Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, September 7, 2016

Wakati ukuta...


 Wakati napita barabarani, kwenye vimtaa vinavyoingia kwenye ofisi mbalimbali, nikavutiwa na bustani zilizopembezoni mwa barabara hizo, ambazo zimetengenezwa na wenye maofisi hayo. Macho yangu yalivutiwa na ua-waridi, lilikuwa ndio kwanza linaanza kufunuka na ule uzuri wake ulikuwa ukianza kuonekana, nikatabasamu na moyoni nikasema, ama kweli ua waridi ni mrembo wa maua. Basi ikawa kila nikipita hapo nalichungulia lile ua, mpaka likachanua vyema na kudhihiri ule uzuri wake, wa kuitwa ua waridi, na wengi walikuwa wakilitupia jicho, kwa tamaa za kulichuma.


Nilikaa siku kadhaa bila kupita njia hiyo, kwasababu mbalimbali na jana nikaona nipitie hapo, nikakumbuka lile ua waridi, nikalichungulia kwa hamasa nikaongeza mwendo ili nifike maeneo yale. Nilipofika hapo nilitamani kulia, kwani lile ua-waridi lilikuwa limeanza kunyauka, na yale mabawa yake ya pembeni , yanayoliremba kwa rangi yalikwa yamelegea karibu kudondoka chini. Nikalisogelea na kujaribu kuyainua yale maua yake ili yakae vyema, lakini haikuwezekana, kwa yakini lilikuwa limeisha muda wake, na mbegu zake zilidhihiri, nikatabasamu na kusema angalau mbegu hizo zitadondoka na kuzalisha miti ya maua waridi mengine mengi.

Wakati nahangaika na lile ua mara likapita gari la mwanadada mmoja, kwa umri wake sasa huwezi kumuita mwanadada, ingawaje hajabahatika kupata mtoto, na kama angebahatika kupata mtoto na mtoto wa kike labda angelikuwa na wajukuu! Nikamtizama akipita na hilo gari huku kumbukumbu za akili zangu zikinipeleka enzi hizo ambapo nilikuwa bado nasoma, na huyu mwanadada alikuwa keshaanza kazi, na sie kama wanafunzi wa sekondari damu moto, tukawa tukimuona tunatamani kuongea nayeye. Na yeye alikuwa mkali sana, akituasa kuwa tusome tusiwe na tamaa na watu wakubwa. `Naombeni mniheshimu mimi ni dada yenu..’ alikuwa akisema hivyo!

Dada huyu namkumbuka sana, kwani tulipokuwa wanafunzi, wengi tulikuwa tukimuona akipita na magari ya matajiri, na kila mmoja wetu alitamani ampate mrembo kama yule. Ni kweli alikuwa mrembo, na kama angeliamua kugombea huo urembo wa dunia, angelikuwa miongoni mwa washindi. Lakini siku moja tulimsikia akisema, `nigombee urembo ili iweje, mwenyewe najiamini kuwa mrembo, halafu nitafute watu wanilinganishe na wengine…na kama ni pesa ninazo za kutosha kwanini nihangaike…

’Kweli mungu alimjalia, toka sura hadi maumbile ya mwili, ila kasoro tu tabia ilikuwa haiwafurahishi wengi. Labda ni kutokana na urembo wake ndio maana aliringa sana, na hata kuwadharau wenzake na hasa wale wa hali ya chini. …labda!

‘Mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama..’ huu ulikuwa mmoja wa msemo wake, pale alipokuwa akigombewa na matajiri mbalimbali, kila mmoja akitaka kummiliki yeye na hata kumtaka awe mpenzi wake. Lakini kwa kunata kwake , alihakikisha anawatoa majaso hawa wanaume na mwisho wa siku midume yenye uroho waliambulia kutoa zawadi kibao na bado akawa hataki kumilikiwa na yoyote katii yao..., kama mpenzi wa kudumu.

‘Mimi sitaki rafiki wa kudumu, kwani sijafikia umri wa kuolewa, kwahiyo anayetaka urafiki na mimi, ajiandae kwa `part- time’ tu..’ aliwaambia hawo wanaume waliokuwa wakijigonga gonga kwake. Na kweli ungelimkuta muda wa chakula cha machana utakuta yupo na mwanaume huyu, chakula cha usiku mwanaume huyu, hatujui kama usiku alikuwa na rafiki mwingine, lakini yeye alisema waziwazi kuwa urafiki na waume hawo mwisho wake ni geti la nyumba kwao, hana mpenzi wa kuchezea mwili wake!

Ni heri kwake kama msimamo huo ulikuwa wa kweli, na watu wakamsifia kuwa kama ana msimamo huo wa kuwa `hataki watu wa kuchezea mwili wake’ basi atakuwa na mawazo ya maana sana. Lakini tukasikia kipindi fulani kuwa kapachikwa mimba, na mtu aliyempachika mimba ni njemba fulani, na njemba huyo ni wale ambao sura hazina mvuto.

