Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, April 11, 2011

Dawa ya moto ni moto-1  Alichukua simu yake ndogo, akapachika waya halafu akaunganisha na computa yake ndogo, akabonyeza sehemu na picha zikaanza kuonekana, alitizama kwa muda halafu akachukua santuri ndogo za kunakili na kuanza kunakili kile kinachoonekana kwenye computa ndogo, alipomaliza santuri , akachukua nyingine, na nyingine, halafu akachukua santuri, na mbili akaziweka kwenye kabati ambalo alilifunga na funguo,
  
Alichukua simu yake akatafuta mtandao wa yahoo, akatuma zile picha ambazo zipo kwa mtindo wa video kwenye barua pepe yake. …wakati anaendelea hivi, akahisi nywele zikimcheza, hii ni moja ya dalili kuwa kuna kitu kisicho cha kawaida, akahisi kuna mtu anamchungulia …akatizama huku na kule huku akitega masikio, lakini hakusikia kitu , ila hisia zilimuelezea kuwa kuna mtu au kitu kisicho cha kawaida. Akazima komputa yake na akachukua ile simu, aliyopewa na rafiki yake na kabla hajafanya kitu akazima taa.

Alipowasha taa akahisi hayupo peke yake ndani ya chumba, aliwaza huyo aliyeingia ni nanii na aliingiaje, wakati chumba chake alikifunga, akaogopa kugeuka haraka, akijua kama ni adui atajua kuwa kagundulika na anaweza akachukua hatua haraka ya kumwangamiza kabla hajajiandaa, kwahiyo akajifanya kama vile hajui kuwa kuna mtu. Mwili ulianza kumzizima kwa woga, akahisi kuwa huyo mtu aliyepo nyuma yake ana nia mbaya, …
Akahesabu moja mbili tatu..akaina chini kidogo halafu akageuka…alipata mshituko ambao hajawahi kuuona katika maisha yake, alibakia mdomo wazi, akataka kupiga yowe lakini sauti haikutoka kabisa, na kabla hajafanya kitu, kisu kilichotupwa kwa ustadi kilimchanya pembeni mwa shingo na kwenda kuzama ukutani mwa chumba.

‘Hilo ni onyo, mshikaji, kuwa hatutaki mzaha, unamuona mwenzako alivyo, hapa anahesabau masaa kabla hajakutana na mtoa roho, na wewe ukileta ubishi na kutoshirikiana na sisi ni swala la sekunde chache utaiona dunia nyingine, kwetu hakuna shida, …siunajua tena tunachojali ni pesa…’ ilikuwa sauti nyuma ya mwili unaovuja damu, sura ya mtu ilikuwa imebadilika kabisa, sura ya mtu aliyekuwa naye jana, leo siye yule mtu tena, macho yalishanza kuonyesha weupe, labda ni kwasababau ya kuvuja damu nyingi.

‘Usiwaambie lolo…te, acha nifa, nimeshakufa…na wewe hata ukiwaambia, wata-ku-ua tu…’ kabla hajamaliza maneno kisu kilipita shingoni, na kusambaza damu chumba kizima, kilichofuta ni mkoromo….
 Jicho lilimtoka jamaa, akajua kweli hawa watu hawana mchezo, kweli mwenzake ndio huyo kaaga dunia, inayofuata ni zamu yake, kwa macho ya kujificha akachungulia dirisha, akaona kuwa ule upenyo na utaalamu wake wa sarakasi atapenya tu, na hiyo ndio njia pekee.

