Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, March 22, 2011

Maisha yana kila aina ya mitihani-2


‘Una taarifa zozote za jamaa yetu kwani tulipoachana siku ile akisema anaitwa na polisi sijamsikia tena, ..” nikamuuliza mwenzangu ambaye tulikuwa naye siku ile, naye akanijibu kuwa hajawasilina na huyo jamaa yetu ..akashauri tumuendee ofisini kwake. Tulipanga twende kwake muda wa jioni ambapo kutakuwa hakuna mishughuliko mingi, na wafanyakazi wengi watakuwa wameondoka.


Tulifika tukamkuta yupo anajiandaa kuondoka , akashituka kidogo kumtembelea bila taarifa, lakini kwa vile anatujua kuwa sisi ni rafiki zake wa karibu sana, akatukaribisha ofisini kwake.

‘Karibuni, unajua nilikuwa nataka kutoka, manake nyumbani wife hayupo..na …ok’ akatukaribisha kwenye makochi ya wageni na kutuletea vinywaji.

‘Sisi hatukuja kukupotezea muda wako, kwani huu ni muda wa kwenda kuiona famlia yako na sidhani kama wife wako anajua kuwa utachelewa, kwahiyo jambo lililotuleta hapa nikujua kuwa upo usalama, kuhusiana na ile kadhia yako na mfanyakazi wako, …’ tukamuuliza, yeye akacheka na kutikisa kichwa.

‘Rafiki zangu maisha yana mitihani mingi sana, na unaweza ukajifanya wewe upo makini kwa kila jambo, lakini ipo siku moja unaweza ukanaswa na mtihani mdogo tu…na hivyo ndivyo ilivyotokea kwangu, …umakini ulinitoka kwa masaa machache na mengi yametokea ambayo yamenifanya nijute sana, lakini yataisha tu,… kwasababu sijakwenda kinyume na misingi mizima ya…’kabla hajamaliza simu ikaita.

‘Halloh, ndio bado nipo ofisini, nina wageni kidogo, vipi unapiga simu toka wapi…nyumbani, umefika mke wangu…oh, hata bila taarifa, ok,tutaonana nyumbani, una wageni…wazazi wako..kwani vipi tena, nilshakumabia…. , sawa tutaongea, hakuna taabu, sina wasiwasi kabisa mke wangu…’akaweka simu chini na kutuangalia machoni.

Ndugu zanguni, huyo ni mke wangu alikuwa kaondoka nyumbani na kwenda kwao kwa hasira, …sasa karudi na wazazi wake sijui ili iweje, lakini sijali sana, najua wataelewa tu…’ akasema huku anafunga funga vitu vyake.

‘Hebu tuambie kwa kifupi ilikuwaje kabla hujaondoka, maana usiharakishe kwenda kumbe tunaweza tukashauriana lipi jema la kufanya…’ Akakubali na kukaa kwenye kiti chake !

‘Siku ile nilivyoondoka pale nilikwenda moja kwa moja ofisini kwangu, kwani maaskari walikuwa wakinisubiri kama nilivyoambiwa kwenye simu, nilipofika ofisini kwangu nikawakuta wameshakaribishwa ndani kwenye ofisi maalumu, nikawafuata moja kwa moja kwenye ofisi hiyo, na kuwasilikiliza wanasema nini;

‘Ndugu Bosi, tumekuja hapa , kukuulizia maswala machache na kupata tarifa kamili, kwani kama hatukosei wewe ndiye uliyepiga simu polisi kuiarifu kuwa umemkuta mwanamke, kwa jina Rose, ambaye ni mfanyakazi wako, kanywa sumu, au sio? ‘ akaluliza polisi nami nikawajibu kuwa ndio mimi niliowapigia simu.

Mmojawapo aliyejitambulisha kama askari mpelelezi akaniomba nieleze ilikuwaje, nikawaambia kuwa kama kuna lolote baya inabidi nimuite wakili wangu, kwani hapo nipo ofisini na mambo ya kiofisi yanaendeshwa kiofisi, wao wakasema kwa muda ule walikuwa wakitaka taarifa fupi , kwa ajili ya kufungua jalada lao, kama itahitajika wakili itakuja baadaye.