 Kilichotokea ni kuwa njemba huyo kwa vile alikuwa na pesa aliamua kumtoa huyo dada kwa chakula cha usiku na kumbe ulikuwa mpango rasimi wa kumkomoa huyo mwana dada, kwenye kinywaji akawa kaweka dawa ya kulevya, na dada alipoishiwa nguvu, akachaguliwa bega!

Katika skendo hiyo , huyo dada ndipo alipobebea mimba,na kitendo hiki kilimsononesha sana huyu mwanadada, kwani alisema hataki azae mapema, na hata akizaa hataki kuzaa watoto wenye sura mbaya, alitamani sana kuzaa watoto wenye sura za kizungu-kizungu , …alipenda sana wazungu na ndoto yake ilikuwa kuolewa na mzungu. Alipogundua kuwa kapachikwa mimba na huyu jamaa, ilikuwa imeshapita miezi miwili. Mwenyewe alidaii kuwa siku zake zinaweza kuchelewa hata miezi miwili, lakini kutokana na mabadiliko fulani mwilini alijihisi kuwa ana mimba, akaenda kupimwa na kukutwa kweli ana ujauzito.

Kwa hakika alijua kuwa nani kampachika hiyo mimba, ila sisi wa mitaani tukawa tunajiuliza itakuwa mimba ya tajiri gani, au mzungu gani kama mwenyewe alivyotaka, na kwanini mimba hiyo ikaja mapema. Penye wengi hapafichiki kitu, licha ya kuwa yeye mwenyewe alifanya siri, lakini uvumi ulienea mitaani na kila mtu akajua. Swali lilikuwa ni uja-uzito wa nani,…!

‘Siwezi kuzaa mtoto mwenye sura mbaya kama njemba ile, lazima nikaitoe hiyo mimba…’ akasema na yule njemba aliposikia hivyo, akajitahidi kumbembeleza huyo mwanadada asiitoe kwani yupo tayari kumuoa, lakini huyu mwanadada aksema wazi kama ni lazima kuolewa na mtu kama yeye, labda aoe mwili wake ukiwa mfu! …kufuru!

Basi mwanadada huyo akafanya mpango akakutana na mtaalamu wa kuporochoa viumbe vya watu visivyokuwa na hatia. Na mungu kwa uwezo wake akataka kumpa mitihani huyo mwanadada, kwani wakati anaitoa hiyo mimba kukatokea matatizo, ambayo yalipelekea mwanadada huyo kupata matatizo ya ndani kwa ndani. Mimba ilikuwa haikutoka vyema, ikawa imeleta mdhara ndani ya kizazi. Na matokeo yake ikahitajika dada huyoo kufanyiwa upasuaji na kusafisha kizazi, na kilichotokea ni kuharibika kabisa kwa kizazi chake,…!

‘Eti nini ina maana sitazaa tena?’ akamuuliza docta

‘Nasikitika sana ndio hivyo, kwani ulivyotoa hiyo mimba imeleta athari kubwa sana kwenye nyumba ya uzazi , na bahati yako ndiyo hiyo kuwa kizazi kimesafishwa vyema na kuondoa balaa ambalo lingekugharimu maisha yako…’ akamwambia docta

‘Sawa, hata hivyo watoto wa nini…’ akajisema huyo dada na kuondoka zake

Miaka ikaenda na umri wa yule dada ukawa umesogea, akabahatika kuolewa na mwanaume mmoja, lakini hawakudumu naye, wakaachana, …haikuchukua muda akaolewa tena, ikawa ndio hivyo akiolewa anakaa na mume mwaka au miaka mwili anaachika, kwasababu ya tabia yake ya kutaka anasa au kugundulika kuwa hazai. Na hili likamfikisha hapo alipo, umri umekwenda mbele sasa hana mume wala mtoto.

Umri haujifichi katika maisha ni kama kifo, ambacho hakikwepeki, umri hauna dawa kama kama kilivyo kifo, ufanye ufanyalo umri huwa unasogea mbele, na maumbile ya kibinadamu hubadilika siku zinavyokwenda. Uzuri wa ujanani haudumu, una muda wake, na sura ile ya mvuto hubadilika na kuwa sura ya makunjazi,…sura ya utu uzima na hapo tena inabakia kusimulia, `enzi zangu bwana…’

Dada yetu huyu ambaye yupo kwenye umri wa akina mama ambao walitakiwa kuwa na wajukuu, hadi leo hana mume wala mtoto, na uzuri ule aliokuwa akiringia nao umetoweka, sio `mrembo tena wa kimataifa’ bali `ni aliyekuwa ..’ .

