote litakalotokea, ni heri aumie yeye, kuliko kumuachia mama yake aumia. Halafu kwa haraka akageuza shingo kuangalia ni nani aliyeingia mlango, ingawaje moyoni alishajua kuwa ni nani…
 Kweli hisia zake zilimtuma vyema, kama alivyotegemea, hakuwa mwingine, ni yule yule Simba wa ndani, maana yeye akiingia ndani hata kama tulikuwa tukiongea tunakuwa kimya, simba kaingia, … akazidi kuwaza Maua,…alipofika hapo kimawazo Maua akacheka, aliona huo ulikuwa ni utoto, …ulikuwa ni utoto haiwezekani afanyiwe hivyo kwa sasa, hayo yalikuwa maisha yake ya nyuma…akapiga meza kwa ngumi, kama vile anaidhibu, akasonya na kusema, ….sasa nimekuwa …
 Alikumbuka jinsi gani watoto wote walivyokuwa wakiwa wanyonge, hata yeye …ambaye alikuwa kipenzi cha baba …kwani cha ajabu licha ya kumuogopa baba yake, baba alikuwa akimuonyesha upenda sana Maua, akirudi atamwinua na kumpakata, na atamuuliza  maswali mengi, na mwishowe anampa zawadi.
 Je kwa mtindo huo isingeingia akilini kusikia dhana kama ile, `kuwa huenda yeye sio mtoto halali wa baba huyu..hili halikumuingia akilini kabisa Maua. Akajisemea moyoni, hata kama mama kanikataza kumuuliza baba kuhusu aliyoyasikia, ipo siku atamuuliza kwanini alitamka maneno kama yale.
Baba alipoingia na kuwakuta Maua na mama yake wakiwa katika ile hali, na kumuona mama akiwa analia, akahisi kulikuwa na jambo lisilo la kawaida, alijifanya kama hajaona kitu, aliwapita kwanza, alipofika mbele kidogo alihisi kama kakosea kukagua kitu, akageuka na kuwasalimia wote kwa ujumla, lakini mama kama kawaida yake akakaa kimya,… Maua akiitikia na kutoa shikamoo. Maua akamtizama mama yake aliyekuwa katizama chini, akificha macho yake yaliyokuwa na machozi, akiijitahidi kujifuta machozi haraka, huku akijifanya ana mafua. Maua naye kwa harakaharaka  alimtizama baba yake, kuhakikisha kuwa labda alikuwa hajamgundua mama yake kuwa alikuwa kafanya kile alichomkataza, na sasa alikuwa kama analia… Macho ya Maua yakatua kwenye  macho ya baba yake ambaye alikuwa kasimama akiwaangalia. Alionekana dhahiri kukerwa na kitu fulani…!
‘Maua nakuomba uje nataka kuongea na wewe,… au mna maongezi gani na mama yako, naona kama …’ akasita na kutaka kuja pale walipokaa Maua na mama yake, lakini akaghairi na kutokomea ndani kwenye chumba chake maalumu cha maongezi, Maua alimwangalia mama yake ambaye bado alikuwa kainama chini,…mama yake  akamuashiria kwa mkono kuwa aende kwa baba yake, huku akitafute kile alichokificha awali…. Maua akainuka haraka, huku akimwangalia mama yake kwa mashaka, na huku anafikiria nini baba yake anachomuitia,…na je inawezekana ni nafasi nzuri ya kumuulizia yale yanayomkera, akasema moyoni huo sio wakati muafaka…
Alipofika chumba maalumu cha baba yake alimkuta akifanya kitu kwenye komputa yake, akaashiriwa akae,…alikaa kwa muda kama vile kasahauliwa kuwa yupo, lakini baadaye akasikia kauli ya baba yake, ikimuita, kwani naye usingizi ulishamchota pale alipokuwa amekaa, alipofumbua macho yake akakuta baba yake akimtizama machoni kwa muda , mpaka Maua akaona aibu na kutizama chini.
 Ndipo akaanza  kumwambia Maua maneno, maneno ambayo kayaambiwa tena hivi karibuni, pale alipokutana na baba yake, alikutana naye baada ya kitambo kirefu, kwani huwa hana mazoea ya kukutna na baba yake, labda kuwe na shughuli muhimu, hasa tangu alipoolewa. Aliyakumbuka sana maneno hayo, ambayo hujiruidia rudia sana kichwani mwake…i