‘Sawa,…’ nikawaelezea kuwa, ` mimi nilifika pale asubuhi, nan i kawaida kuwa mara nyingi nampitia mfanyakazi wangu huyo, kwani wao wapo njiani, nikielekea kazini napita hapo, na mara chache sana nikiwa nimechelewa namkuta keshaondoka. Basi siku hiyo nilipofika hapo nyumbani, asubuhi kiasi cha saa kumbi na mbili na nusu, nikapiga hodi, lakini kulikuwa kimya…’

‘Kwa vile huyo mwanamke alishaniambia kuwa mume wake kasafairi, nikaona labda kapitiwa na usingizi, au lolote linaweza kuwa limetokea kwani jana yake aliondoka ofisini akiwa hajisikii vyema…’ nikawaambia polisi nikificha ukweli.

‘Hajisikii vyema kwa vipi..?’ akauliza polisi.

‘Alisema anajisikia vibaya kwahiyo anakwenda nyumbani kupumzika…’ nikazidi kusimamia kwenye uwongo huku nikiwaza yale maneno ya Rose aliyoniambia kuwa `kwa vyovyote iwavyo nisije nikasema ukweli wa hilo aliloniambia…’. Nilijua pale nasema uwongo, lakini uwongo wa kulinda ahadi niliyoiweka kuwa sitasema siri yake…ilibidi iwe hivyo

‘Ok, endelea tutajua hilo baadaye..’ akasema yule askari mpelelezi

‘Niligonga mlango na kuita mara nyingi bila kusikia lolote, mpaka nikaingiwa na wasiwasi, nikajiuliza nifanye nini, nikachukua simu yangu na kupiga namba ya huyo mwanamke , ikawa inaita- inaita bila kupokelewa, na kwa mbali nikasikia simu hiyo ikiita humo ndani, kwahiyo , nikawa na uhakika kabisa kuwa yumo ndani, labda anaoga au yupo katika hali ambayo anaogopa kunikaribisha , siunajua tena ni asubuhi na wanawake hawapendi kukutana na watu asubuhi kabla hawajajiweka sawa. Nikasubiri kama nusu saa nikaita tena, kimya, nikapiga simu ikawa inaita …hadi inakata, haipokelewi nikaingiwa na wasiwasi, …nikaona labda nijaribu kufungua mlango …’ nikasita hapo kidogo, nikijua hapo nilifanya kosa

‘Umsesema ulijaribu kufungua mlango, huwa mara kwa mara ukija hapo kumchukua unafanya hivyo..?’ akauliza yule mwana usalama.

‘Nakumbuka ilishatokea hivyo, lakini baada ya wao kuniambia hivyo… kuwa nifungue mlango upo wazi…., lakini safari hii hakukuwa na sauti ya mtu kuniambia hivyo, nikaona nijaribu tu kufungua…’ nikasema kwa kujitetea

`Endelea , hilo tutalijua baadaye..’ akasema yule askari.

‘Niligusa kile kifungulio cha mlango na kwa maajabu nikakuta mlango unafunguka, …hii ilinishitua sana, nikaita tena kwa sauti, lakini kulikuwa kimya kama hakuna mtu. Nikaingia ndani na kutizama huku na huko, nikawaza nifanyeje, nikapiga ile namba , na nikasikia mlio wa simu ukitokea chumba kimojawapo, nikaita kwa nguvu mara nyingi, sikusikia sauti ya mtu. Nikaona jambo jema ni kujua nini kimetokea, nikaamua kufungua chumba hicho simu inapotokea…’

‘Hujawahi kuingia hicho chumba kabla…na kwaniniusifikiri kuwa katoka kwenda dukani…’ akauliza askari usalama.

‘Sijawahi kuingia humo, nitaingiaje chumba cha watu, tena chumba cha kulala,…na wazo la kuwa labda katoka kwenda dukani nilikuwa nalo, nilisubiri kwa muda, nikiwaza hivyo, lakini akili ilituma kuwa kuna jambo lisilo la kawaida…na mara nyingi nafika hapo, nakusubiri barazani , kama ni lazima, lakini wakati mwingi nasubiria nje ndani ya gari langu.

‘Inakuwaje mara nyingine uingie hadi ndani na mara nyingine unasubiri nje..’ nikaulizwa tena

‘Kama nina maagizo ambayo ni muhimu, kwa mfano namuhitaji Rose.. nikiwa na maana huyo mwanamke akayafanye mambo fulani ya kikazi, na kwa minajili hiyo namuachia nauli au namwangiza tu, na mimi narudi nyumbani au naelekea sehemu nyingine kikazi. Na mara nyingi kama tunaondoka naye namsubiri nje ya gari..’ nikaielezea.