‘Ukileta ujanja utatangulia mapema, mkakutane na huyu kikaragosi wako, sasa amepata faida gani, hebu jiulize na wewe amefanya nini na kapata faida gani,…zamu yako, wapi ile kamera mliyochukulia zile picha za video, na wapi picha za video, ….hatutaki kupoza muda, wewe kifo chako bado, sema ukitupa jibu muafaka , basi huenda bosi akaridhika uka…’ kabla hajamaliza nilikwisha hesabu moja mbili tatu, kama mshale niliruka, na kichwa kilitangulia mbele nikapenya kwenye dirisha na kutua nje, na kabla sijatua vizuri, nilijizungusha hewa, kuhakikisha kama kuna kisu kimetupwa kisinipate, nikatua kwenye majani , na kabla sijatulia nikaruka juu na kutua juu ya ukuta unaozunguka nyumba na kupaa hewani, nikijua sasa ama kufa kwa  kisu au bastola au kufa kwa kugongwa na gari au kudondokea kichwa kwenye lami…..
                 ******************
` Kwani ilikuwaje kabla hujafika huko, kwanza siku ile ulihadithia kuwa umeamua kumuoa yule mtoto wa tajiri, licha ya kukuonya kote kuwa yule sio maharimu wako, yule anakupenda tu kwasababu, lakini akibadili mawazo atakuchukia kama kinyesi….ukaamua kumuoa, sasa visa vinakuandama, sijui lini utakutana na makucha yake, sisi hatupo, maana pale ni maji marefu, ilikuwaje, na umaechukua uamuzi gani hadi sasa…’ akaulizwa jamaa
‘Najua wengi mtashangaa kwa hatua niliyochukua, lakini ilibidi iwe hivyo, kwani wahenga walisema dawa ya moto ni moto,…’ ilikuwa sauti ya jamaa akimuhadithia rafiki yake, nami niliposikia usemi huo wa `dawa ya moto ni moto’, nikavutika kusikia nini kiliajiri.
Nikawasalimia kwanza hawa jamaa wawili halafu nikaagiza juice  nakukaa pembeni huku masikio na akili zikiwa zinafuatilia mazungumzo hayo…nilikuwa tuli!

 ‘Mimi nilimpenda sana mke wangu, wengi walifikiri kuwa nilimpenda kwasababu ya hali yake ya  kipato, na wengine walidiriki kusema nilimpenda kwasababu ya kupata hifadhi kwasababu sikuwa na mbele wala nyuma. Yote ni sawa na huwezi kuzizuia hizo hisia, na midomo ya watu na kwasababu moja ya kazi ya hisia za wanadamu ni kuhisi vyovyote iwavyo na kazi ya midomo ni kuongea.

‘Huyu mwanamke nilianzana naye urafiki wakati tupo shuleni, kiumri tumepishana  naye kwa mwaka mmoja tu, na tulipata bahati ya kusoma shule ya msingi pamoja na hata sekondari ya awali hadi kidato cha nne, mimi nikakwama kwasababu ya hali ngumu, mwenzangu wazazi wake wakamuendeleza hadi chuo kikuu. Na kipndi chote hicho akiwa kidato cha tano na cha sita hata chuo kikuu tulikuwa tukiwasiliana na akirudi likizo tunakutana na kujuana hali, kama marafiki na naweza kusema kama wapenzi!

‘Alipomaliza chuo kikuu akapata kazi nzuri, mimi nami wakati huo nilikuwa nafanya bisahara ndogondogo tu, na sikuweza kufika mbali, kwani leo unainuka kesho huna kitu. Nikawa mtu wa vijiwe, nipate nisipate siku zinakwenda. Basi kwa hali kama hii , sikuwa na mategemo kabisa ya kumpata Maua kama mke wangu. Utawezaje kumuoa msomi, mweny kazi ya maana, na…lakini hutaamini, yeye alikuwa haishi kunikumbuka, kwa simu na hata wakati mwingine ananitembelea.

‘Na kila tukikutana naye, nilikuwa nasononeka sana, na wakati mwingine nilitamani asiwe ananitembelea,kwani,nilikuwa naumia sana roho, kwani ni msichana ninayempenda sana na alijaliwa sura nzuri…na hayo niliyotaja awali! Kwahiyo moyoni nilikuwa nasononeka , wivu ulikuwa umanijaa na ilifikia hatua najuta…nilikuwa najutia maisha yetu, maisha ya familia yangu iliyonilea, kwanini mimi nilizaliwa katika familia ya kimasikini, nilitamani sana kusoma, lakini kwa jinsi gani.