Mwanangu nimekuita hapa leo, unajua tena mimi ni mzee, na sipendi kuishii kiajabu-ajabu, lazima niwe karibu sana na wanangu. Usipende kudekezwadekezwa na mama yako…mimi nakupenda mwanangu, ushakuwa msichana mwenye akili…mama yako anafikiri sikupendi, kwanini nisikupende wakati wewe ni mwanangu…achana naye, ila ninachotaka kusema ni kuwa naomba uishi vyema katika maisha yako, uolewe na upendane na mume wako,kama ni lazima umsaidie mumeo, …ila naomba sana usimsaliti mumeo, ni kitu kibaya sana katika ndoa…kama unavyojua mimi nafanya kazi  nyeti sana, hazihitaji kashifa…,
Maua aliamua kuyaandika haya maneno kwenye komputa yake, akiwaza kwanini baba yake akayarudia tena maneno yaleyale, yakiwa na ajenda ile ile. Akayasoma mara nyingi bila kupata jibu, lakini kilichomkwaza zaidi ni kile kisa cha mama yake mzazi na mtunza bustani, kilionekana ni kisa kilichohitaji umaliziwaji, ilikuwaje pale mama alipoingia chumba kile, aliona nini, je mama yake aliona nini siku le alipofika kule kwa mtunza bustani, je aliuwawa huyo mtunza bustani, je yupo hai, je ni baba yake….ikawa ni tungo tata…
Maua alipofika hapo kimawazo, akajikuta machozi yanamtoka, akamkumbuka sana mama yake kipenzi, alimkumbuka jinsi gani alivyompenda, licha ya mapungufu yake ambayo yalimfikisha kubaya, na huenda alikuwa na kitu kilichokuwa kikimkwaza mpaka akafikia hapo…akaondoa mkono shavuni, akashika kidevuni…akasema, lakini kwanini mama umeniweka kwenye mawazo kiasi hiki…oh mama nakupenda sana mama yangu..!
 Maua alitamani sana kumuulizia baba yake ukweli wa maisha yake, lakini aliogopa, aliogopa kwasababau mama yake alimkataza, na pia alimuogopa kama alivyokuwa akimuogopa siku nyingine, licha ya kuwa karibu naye sana, lakini hata hivyo kila mara alipojaribu kutaja jambo kuhusiana na mama yake, baba alimkatisha na kumwambia asijaribu kutamka tena jambo kuhusina na mama yake, kwanai anaumia sana moyoni…
 Maua akaangalia juu huku kaegemea kiti chake na kusema kwa sauti ndogo, `Kwanini mama alishindwa kuniambia ukweli, na je kuna nini kimejificha kati yao, kwanini tangu niwe na akili mama na baba wamekuwa hawaelewani,..’ akajiuliza kwa sauti ndogondogo, halafu akatabasamu, alitabasamu alipokumbuka siku zile na mama yake kuwa aliona mabadiliko ambayo yalimpa faraja alishangaa alipomuona baba anamnyenyekea sana mama yake isivyo kawaida, na hata kuongea naye kimapenzi, na ndipo aliposhukuru kuwa sasa huenda wazazi wake wamejirudi, lakini kumbe…..Alipofika hapo akashika shavu.
Kipindi mama yake akiwa katika hali hiyo ya kulewa na hata hataki kusikia la mtu, ndicho kipindi Maua alikuwa akisoma chuo kikuu, na  mara kwa mara alikuwa akirudi nyumbani kuwajua hali, na likizo yake aliitumia akiwa nyumbani mara chache sana alikuwa akitoka nje ya jiji hili. Safari ambazo alikuwa akimalizia masomo yake, ndicho kipindi ambacho alishuhudia  mama yake anavyoisha, afya ikiwa sio njema, kiasi kwamba aliogopa..na hata kumwambia baba yake aonavyo yeye, akamuomba baba yake amtafutie dakiatri bingwa wa watu waliozidiwa na pombe, …baba yake alimwambia kamtafutia sio mmoja, wengi tu lakini haikusaidia, imukuwa kama sikio la kufa ambalo halisikii dawa. Maneno haya yalimkatisha tamaa kabisa Maua…`sikio la kufa…, hapana mama sio sikio la kufa…lazima niwaambie akina kaka waje tumkalishe kikao mama…’akaweka hilo moyoni