Endelea, naomba unielewe kuwa tunachotafuta ni ukweli, sio kwamba unashukiwa kwa lolote lile..’ akajitetea yule askari usalama, nikamkubalia na kuendelea na maelezo yangu.

‘Basi nikakisogelea kile chumba na kabla sijakishika, nikawaza mbali, labda kuna jambo limetokea baya na mimi naweza kufanya makosa ya kuacha alama za vidole, nikachukua anjifu yangu nikajifunga mkononi, halafu nikafungua kifungulio cha mlango, na malngo ukafunguka nusu, nikaita mara mbili kimya, nikaufungua kwa mapana ya kuweza kupita mtu, nikachungulia kwa ndani. Sikuweza kuona kwa uwazi zaidi, nikaita mara mbili kimya. Nikaingia ndani ya chumba, nilijikuta nipo kwenye chumba cha kulala, kwani ndani kulikuwa na kitanda kikubwa, meza ndogo na namna namna kama chumba cha kulala kinavyokuwa.

‘Moyo ulianza kunienda mbio, kwasababu ..’ akanikatiza askari usalama.

‘Kabla ya hapo, mazingira ya mle ndani uliyakutaje?’ akauliza askari usalama

‘Mhh, yalikuwa kama chumba kingine cha kulala, ila kulikuwa kimya, na kila kitu nilikiona kipo sawasawa, ila nilipogeuza macho na kutaizama kitandani…’ akanikatiza askari usalama tena.

‘Nina maana kuwa hakuna mihangaiko, yaaani nguo , vitu kudondoka kila mahali au …kama chumba kiwavyo, kulionkanaje, na uliona nini kischo cha kawaida..’ akauliza yule askari, nilijua ananitega , nikakaa kimya kama nawaza, na kweli nilikuwa nikiwaza mbali sana, jinsi ilivyokuwa siku ile:

Mle ndani kulikuwa kimya, na hutaamini, nguo na kila kitu vilikuwa vimepengwa safi kabisa, utafikiri hakuna mtu ndani, kama ndivyo wanavyoishi hivyo kila siku basi wana utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa kila kitu kinakaa mahala pake. Niliogopa sana kutizama kitandani, nikiwa nawaza mengi, na moyo wangu ulifikiria mengine tofauti na nilivyokuta. Haya niawaza kichwani sio kuwa nawaambia askari usalama

Niliwaza kuwa akina mama ni wajanja sana, kuwa huenda anaweza akawa amefanya vile kimtego, kuwa niingie, na nimkute katika hali ya kuninasa kitamaa, yaani nimkute akiwa uchi au…jinsi ambayo itanifanya nitamanike na yeye, kwasababu alishaanieleza nini lengo lake na ikizingatiwa kuwa mume wake hayupo! Haya sikuwaeleza polisi hivyo, ila nilikuwa nawaza hivyo siku ile, kwani kama ningewaelezea hivyo wangeliniuliza zaidi na mwisho wa siku ningelijikuta natoa siri ambayo haikutakiwa kujulikana.

Nikageuza uso kidogokidogo nikiogopa na mpaka uso wote ukawa ume-eleeka kitandani, ndipo nikashikwa na mshituko mkubwa sana.Mshituko huo ulinifanya nisahau kuwa mwangalifu, hata kile kitambaa, nilijikuta nikiweka mfukoni badala ya kukivaa mkononi. Nikakurupuka mbio hadi pale kitandani, na…., lakini nikashituka kidogo, kwani alikuwa hajavaa nguo hata moja, lakini kwa hali aliyokuwa nayo sikuweza kukumbuka hayo.

Mapofu meupe yalikuwa bado yanatoka mdomoni, , lakini mwili ulikuwa umetulia kabisa, na macho yametoka kuangalia juu, …kuonyesha kuwa uhai pale ulikua mdogo, na pembeni nikaona gilasi ya maji na baadhi ya vidonge vikiwa vimabakia mezani, na hiyo ilikuwa dalili moja kuwa huyo mwanamke alikuwa kanywa vidonge vingi kujiua au…nikashika shingoni kutizama mapigo ya moyo, nilihisi bado yapo!