 Nilikuwa nasononeka sana nikiwaona wenzangu waliojaliwa kusoma au kusomeshwa na wazazi wakirudi likizo ,  na sikupenda kuonana nao, lakini haikuwa rahisi kwani walikuwa majirani zangu. Na siku zilivyozdi kwenda mbele, bila kupata nafasi hiyo ya kusoma ndivyo nilivyokata tamaa kabisa ya kusoma , nikajipa moyo kuwa kusoma sio kila kitu lazima nihangaike kivingine, na moja ya malengo yangu yakawa kuhangaika kibiashara hadi nitakapoweza kuwa mfanyabishara mkubwa,lakini kila hatua ilikuwa kama kujaza pipa kwa kijiko…nikawa naota ndoto kubwa zisizo na mafanikiwa,  ilikuwa kama zile ndoto za Alinacha. Kila biashara niliyobuni, nilishia kupata hasara na hata mtaji kwenda arijojo,  na mwisho wa siku ninabakia mikono mitupu.
‘Basi katika kutapatapa, huku na kule nikawa nakutana na marafiki zangu wa kibiashara, na wao wananihadithia habari za jiji la Dar-es-salaam, mwisho wa siku nikaamua kuzamia ndani ya jiji hilo. Ili kufanikiwa hili, nikapatana na jamaa mmoja ambaye aliniambia atanisaidia , nitafute nauli na hela kidogo, nikifika huko atanipa njia na mbinu za kuishi ndani ya jiji hilo. Kweli ikawa hivyo, nikawaaga wazazi wangu, na siku moja nikadamkia basi liendalo Dar-es-salaam.

 Nilipofika kwa mara kwanza nikawa naishi kwa jamaa yangu huyo aliyenishawishi kuja kwenye jiji hili, yeye alikuwa na chumba kimoja, basi tukawa tunachangia hicho chumba.Muda wetu wa kukutana na jamaa yangu huyu ni usiku, mimi nahangaika kivyangu na yeye kivyake, kwani alishanionyesha jinsi gani ya kutafuta, kwahiyo haikuwa na haja ya kuongozana naye kwenye mihangaiko yake, tukawa tunakutana wakati wa kulala, na hapo tunapeana stori za mishemishe, kama nimekwama au mwenzangu kakwama, tunainuana kimtindo.

 Siku moja muda wa mchana nikarudi kwenye chumba chetu tulichokuwa tukiishi, nikiwa nimechoka sana, kwani nusura nisweke ndani, kwa kukutwa nikiuza maeneo yaliyopigwa marufuku…nilikuwa na biashara za mikononi, nguo chache na vitu vingine, unachofanya nikutafuta wateja, na kuhama hapa na pale…mara nikaingia maeneo ya watu, wakati naongea na mteja, mara mgambo hawa wakatokea…ilibidi nikimbie na kuacha nguo zangu na baadhi ya vitu. Mimi kwa kukimbia ni mwepesi sana, kwani nilipitia mazoezi ya mbio na sarakasi. Nilipowapotea, nikaiona siku hiyo imeingia mkosi, nikawa sina jinsi, ila kuirudia nyumbani na kutafakari jinsi nyingine, nikajikuta nimepitiwa na usingizi.

Nikasikia mlango unagongwa, nikainuka kuangalia ni nani,mawazo yangu  nilizania na hawo mgambo wamekuja kunikamata, nikatamani niingine mvunguni, lakini nikaona haitasaidia kitu, nikafungua mlango kimachale, kwa kama ni wao nitachomoka na kupotelea mitaani …

‘Nimemkuta Michizi…’ ilikuwa sauti ya msichana mdogomdogo
‘Michizi hayupo …kwani unamtakia nini…?’ nikamuuliza yule msichana, alionekna bado mwanafunzi ingawaje hakuvaa nguo za shule.