Aliikumbuka siku moja aliporudi toka chuoni akamkuta mama yake yupo nje ananyweshea bustani, alifurahi moyoni, kuwa kamkuta mama yake hajambo, kwani mara nyingine anamkuta ama kalala au anakunywa pombe, au kazidiwa na pombe, ni wa kubebwa kuplekwa ndani, lakini siku ile ilikuwa tofauti. Mama kavaa vizuri, …oh, mama huyo, alitamani kusema vile, lakini aliona asimshitue, …akasogea taratibu hadi aple alipo mama yake, na mama yake alipomuona akaacha ile kazi, akampokea wakaingia ndani
‘Maua mwanangu umerudi likizo au ndio umemaliza chuo, maana huko kusoma hakuishi..’ mama yake aliinua kichwa akiwa kaka kwenye kochi kubwa akiwa kajilaza, na kipindi hicho baba yake alitoka ndani alipokuwa kajipumzisha na kuja kukaa pembeni ya mkewe,  hii ni mara ya pili anaporudi nyumbani na kuwakuta katika hali hii, alimwangalia mama yake akiwa kadhoofika, na alihisi harufu ya pombe kali,…akamwangalia baba yake.
Baba yake naye alionekana kukonda, licha ya uzee, lakini alionekana hana raha kama kipindi chake cha nyuma, tabia yake ilikuwa ujasiri na amri, alikuwa hababaishwi na kitu, lakini hali aliyomuona nayo ilionyesha kuwa anatatizwa na jambo, akaona labda ni matatizo yao ya kutokuelewana, akajaribu kuulizia kiujanja kuwa kuna tataizo ndani ya familia, jibu alilolipata lilimshngaza sana.
‘Mwanangu, unavyotuona tupo kama ile enzi yetu ya fungate, kama mungu angetubariki akatudisha miaka ya nyuma nahisi tungelifanaya vyema katika ndoa yetu tungelionyesha jamii kuwa kweli sisi ni mke na mume…lakini uzee ukija hauna dawa, uzee ni mtihani, …unafikia hatua unawaza makosa yako, unashindwa jinsi gani ya kuyarudi kwani mengine hayawezekani tena, yalwezekana kipindi hicho, …’ akasema baba.
‘Ndio mtihani huo, mimi sijali tena, nimeshapoteza ujana, nasubiri kifo, sijali kabisa, sijui kama niliwahi kupata raha katika ndoa yangu, lakini nakiri sasa baba yako kajirudi, tupo pamoja, ananipenda, sijui kwa vile anajua ndio naishia…sijui, atajaza mwenyewe..’ akasema mama, akiangalia pembeni kutafuta kinywaji.
‘Hayo ndiyo ya mama yako, hawezi kuongea mpaka anywe, hawezi kuizua,nimejaribu kila njia, nimeshindwa, nimetafuta madakitari bingwa wa kumshauri ieshindikana, sasa namwachia mwenyewe, maana, yeye sio mtoto mdogo, kama anapenda tama yake ya pombe kuliko sisi, kuliko watoto…tutafanyaje’ akasema baba mtu.
‘Acha kabisa kuingiza watoto wangu, nawapenda sana, kuliko chochote,..kuliko hata,,,kinywaji, pombe, sio kwamba naipenda, naitamani tu…nawapenda sana watoto wangu ndio maana nakunywa pombe, vinginevyo ningeshawakimbia zamani, nikajaribu maisha mengine, nimevumia yote kwa ajili yao…hii kunywa yangu ni kafara niliyojitolea kwa ajili yao, mtalaumu sana, lakini hamjui nini kinanitesa, nini kimenivuta mpaka kufikia hali hii…na hakuna atakayejua ila muumba peke yake, najua atanisamehe kwa hili, kwani sikupenda kabisa iwe hivi…’ akaanza kukohoa mfululizo. Hii iliashiria kuwa kuna tataizo jingine la kiafya, na wanalijua wazazi wake.
Maua alipoona mama yake anakohoa vile akajaribu kudadisi kuwa kuna tatizo jingine, baba yake alimwambia hakuna,takuwa anakohoa kwasababau ya kunywa, koo ni kavu, lakini hakuna tatizo ingine…asiwe na wasiwasi.`Unajua mwanangu mama yako akiacha pombe, yupo safi kabisa, afya yake itarejea kama zamani, lakini hanielewei…’ akasema baba. Maua hapo hakukubali akilini alijua kabisa kuna madhara yameshamuathiri mama yake na huenda hawataki kumwambia kwa vile yupo shuleni.
