Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, March 9, 2011

Siku ya akina mama duniani


Jana niliamua kuwafungulia mifugo yangu ambao mara nyingi naifungia ndani ya banda, kwa kuchelea wizi na uharibifu kwenye majumba ya watu. Ilibidi iwe hivyo, la sivyo ingekuwa kero kwa watu na hata kupoteza baadhi ya mifugo. Lakini mifugo hii iliona ni kero…kwani kila kiumbe kina uhuru wake, kuku wakawa wanaruka madirishani, na hata bata, kwahiyo inabidi wakati mwingine nifanye kazi ya ziada, ya kusiriba kila mahala. Ilikuwa kama jela ya mifugo, na kwa ujumla hawakuwa na raha kabisa, na nilijua hivyo, lakini kipi bora, niwaachie wakalete uharibifu kwa watu na hata kuuwawa, au niwafungie ndani na kutaabika kama wafungwa.


Basi nikaona ngoja leo niwafungulie angalau wapate hewa. Ilikuwa kizaa, zaa, maana ile hatua ya kutoka mlangoni, ilikuwa kupandana na wengine kuruka juu, na kwa vile walikuwa wengi, na mlango ni mdogo, ikabidi wagande pale mlangoni, wakisukumana, kila mmoja akitaka atoke kwanza, mpaka nilipoamua kuwasukumiza nje, na hapo wengine walitoka huku wanachechemea. Lakini hata hivyo walipoonja hewa ya nje na kujiona wapo huru, hawakujali kuwa wameumia,na kama ilivyo hulka ya ndege, wengine waliamua kutumia mabawa na kuruka,ili wasijitonyeshe miguu yao ambayo iliumia wakati wa kutoka.

Hakuna kitu cha raha kama uhuru. Uhuru huo sio kwa binadamu tu hata ndege au wanayama wanauhitaji sana.

Basi wale kuku na mabata wakaanza kukimbia huku na kule, wengine wakavamia vyakula vilivyoanikwa , wengine wakaingia mashamba ya watu, wengine, wakaenda hata sehemu za hatari , bila kujali kuwa wataangamia. Ilikuwa nusu saa, … nikaamua ni heri niwarudishe ndani,…ilikuwa ni kazi kubwa kuwapata, kwani walishaonja neema ya uhuru, hawakamatiki tena. Ikabidi nisalimu amri na kusema, nitawapata jioni , mkirudi kulala, sitawafungulia tena.

Wakati nahangaika na hawa mifugo, nikakumbuka kuwa siku hiyo ilikuwa siku ya akina mama duniani. Niliwaza mbali sana, nikajisemea moyoni `kama wanyama wengine kama vile ndege na viumbe wengine wanahitaji uhuru, wanahitaji amani , wanahitaji nafasi yao ambayo watajitanua wawezavyo, mbona kuna binadamu wengine hawana uhuru, kama wengine, wapo ndani ya kifungo , kwenye jela iliyoandikwa kwa nje, `UJINGA,’, nyingine, imeandikwa `UMASIKINI’ , nyingine imeandikwa `MARADHI’. Nikakuna kichwa, …

Nilikuna kichwa nikimkumbuka mama yangu enzi za utoto wangu , jinsi alivyokuwa akihangaika, kulima, kuchota maji, kutafuta kuni, kuvuta majani kwa ajili ya kuwalisha ng’ombe ambao hufungiwa ndani masaa yote, na kazi yao ni kulishwa na kusafishiwa mahali pa kulala.Na ikitokea siku ngombe huyo kachomoka hapo anapolala, inakuwa kizaa-zaa, kwanini, kwasababu hata yeye anahitaji uhuru,nafasi na amani. Lakini mama yangu na akina mama wengi vijijini hawana uhuru huo, wamezungushiwa ukuta mnene, ndani ya jela iliyoandikwa `UMASIKINI’ NA KUTA NYINGINE, MARADHI, NYINGINE…