Sikupoteza muda nikakimbilia nje ya kile chumba na kutafuta mueleeko wa jiko au popote kwenye kabati wanapohifadhia vitu, nakumbuka kabisa kuwa huyu mwanamke alikuwa na biashara ya maziwa ya ngombe, kwahiyo hiyo ilinipa faraja kuwa nitakuta maziwa mle ndani. Na kweli nilipofika kwenye jokofu la kuhifadhiwa vitu kama maziwa yasigande nikakuta ndoo ya maziwa, harakahraka bila kujali , nikachota maziwa kwenye kikombe na kurudi nayo chumbani.

Nilihararakisha na kujaribu kumfungua mdomo ili nimnyeshe,. Ilikuwa kazi ngumu kidogo , lakini baadaye nilipata upenyo wa mdomo na mziwa yakapita, na nilishukuru kuwa maziwa ya kutosha yalikuwa yamepita mdomoni hadi tumboni. Nilihakikisha kuwa hili limefanyika, harakka haraka nikaangalia mzingira ya mle ndani, nikaona karatasi juu ya kitanda. Kabla ya kuisoma nilitafuta gauni au nguo ambayo nitamvalisha ili watu wakija wasije wakamkuta katika ile hali! Na nilipomuweka katika mazingira mazuri nikaisoma ile karatasi, iliandikwa hivi:

Kwa mume wangu

‘Samhani sana mume wangu kwa kuchukua uamuzi huu, ila nimeona maisha hayana maana kwangu,, kwani kama wewe umeamua kuwa mtoto ni muhimu sana kuliko mapenzi yetu, na mimi inavyoonekana sina uwezo huo wa kukupa mtoto, kwa muda unaotaka, na huenda kwa hili ninaweza nikaadhirika zaidi, na ili kukwepa kuadhirika zaidi nimeona nikuachie nafasi ili uweze kumpata mwingine, lakini sitaweza kuona ukimpata mwingine, ilihali sijui kosa langu ni lipi…huu ndio uamuzi wangu muafaka, na naomba uniombee msamaha kwa bosi wangu kwa kumshirikisha kwa jambo lislomuhusu, nilifanya hivyo kwa nia njema kabisa, kama ulivyopenekeza wewe mume wangu

Kwaheri..

Niliitizama ile barua nikaona kama itabakia pale na polisi wakaiona, huenda ikanitia matatani na mimi, na hata siri aliyotaka isitoke itakuwa imejulikana, ingawaje haijasema wazi …

`Hebu utuambie ulimkutaje huyo mwanamke..’ akaniluliza yule mwana usalama baada ya kuniona nimetulia kwa muda, kwani nilikuwa nawaza mbali, nakuisahau kuwa nilikuwa naulizwa maswali na natakiwa uyajibu kwa uangalifu.

‘Nilimkuta akiwa kalala huku anatoa mapofu mdomoni, na pembeni ya kistuli nikaona gilasi na dawa, vidonge viwili …na nilipotizama ile karatasi nikajua kuwa huenda kulikuwa na dawa zaidi na huyo mwanamke atakuwa kameza zaidi ya kawaida, mimi sikupoteza muda nikatoka mle nakutafuta maziwa na kumnyesha kwa nguvu, na wakati wote huo alikuwa kama kazimia, nilijitahidi mpaka maziwa yakaingia mdomoni, na bahati nzuri yakawa yamepita hadi tumboni.

Basi baadaye nikawapigia simu nyie, na hospitali yetu ambapo wafanyakazi hutibiwa ili wae wamchukue …na wao walisistiza kuwa niwaarifu polisi wafike, ilii wakifika hapo kuwa hakuna matatizo. Nilipohakikihsa kuwa taarifa zimefika kwenu na makasema mnakuja, mim nikaona niwahi ofisini kwani kulikuwa na wageni muhimu wa kikazi nawategemea asubuhi hiyo..’ nikamalizia hapo.

‘Sawa maelezo yako tumeyapata, na kwa ufupi hali ya mgonjwa ni mbaya sana…, hatujui hatima yake, na madakitari wanahangaika kuokoa maisha yake, na mpaka tunaondoka, walikuwa wamefikia hatua ya kumfanyia upasuaji kama itasaidia na mume wa huyo mwanamke alishafika, …kwa taarifa tu za harakaharaka huyo mwanaume, kasema atafungua kesi kuwa mke wake kanyeshwa sumu , kwani ni mcha mungu asingeweza kufanya jambo kama hilo, kama alivyodai kasema `huyo aliyejifanya kumnyesha maziwa ndiye atakuwa kasababisha, au anahusika na kutaka kumuua mke wake, kwahiyo atafungu kesi na huend wewe ukama mshukiwa muhimu wa yote, akifa wewe utakuwa mshukiwa namba moja, akipona bado una kesi na mume wa huyo mwanamke…!’ akasema yule askari usalama.