‘Kama hayupo mimi siondoki hapa, …mimi..sijui nitafanya nini,…wazazi wangu wamenifukuza, na sina pa kwenda, na sijui kama wameelekea polisi au vipi …’ akawa yule msichana analia, na kuniacha nisijue la kufanya.

‘Kwani imekuwaje wewe msichana, mbona unakuja hapa na kuanza kunililia, unafikiri watu watanielewaje, watu watanifikiria vibaya…’ nikajitetea, huku naangalia huku na kule, nikaona nimkaribishe ndani, ili kutowavuta watu, kwani watu wa Dar hawana dogo.

 Na mara rafiki yangu akaja, haikuwa kawaida yake, nikajua alikuwa anafahamu ujio wa huyu msichana, nikatoka nje niwape nafasi ya kuongea. Maongezi yao yalikuwa hayana maafikiano mazuri, kwani baadaye rafiki yangua akaniita pembeni na kuaniambia nini kianendelea,

‘Nimelikoroga rafiki yangu, huyu binti ni mtoto wa shule, nilimjaribu kidogo akaelekea, mara tukaanza mapenzi, sikutegemea kuwa itakuwa hivi, sijui hata demu wangu wa siku nyingi akigundua itakuwaje, lakini sina jinsi, sasa …unajua tena, nimemjaza mimba, na wazazi wake wamesema ili nisifikishwe polisi nimchukue, nifungishwe ndoa ya mkeka…yaani hapa nimechanganyikiwa, unaona hali ilivyo, chumba ndio hiki kimoja na hali yenyewe ndio hii, sasa sina jinsi…kumbuka binti ni mwanafuzi wa darasa la saba kafukuzwa kwao, sasa ili nilitatue hili, haina jinsi …wewe sasa rafiki yangu ni mwanaume utafute sehemu nyingine ya kujishikiza…’ akasema rafiki yangu.

Tukashauriana mwishowe nikakubali, hata kama nisingekubali tungeishije humo ndani, chumba kimoja, hakuna jinsi ikabidi jamaa Abakie na huyo msichana waishi naye. Mimi ikabidi nitafute sehemu yoyote ya kuishi, … nikawa kama kuku mgeni…niliwaza sana nikaishi wapi, wapi nitapata chumba, mwisho wa siku nikaoana niwe nafanya kazi Kariakoo ya kubeba mizigo, ikifika usiku natafua maboksi unajibanza mahali hadi asubuhi, unadamkia kubeba mizigo, ukipata mabaki ya vilivyodondoka, unapanga pembeni hapa na pape unaongezea visjisenti siku zinakwenda.

 Siku moja nilikuwa naosha gari moja la wafanya biashara,  kwani sikuwa nafanya kazi moja, wakati mwingine nauza vitu nilivyopata shimoni Kariakoo, wakati mwingine nasafisha magari….basi siku moja nilikuwa nasafisha magari ya watu mbali mbali , na mara gari moja lenye rangi nyekundu likasimama pale nilipo, nikiwa na brashi langu mkononi, huku nikiomba mungu, awe mteja….! Kwani wakati mwingine anaweza akaja mtu kukukoga tu, na ukimfanyia kazi yake anaondosha gari …watu wengine bwana, haya ….

 Mara wakati nawaza haya na kumuomba mola  akatokea mrembo ndani ya lile gari  jekundu, nikasema leo naweza nikapata bingo. Kwasababu ya uzoefu wa kazi hizi, unapata hela nzuri akiwa ni mwanamama, tofauti na akina baba, wao ni mawili ufanya kazi ya kujitolea na kuambulia matuzi au upewe hela yenye masimango, …lakini hapo, nikaanza kumeza mate, kuwa leo nitapata kinywaji bariidi, na nyama choma, siunajau tena watu kama sisi ukipata kidogo unajipongeza kama tajiri ….Hilooo…bingo hilo, linakuja kwani yule mrembo akawa ananisogelea hadi niliposimama, halafu akavua miwani.