Maua alikumbuka docta alivyomwambia mama yake siku moja, kuwa kama anataka afya yake irejee vyema, inatakiwa aache pombe kabisa. Na siku ile mbele ya docta baba yake alisema kwa hasira kuwa kajaribu kumkanya mke wake aachane na pombe kali kama alivyofanya yeye lakini hakukubaliani naye kabisa.
Baba yake aliacha pombe kali , na baadaye akaamua kutokunywa pombe kabisa hasa pale aliposhauriwa na dakitari, lakini haikuwa hivyo kwa mama yake.
‘Mama kwanini unajiua mwenyewe kwa pombe, halafu pombe zenyewe ni pombe kali…? Siku moja akamuulizia mama yake
‘We acha tu mwanangu, pombe ndio …kila kitu kwangu sasa,… lakini mwanangu usiwe na wasiwasi kwani ipo siku,… ipo siku hamtapata usumbufu wowote toka kwangu…nitaacha pombe,..kabisaaa…na hamtasumbuka tena na mimi…’ akasema mama yake meneno hayo kilevi levi.
‘Mke wangu hebu sikia maneno ya mwanao hata kama mimi hutaki kunielewa, mwanao anakupenda sana, ukiendelea kunywa unamtia simanzi, na mwisho wake ni mbaya….nimekuambia ya kale yapite tugange haya na yajayo, mimi nipo tayari kufanya kila kitu ukitakacho, ili tuwe sote wapenzi kama siku ile tuliyo-oana, unaikumbuka ile fungate yetu, tulikwenda wapi mke wangu…’ baba akamsogelea mama na kumshika kichwa
‘Zanzibar…ooh, Zanzibar…nakumbuka sana, sana…mmh, mume, sijui nianze kukuita mume wangu kwani maneno yako mataaamu siku hizi, hivi huyu mume katoka wapi siku hizi..hahaheee, utafikiri kweli, au kwa vile unajua sitaishi muda mrefu tena, au…sawa, kama usemayo ni kweli ,kama kweli unanipenda, niletee ile chupa ya konyagi…usiponiletea hapa nakuninywisha najua unanichezea shere…na mwanangu nakupenda sana…lakini, lakini, lazima ujue ipo siku hutapata usumbufu wangu tena, utakaa huru, pombe nitaacha, na maisha nita-yaacha, …na baba yako atakuwa huru,…huru, nipe konyagi yangu..hiyo hapo…’ akainuka nakuanza kupepeseka.
Maua akikumbuka hiyo hatua alijikuta hawezi kuzua machozi yake, …akajiuliza kwanini inafikia hatua kama hiyo binadamu hataki kuelewa ukweli kuwa anachofanya ni kutafuta umauti wake mwenyewe…akatikisa kichwa, na kuchukua leso yake kufuta machozi. Lakini ile taswira ya siku ile ilizidi kumuandama, kwani anakumbuka siku ile saana, na ndiyo inyomtesa akilini, kwani hakuwahi kupata muda wa kumuulizia mama yake kuhusu kile kisa cha mtunza bustani kilichoacha kumaliziwa, na kila mara akirudi nyumbanai anakutana na matatizo ya mama yake na baba, hakuna muda wa mongezi.
 Siku ile pale walipokuwa wamekaa, mama yake aliomba apewe hiyo chupa ya konyagi, lakini hakuna aliyemkubalia, …ilikuwa wakati baba anaitaka kuichukua ile chupa na kuitupa kama anavyofanya, lakini alishitukia, mama kainuka na nguvu za ajabu, akiwa hakutegemea kabisa, aliwatoka, na alivyoidaka ile chupa, na kwa haraka akawa kaifungua na walichoona ni  chupa tupu ikidondoka chini ikiwa nyeupe.
‘Sasa ongeeni, sasa nipo shwaari…na mwanangu kapumzike, maaana siku ya leo naiona shwari..baba yako amekuwa akinikataza nisinywe, kajaribu weee, nikamtoroka,…kama nilivyokuwa nafanya siku za nyuma, ananifuga kama mbwa, …nani kakuambia binadamu anafugwa, au huo utajiri wako uliambiwa ili uupate umfuge mkeo kama….basi mwanangu  nikanunua chupa kumi nikazificha, nikawa nazinywa taratiiibu kwa siri…hii ndio ya kumi…ya kumi, …sasa labda niseme na-acha pombe..naacha kabisaa…naacha, siwasumbui tena.