Basi waliondoka, nikabakia ofisini nikiwa nawaza, wapi nimefanya kosa, nilisita kumuita wakili wangu mapema kwani nilikuwa sijaona kosa lipo wapi, lakini pale waliponielezea kuwa hali ya huyo mwanamke ni mbaya sana, nikaingiwa na wasiwasi. Nikamuita wakili wangu nikamuelezea juu , juu, lakini sikumuelezea kiundani wa kila kitu , hasa nikificha ile siri niliyoambiwa niitunze.

‘Ni hayo ndugu zanguni,…ilivyokuwa siku ile’ akasema huku anasimama.

‘Sasa mke wako kajuaje?’ nikamuulizia.

‘Hilo ni balaa jingine rafiki zangu, lakini hilo ingawaje ni kubwa kuliko,lakini lipo ndani ya mikono yangu, kitu ambacho nimeshindwa kujua….sijui mke wangu alijuaje, kwani polisi walipotoka tu kunihoji, akaingia …unajua nani,?’ akauliza kama haulizi kwani baadaye akajibu mwenye ` …mke wangu’

‘Alikuja macho yameiva, mkononi kashika begi la safari, …nilibaki nimeduwaa, nikijiuliza safari hii ya haraka ni ya nini, kwasababu nilikuwa na uhakika kuwa hajui nini kimetokea, ….hakupoteza muda akaniambia kuwa kayapata yote, kuwa mimi nina mahusiano na mfanyakazi wangu, na katika mahusianao hayo imefikia hatua mwanamke wa watu kujiua, …. Na huenda nimempa ujauzito na nimeukataa ujauzito huo, ndio maana akaamua kujiua…kwahiyo yeye kachoka kudanganywa anaondoka kwao, ili aniachie nafasi ya kumaliza mambo yangu na huyo mwanamke, …akasema `hawara wangu’, ikibidi talaka yake imfuate huko, nilikomtoa….’ Alipofika hapo akashika kichwa na uso ukajaa huzuni…

Je ilikuwaje baadaye...naomba tusikose sehemu muhimu inyofuata!

Ni mimi: emu-three
Enhanced by Zemanta

7 comments :

Fadhy Mtanga said...

M3 ahsante sana sana kwa simulizi hii. Nakiri huwa napata wakati mzuri sana kila siku ninapotembelea humu na kuvisoma visa hivi.

Hongera sana kwa uandishi mzuri wenye kusisimua.

SIMON KITURURU said...

Duh! mie naisubiri sehemu ijayo kwa maana duh!

Yasinta Ngonyani said...

Kisa hiki kina mitego mingi kweli ni kizuri kinasisimua na utamu unakolea. Halafu inaonekana hakuna uaminifu. Maana sehemu ya kwanza mume wake Rose alimtuma akatafute mtu afananaye na yeye na sasa amebadilika je yeye alifikiria nini. Bosi naye kafikiri anatenda wema kumbe??? na mke wa bOsi nani kamwambia haya yote ??? Aise nahisi nitapata jibu muda si mrefu....Simuliza/kisa nzuri MMM.

Candy1 said...

Mmmmh...yanazuka mengine baada ya mengine na binadamu sisi tuna-react sana bila kujua hali halisi ya tukio lolote...haya mi nipo

John Maembe. said...

Duuuuh mambo yamekuwa mambo.

Aisee niko faster kidogo lakini nachotaka kusema ni kuwa WEMA WAKE UMEMPONZA SASA MACHUNGU YA DUNIA ATAYAONJA" km Rose akifa unadhani nini kitafuata baadae jamaa lazima apandishwe kizimbani na maneno yakipishana kidogo tu, Selo itamwita.

Thanks m-3 & Goodbye.

Anonymous said...

JAMANI BADO TUNASUBIRI MUENDELEZO WA KISA HIKI MIRAM3! MBONA KIMYA

emu-three said...

Ilibidi nisitishe kisa hiki kwa muda ili tuendeleze kisa cha dawa ya moto ni moto kutokana na ushauri kuwa tumalize kisa kimoja kwanza tusichanganye visa zaidi ya kimoja