‘Ile brashi ilinidondoka mkononi…., sikuamini macho yangu, hebu jaribu kufikiria , wewe umeamua kuzisaka pesa, ili uje umuonyeshe umpendaye kuwa unazo, ili akukubali, nan i msichana unayempenda sana, na usingependa kabisa ajue kuwa maisha yako yako hivyo, na ukumbuke kuwa ni msichana ambaye huishi kumfikiria na unahangaika ukiomba Mungu, kuwa ipo siku utapata na utaweza kumtafuta na kumuomba awe mke wako, na mara anatokea usoni mwako na hali kama ile…nipo nyapinyapi… sitamaniki …midwabadwa, viraka hadi chupi inaonekana…nikagwaya!

Jamani hapo ndio mwanzo wa kisa chetu kipya, niendelee au nisiendelee...?., maana kimiya kingi kina mshindo,wapenzi wa blog hii siwaoni, mpo ? sijui kuwa mpo maana kimyaa…sawa, ...lakini sikati tamaa, hapo ndio nakianza kile kisa chetu kipya kama nilivyo-ahidi. TUWEPO

Ni mimi: emu-three
Enhanced by Zemanta

12 comments :

Anonymous said...

Yaani mbona unataka kututoa roho! eti wasema usiendelee? Wacha mzaha, kwana kila siku lazima nichungulie kuona kuna nini. Leo nimefurahi kukuta hiki kisa.

Swahili na Waswahili said...

Ubarikiwe ndugu!!!!!!!Nakuaminia sana tuu na Mungu akubariki katika yote!!!!

Nancy M said...

Mmmh mbona unaturusha roho? Kwa sauti kubwa ENDELEA!!!! Usione kimya wapenzi wa blog yako tuko pamoja nawe. All the best!!

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Hii naahidi kuifuatilia tangu mwanzo hadi mwisho. Tuwemo!

Anonymous said...

endelea mkuu tuko pamoja hii kitu nikali sana inaoneka itaendelea kuwa nzuri zaidi hangera sana na ubarikiwe kwakutuletea stori nzuri nzuri

Candy1 said...

Haya ndio mambo sasa! M3 mbona sie tupo....wewe tu! Hahaha endeleaaaaaaa!!! Mi nipo kama kawa

Anonymous said...

Umeongeza idadi ya wapenzi wa blog yako rafiki - mimi (am not sure if you're he or she) unakipaji kizuri sana. Haipiti siku nisiingie humu japo mara tatu ama ndo nikuache hewani siku nzima kazi yangu kurefresh tu kuona umeleta nini kipya. Keep it up - stay blessed!

Yasinta Ngonyani said...

Eti kama tupo hili ni swali au? we andika/weka wasomaji/wafuatiliaji tupo ukiona kimya wala usiwe na wasiwasi. Tupo Pamoja....nimeupenda mwanzo wa kisa ni kama kawa unaogopesha na kusisimua.....ENDELEA, ENDELEA ENDELEA......

Pamela said...

hii ni love story nahic itakuwa taaaaaaaaaam japo kuna ya kutisha pia mana kuna visu na ujuzi wa kukwepa kwa karate sarakac keep it up kazi nzuri wengine wanapita kimya kimya kaka ucdhani hawapo!!!

John Maembe. said...

Tupo Emu-3.
Endelea kutupa Burudani bhana, maana hicho kisa kizuri sana na kinanikumbusha Stori ya rafiki yangu mmoja hv naomba ukiendelezeee eti.

Kila la kheri katika kzi yako.

samira said...

mwanzo mzuri m3 sasa sichezi mbali na wewe

SIMON KITURURU said...

Mie niko tokea mwanzo Mkuu!