Mama yangu alikuwa naye ni miungoni mwa wafungwa katika jela hizo, kwani majukumu ya kuilea familia , mifugo, shamba nk hayakumpa nafasi ya kupumzika hata kidogo, toka alifajiri hadi usiku na akipata mwanya wa kuweka ubavu, bado anakumbana na shida ya mbu, au shida ya baridi, au shida za watoto wake wakimsumbua , huyu anaumwa hiki huyu anataka kile, …kwasababu jela zote kasukumiwa mwanamke…kwahiyo mpaka kunapambazuka utakuta mama huyo kalalla sehemu ndogo tu ya usiku, na jogoo likiwika haamini jinzi gani usiku ulivyokuwa mfupi, na hapo hana la kusubiri, anatakiwa kuamuka kwenda kuwatafutia ng’ombe majani, anatakiwa kwenda kuteka maji kisimani, ili aoshe vyombe na awapikie watoto chochote kama kipo, kama hakipo anatafuta njia ya kuwaliwaza watoto ili angalau akabangaize mahali watoto wasitiri njaa. Je huu sio utumwa, huu sio ufungwa…

Wakati akina mama wanasherehekea siku yao ya akina mama , niliwaza sana, hivi kweli akina mama kijijini wanaielewa hii siku, au ndio huku mjini tu. Nilimpigia mama mkwe wangu simu na kumtakia kila-laheri na siku hii, akashangaa na kusema kila-laheri ya nini na ina maana gani, kwani yeye yupo shambani, anahangaika na kupalilia shamba,kwani mvua kidogo zimenyesha na mazao yatazungukwa na majani.

‘Leo ni siku ya wanawake duniani, ndio nakutakia siku njema..’ nikamwambia

‘Hizo siku za wanawake huku kijijini tunazo kila siku, …, labda nyie huko mjini mnazipata mara moja kwa mwaka’ akaniambia

Nafikiri hakunielewa, au alikuwa kabisa hajui , siku hiyo ina umuhimu gani kwake. Alianza kunielezea shida zake zake kuwa sasa hivi sukari hawaiwezi tena kununua kwani bei ni juu kuliko uwezo wao, wanachofanya ni kununua miwa, kuikamua itoe juice waweke majani basi ndio chai, na kwasababu hiyo miwa imepanda bei pia, kwahiyo ili wapate nguvu asubuhi wanakunywa uji wa chumvi…Ndio maana niliulizia swali hili kwenye blogi moja, je nyie mnaosherehekea siku hii ya wanawake huku mjini na kupewa tunzo nakadhalika mliwahi kunywa uji wa chumvi.

Kwa uoni wangu hawa wanawake wa kijijini wanahitaji tunzo kubwa sana, na sijui ni nani atawapa hilo tunzo,…zaidi ya kutumiwa shida zao, kisiasa na mwisho wa siku hakuna wanachopata. Nasema hivi kwasababu hakuna anayewaona kihalisia, na wakihadithia madhila wanayoyapata wengine hawaamini kuwa ni kweli, mpaka janga litokee ndio watu wanashituka, hivi kweli, na hata wengine wanachukulia matatizo yao kama hadithi za pauka pakawa. Na hata wengine huwazihaki na kuwaambia hawawajibiki. Kwanini wamekubali kuolewa na kunyanyaswa na waume zao, ambao wamewaoa na kuwatelekeza huko vijijini huku waume zao wako mjini wakistarehe.

HONGERENI SANA AKINA NA MAMA KWA SIKU HII MUHIMU, NA WALIOPATA TUNZO HONGERA SANA, MNASTAHILI SIFA, NA NINA IMANI MWAKANI MTAWAPA TUNZO HATA AKINA MAMA WA KIJIJINI KWANI WANASTAHILI SANA KUIPATA HIYO TUNZO KULIKO MTU YOYOTE!

Ni mimi: emu-three

8 comments :

Anonymous said...

Mbona umeichelewesha kuitoa hii, ilitakiwa jana, siku yenyewe...lakini sio mbaya, natumai ujumbe umefika.
Nami naungana nawe kuwa kijijini ndipo panapostahili tunzo, lakini ukumbuke matuzo, wanapewa `watetezi' au waliofuzu, au...labda
Shukurani, sina cha kuandika zaidi kwani umemaliza kila kitu

chib said...

Hta nami nimekosa cha kuongeza!!

EDNA said...

Asante sanaaaaaaaa.

EDNA said...