`Mwanangu mpende sana baba yako,…tumetoka naye mbali…tumaishi kama paka na chui lakini ni mke na mume, watu hawajui..hawajui, kwasabau wakijua ni kashifa…kashifa hatakiwi kwenye nyumba hii…kazi hiyo anayofanya, hivi baba nanihii…mume wangu nimesahau, toka sasa wewe ni mume wangu, nakupenda mume wangu, …hivi nilitaka kukuuliza nini vile…ooh, kazi umestaafu au bado…oh mume wangu nakuonea sana huruma, umeteseka sana na mimi, hasa kipindi hiki, nakuomba sana unisamehe..umenisamehe mume wangu …nashukuru kama umenisamehe, ila kiukweli na wewe unatakiwa utubu…kwani wewe sio kwamba ni mtu mwema, hakuna…wewe ni mbaya kama nyoka…
 Baba akamsogelea mke wake , akamwangalia kwa muda halafu michirizi miwili ya machozi ikamtoka, akamsogelea mke wake, akambusu akamwambia `mke wangu mimi nimekusamehe kama ulinikosea, …ndio maana nakushauri acha pombe tuanze maisha upya…nakuoenda sana mke wangu…’ akamwangalia na michirizi miwili ya machozi ikamtoka mzee mzima, na hapa Maua alijkuta nay eye anatokwa na machozi. Akainuka kutaka kuondoka.
‘Mwanangu kampumzike, mimi na baba yako tupo kwenye fungate, usijali nimesemaje, naacha pombe kabisaa…siunataka niache,…sasa wewe soma, soma kwa bidiii, baba yako atafaidi matunda yako, na…usinisahau, kwa vyovyote itakavyokuwa, nakupenda sana mwanangu na naomba unisamahe kwa tabia hii chafu…najua inawakera, lakini sijapenda iwe hivyo…nenda kampumzike mwanangu…’ akamgeukia mumewe, na kumwambia amsindikize mwanae nje yeye anataka kulala..’ basi baba akainuka pale akanishika mkono, tukatoka naye wakati tunapita kizingiti cha malango tukageuka pamoja kumwangalia mama, akatupungia mkono, tukatabasamu, naye akatabasamu, na ule mkono ukadondoka kwa kasi…ki kawaida mtu unaurudisha mkono wako taratibu, lakini haikuwa hivyo kwa mama, ilikuwa kama vile kitu kimedondoka na kugonga pembeni mwa kaitanda, ukafuatia mkoromo, na mara kimya!
 Baba na mwana walikuwa wameduwaa mlangoni, walipoona ile hali wakarudi haraka kitandani, na haraka baba akamshika mkewe kichwani na kukilaza kichwa miguuni mwake, akamtizama mkewe, akamshika shingoni, akamwangalia ..halafu akamshika shingoni tena na mkononi, akamshika kwa muda, huku kaangalia pembeni, bila kumgeukia Maua, akasema
‘Maua kapige simu haraka dakitari aje…haraka sana….’ Ilikuwa ile sauti wanayoiogopa, sauti ya kuamrisha…Maua akiwa akiwa nguvu zimemusihia, miguu yote inemchezacheza akatoka nje haraka badala ya kuingia chumba cha maongezi ambapo ndipo simu ilipo, alipogundua hili akarudi haraka ndani, bila kuwaangalia wazazi wake akapita hadi chumba cha maongezi, alishangaa kwanini baba alikuwa na simu yake ya mkononi, asiitumie, akaamurisha ipigwe simu ya mezani, au kwa vile mara nyingi wanampigia huyo dakiatri wake kwa simu za mezani, …alikuwa akiwaza huku akikimbilia sehemu ilipo ile simu..
 Alipoifikia, huku akitetemeka mikono, akaiinua na kumpigianamba za dakitari za TTCL, , simu ikawa haipatikani, akachukua simu yake na kuanza kupiga namba za simu za mkononi, lakini simu ilikuwa ikisema inatumika…akawa anarukaruka …akakumbuka, akampigia kaka yake, siku ikawa inatumika..akampigia kaka mwingine ikawa vile vile inatumika…akachanganyikiwa, …akairudia ile ya mezani, haipatikani…’ akaamua kurudi pale alipowaacha baba na mama yake, alipofika,…aliona kimya, watu hawapo…alijikuta akidondoka chini!