Huyu mwanadada alisahau kabisa kuwa wakati ni ukuta, huwezi kushindana nao, ukishindana nao utaumia mwenyewe. Kwani kwa bahati mbaya hana kizazi ambacho kingeendeleza ule uzuri wake. Ni heri ya lile ua waridi ambalo kesho au kesho kutwa litadondosha mbegu na kuendeleza kizazi chake. Si sawa na huyu mwanadada, au mwanamama. Ambaye sasa anatamani hata mume asiye na pesa lakini hampati! Bahati mbaya hiyo!

Haya ndiyo maisha yetu, tunapokuwa katika `chati’ tukawa maarufu tunasahau kuwa kuna kitu muda, na muda huendana na `umri’ umri katu hautongoji, muda ukienda na umri unakwenda na maisha ya mtu yanapungua, na sura halikadhalika inasawajika. Ni dhahiri kuwa, umri unakwenda na wakati na mabadiliko ya wakati huwezi kuyaona mara moja, …labda joto, baridi nk,…ila siku zinavyokwenda mabadiliko ya kimaumbile yatajionesha waziwazi. Ulikuwa ukiitwa mtoto, ukaitwa msichana au mvulana, baadaye dada, mrembo, kaka mtanashaji na sasa mama au baba, na hatimaye bibi au babu…hiyo ndiyo hali halisi.

Upende usipende utazeeka, kwani hakuna dawa ya kuondoa uzee, msijidanganye kwa kujichubua…eti ule umri wa ujanani utarudi…tusijidanganye kabisa .Cha muhimu ni kuwekeza, kiafya, kimaadili, kiuchumi kwa manufaa ya baadaye .

Muhimu wenzangu, tujenge tabia ya kuwekeza kwenye wema, ambao hata uzee ukija utakuwa unakulinda. Wapo waliozeeka, lakini kila mtu anatamani awe naye kama mume wake au mke wake, kwasabau ya tabia njema afya yake nk….Tabia njema, nidhamu , na uadilifu hujenga mwili kuwa `imara’ wakati wote. Hata ukifa jina lako halitasahaulika kwenye kumbukumbu za watu wema.7 comments :

Anonymous said...

Kama kuna kitu kinanivutia sana kuipitia blog yako ni hii jinsi unavyoandika tukio kwa mifano halisi...Hii hata Yesu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake kwa mifano. Hii ni hekima kubwa sana uliyo nayo mzee...sijui nikuite namna gani, kwasababu sijui umri wako, au ujinsia wako. Ila ngoja nitumie neno mkuu
Hongera sana mkuu, usivunjike moyo, kuwa watu hawatoi comments,unajua kwanini, watu hawapendi kusoma, na hili ni tatizo kubwa, kama wangelisoma vitu vyako kiundani wangejifunza mengi na wasingebaduka kwenye blog yako kila siku. Profesa Mbele amesema haya sana, kuwa tatizo la watu `HAWAPENDI KUSOMA'...Waambie maandamano, majungu, vijiwe, kuoengea sana, bila hoja za kisayansi...tutafika kweli hivi!
Shukurani mkuu

SIMON KITURURU said...

Bonge la shule MKUU!Limeniwazisha sana!

Anonymous said...

Hii nimeipenda, ungeweka na katuni iliyotoka sijui kwenye blogu gani hapo juu inayomuonyesha Dr kawapanga foleni wasichana ya kuwatoa mimba. Jamani sasa hivi hali inatisha kwa kweli watu wanaendekeza ujana!

John Maembe said...

Aisee hiyo ndo Elimu ambayo wa2 wanaifind lkn haiwaipati,
Mimi ni mara yangu ya 1 kusoma blog yako na I like It the ki2 ninachokipenda is how u express the storie indeed.

Big Up & God make u still survive.

John Maembe.
Bagamoyo.

Anonymous said...

Kwa kweli nimeipenda hii , ni kumbusho safi sana. Tunashukuru MKUU.
Na hii ya kugoma kwa daladala, najiuliza nani `wanamkomoa?' Wanaoumia sio serikali ni wananchi, je hawana njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuendelea kuwabebesha wananchi mzigo, kwanini wasigome kulipa leseni nk?
Jamani mwataka tufe!
Umeme shida, gharama juu, vyakula gharama juu, usafiri shida na gharama juu, bado mwataka iwe juu zaidi...masikini, masikini, masikini, tutakwenda wapi!

Swahili na Waswahili said...

mmmhh ni habari ya kufundisha sana!kweli ujana ni maji ya moto!Asante sana.

Candy1 said...

Ndivyo binadamu tulivyoumbwa, wengine tu wanasahau kwamba kuna miaka kibao inayokuja na kufikiria ya leo tu. Nimeipenda kweli hii...na waridi kaka, jingine litaota :)...na hizo nauli ndio mmmh...labda watu watafanya mazoezi ya kutembea safari fupi fupi ila naona inakuwa too much sasa.