Asante sanaaaaaaaa.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Akina mama wa kijijini ndiyo mashujaa wa jamii yetu. Bila wao kusingekuwa na familia.

Japo hawatambuliwi rasmi, sisi tuliotoka huko tunao wajibu wa kuwakumbuka na kuwaenzi. Kama tuna kauwezo kidogo tuwakumbuke kwa kuwapunguzia baadhi ya kero walizonazo. Badala ya kunywa bia mijini, tuwachimbie visima vya maji, tuwajengee nyumba zenye hadhi za kuishi, tuwasaidie kwa kadri tuwezavyo.

Tunakuwa hatuwatendei haki kama na sisi tuliotoka huko tunakakawana huku mijini, tukawasahau na kuendeela kuponda raha. Siku ya siku inafika tunaaga dunia na kusafirishwa kurudishwa huko huko vijijini tulikotoka na kuwaongezea madhila zaidi. Ujumbe mzuri sana !!!

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante! na pia Hongera nyingi ziwafikia akina mama,bibi, dada, mabinti na akina shangazi wote duniani

Anonymous said...

Pamoja na kwa kinamama wa kijijini wana tabu zaidi kuliko wa mijini lakini bado wanawake wengi tuko kwenye tabu. Umezungumzia jela ya Ujinga, sidhani kama bado tumefungiwa ndani ya hii jela pengine labda tu bado kwenye hii jela pamoja na elimu tulizonazo. Ama pengine huu ujinga uko kwa wenzetu wa upande wa pili wasiotaka kukubali kuwa dunia hii imebadilika, na ambao bado wanatumia visingizio mbali mbali vya kiaidiolojia kumkandamiza mwanamke kimojawapo kikiwa dini kwa kuwa tu hawajaelewi vizuri mafundisho ya dini yanasemaje, hapa ninaongelea dini ya kiislam na mwanamke wa kiislam alivyothaminiwa na dini yake. Lau kama wanaume wa kiislam wangelielewa au wasingekuwa wajinga wasiofahamu dini yao inasema nini kuhusu wajibu na majukumu yao katika familia basi mwanamke wa kiislam asingekuwa na mzigo mkubwa wa kazi za nyumbani. Tabia zile ambazo ni mafundisho ya dini ya kiislam ndio zimeigwa na wanaume wa kimagharibi na wamefiminist ambao wanapigania haki za wanawake.

Wengine inabidi mwisho wa mwezi ukabidhi mshahara wote kwa mume au kama anafanya biashara basi ama atapewa majukumu makubwa ya nyumba au na yeye atoe mapato yake kisa tu amepewa ruhusa ya kufanya kazi au kusoma na mumewe. Hayo yanafanywa wakati upande wa dini mali ya mwanamke aipatayo kwa shughuli zake ni yake yeye mwenyewe kuitoa kwa mumewe au familia yake iwe kwa mapenzi yake kwa mumewe na kwa mola wake!

Labda niishie kwa kusema tu pamoja na elimu yangu, elimu ya mume wangu mimi ni mmoja wa wanawake wengi waliobeba majukumu mazito ya kutunza familia. Na hayo niliyaona pia miaka mingi nilipokuwa mdogo, nilishuhudia mzazi wangu wa kike pamwe na elimu yake ya Phd bado alikuwa na mzigo mkubwa wa malezi na kutimiza mahitaji ya familia yake. Labda kwa kuwa kundi hili la wasomi linaonekana kuwa limeelimika na lina unafuu katika nyanja nyingine za maisha lakini suala la mfumo dume bado linawaathiri sawa na wanawake wa kijijini.

emuthree said...

Anony wa, March 10, 2011 11:28 PM;
Ujumbe wako ni safi kabisa, kuwa elimu ni sawa, lakini bado wapo wenye elimu ambao , elimi hiyo haijawabadili.
Labda elimu ambayo ipo kama haipo ni elimu ya dini. Na kwa kutokuelewa kwao vyema elimu ya dini yao inasemaje kuhusu haki za ndoa, haki za mke,...watu(waume) wanajikuta wakiwatendea wake zao sivyo dini inavyotaka, na kunazidisha machungu na mzigo mzito kwa mwanamke...
Je wengine mnasemaje?