Ni mimi: emu-three

8 comments :

malkiory said...

Hapa ni nani wa kulaumiwa baba au mama? waswahili walisema majuto ni mjukuu.

Faith S Hilary said...

mmmh, kimempata nini mama! Na kweli...je mama au baba ndio wa kulaumiwa...haya mie nipo M3, siendi popote hehehe!

Anonymous said...

Hii hadithi inanoga sasa, yaani hapo ulipotuchia umetushika pabaya!! Kutwa kuchungulia mublogu kama utaendelea weekend. Nasubiria jumatatu ifike kwa hamu!

Subira

emuthree said...

Natamani nami ningepata nafasi hiyo nikakiendeleza kisa hiki mpaka mwisho kwa kukiendeleza kila siku,lakini ndio hivyo sina jinsi. Tuweni pamoja tu wadau zangu!

Yasinta Ngonyani said...

Inasikitisha, wanawake ni watu wavunilivu sana, wenye kupokea lolote zuri na baya na ni wenye huruma sana. Na pia ni kiumbe ambacho kina hitaji PENZI/PENDO la dhati si MIMALI. Kuna wengine wanafikiri wanawake wanampenda mtu kwa mali au kukiwa na kila kitu ndio PENZI. NA HII HUSABABISHA TATIZO LA MAMA MAUA KIFARIJIO HUWA POMBE AU KUTOKA NJE. KWA VILE MUME HAWI KAMA INAVYOTAKIWA.....

Mama nyengi said...

Ww dada sasa hyo hadithi yako mbona hieleweki imeishiaje,ni sawa na mtu aliye na kichwa ila kakosa miguu.malizia simulizi ili ueleweke au ume copy sehemu.

emu-three said...

Mama Nyegi kwanza nashukuru sana kwa kuwa mpenzi wa blog hii na maoni yako ni muhim sana. Naomba uendelee kusoma hiki kisa kwani wewe ndio upo sehemu ya 5 na kisa hiki kimeshafika sehemu ya 17. Sasa hivi sio kichwa tu bali ni kiwiliwili kasoro miguu ambayo ipo mbioni kuifikia. Mimi sina hiyo tabia ya kukopi visa vya wengine kwani bado nina visa vingi sijapata muda wa kuviweka hewani. Nakuomba tuwe pamoja tu utafurahi mwenyewe.Ahsante kwa maoni yako

Anonymous said...

You are so awesome! I don't suppose I have read through anything like
that before. So nice to discover another person with some unique thoughts on this topic.

Really.. thank you for starting this up. This site is one thing that's needed on the internet, someone with a bit of originality!