Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, February 25, 2011

Uvumilivu una mipaka yake!


`Mfanyakazi huyu anatafutwa na muajiri wake, kwa kushukiwa kutoroka na mamilioni ya hela, zawadi nono itatolewa kwa yoyote atakayetoa taarifa wapi alipo….’


Sikuweza kuendelea kusoma yale maelezo, kwani macho yangu yalivutika kuiangalia ile picha ya mtuhumiwa. Nilipikicha macho kuhakikisha kuwa kweli huyu ninayemuona kwenye picha ndio yeye kweli, yule jamaa ninayemfahamu au ni kufanana kwa sura, kwani dunia hii ni wawiliwawili. Na wakati nakodoa macho kuiangalia vyema ile picha, simu yangu ya kiganjani ikaita

‘Halloh, mkuu umeona gazeti la leo la habari, lina picha ya rafiki yako, anatafutwa na polisi…’ simu ikaendelea kuelezea, lakini mimi nikawa nimezama kwenye, na kukumbuka enzi wakati nasoma na huyu jamaa. Alikuwa mpole, alikuwa hapendi vurugu, alikuwa mtu ambaye kila mtu alimwamini kwa tabia na utendaji wake... Nakumbuka kuna kipindi kulitokea mgomo, jamaa huyu hakujihusisha kabisa, na alipewa zawadi ya nidhamu.

Kipindi nipo nafanya kazi na yeye kabla fagio la walalahoi halijapitishwa na kunikumba mimi na wenzangu, ambao tunadau haki yetu mahakamani hadi leo tuliwahi kufanya mgomo, kushinikiza malipo bora ya wafanyakazi, jamaa huyu hakujiunga kweny emgomo huo, na ndicho kilichomfanya aendelee kuwepo kazini hadi tulipoona hili tangazo kuwa `anatafutwa na mwajiri wake, kwa kupitia polisi kwa kutoweka na mamilioni ya hela, tena za kigeni!

‘Bwana mimi nampa mkono wa hongera jamaa yetu huyu, najua wizi ni mbaya lakini kwake yeye kachukua haki yake aliyodhulumiwa..hajaiba, sisi tuliojifanya waumini tumepata nini zaidi ya kusota mitaani tukiwa mafupa, baada ya kuitumikia kampuni miaka kumi na zaidi, kwa bidii na uaminifu, wanakuja wengine wanakula kilaini…sisi tumepata nini kama sio kutupwa nje kwa dharau…’ akaendelea kuongea jamaa yangu kwenye simu.

Nilimkumbuka sana jamaa yangu huyu siku za karibuni nilipokutana naye, nilimuulizia vipi maendeleo ya huko kazini kwao. Alisema kwa unyonge maneno haya; ‘mimi nimeamini kweli maneno matakatifu kuwa tajiri kuuona ufalme wa mbingu ni kama farasi kupita kwenye tundu la sindano’ Nikamuuliza vipi kulikoni, kwani siku zote ulikuwa mstari wa mbele kuwatetea matajiri kuwa wanafanya haki na wanaoharibu ni wafanyakazi kwa kuwa wavivu…

‘Ndugu yangu, hutaamini tangu muondoke, mshahara wangu ni ule ule haujawahi kuongezeka, licha ya kufanyakazi kwa bidii kwasababu tulibakia wachache, licha ya kuonyesha uaminifu wa hali ya juu, na…lakini hakuina cha nyiongeza wala ahadi za kuaminika,…fikiria hali za maisha sasa hivi, yanazidi kuwa magumu, kwa gharama za vitu kupanda bei, majukumu yameongezeka, kwani nimeoa, na nina watoto, na isitoshe dada yangu alipofariki kaniachia watoto, watoto yatima, hawana baba wala mama, mimi ndio baba yao, mimi ndio mama yao…siunakumbuka mume wa dada yangu alifariki kipindi kile mpo kazini, basi baadaye nikawachukua dada na watoto tukawa tunaishi nao, dada yangu akaanza kuumwa baadaye nikahangaika naye kwa matibabu huku na kule…

‘Hutaamini, nilikuwa naomba angalau mkopo ili nikamtibie dada yangu nilinyimwa, ili hali mimi nashika hela zao mamilioni kwa mamilioni, mimi ndiye mtunza pesa wao, naenda benki nachukua mamilioni yao kuwalipa, lakini hawakukubali kunipa mkopo wa kumtibia dada yangu, eti mshahara wangu ni mdogo, nimeshachukua mkopo mwingine haujaisha makato, kwahiyo sistahili kupata mkopo mwingine.

‘Ni sawa sheria hiyo ipo, lakini kuna dharura kama hiyo ya ugonjwa, hata hivyo kwanini wasiniongezee mshahara wakati wanaajiri wafanyakazi wapya ambao wanakuja hawajui kitu kabisa mimi ndio nawafundisha kazi, na kutokujua kwao kazi, bado wanalipwa mishahara mikubwa zaidi yangu, hebu fikiria, mimi nakisomo changu nalipwa laki tatu, wao wanalipwa milioni tatu, …ni haki hiyo kweli. Wamenizidi nini mimi, eti kwasababu wanatoka nje, eti kwasababu ni watoto wa wakubwa, eti kwasababu ni ngozi nyeupe, eti…wanatoa sababu ambazo haziniingii akilini…

‘Sasa watoto wa dada wamfukuzwa shule, kwasababu ya ada, nashindwa nifanye nini, kwani wakati wazazi wao wapo walikuwa wakiwasomesha shule nzuri za binafsi, na nikaona niwatoe hapo niwapeleke shule ya gharama ndogo kidogo, lakini hata hiyo nimeshindwa kuwalipia…sasa hivi yupo mmoja anaumwa, kila mara , wakati mwingine anarudishwa nyumbani kutoka shuleni kwa sababu ya matatizo ambayo yanahitaji hela nyingi za matibabu, sina hizo hela, nimeomba kazini nimenyimwa…

‘Kumbuka mimi ni cashier pale ofisini, mimi ni mhasibu, mimi nafanya kazi hata za mauzo…wanajua wao kuwa mimi ni `kila kazi’ hapo kazini, hata chai za mabosi natengeneza…wananilipa nini hawa watu zaidi ya kunipa sifa za mdomoni, na ikifika muda wa maslahi wanakuwa hawanijui kabisa, eti kwasababu `sina title’ mtoto wa mlalahoi anayeishi `uswahilini’ kama wanavyopenda kuita wao wenyewe!...sasa nifanyeje, nimechanganyikiwa ndugu yangu, kama una chochote naomba uchangie matibabu ya mtoto huyu, anateseka sana, naomba muwe na Huruma, kwani akifa, nitasononokea sana, inafikia muda anasema `kama wazazi wake wangelikuwepo hai angeshapona…’ Alipofika hapo mzee mzima machozi yalimtoka

Nilitaka kumwambia `unaomba jamvi msibani’ lakini nikatuliza kauli hiyo kwani akuombaye msada kwenye dhiki, usimkate kalima kwa kutoa matatizo yako pia, toa hata msaada wa ushauri, kuliko kuanza kuelezea na wewe una shida hii na ile, kuwa eti na mimi nadaiwa na mimi sina hela ya kula, na mimi…sio busara. Nilimpa nini, mungu ndiye mwenyewe anajua…!

Leo nasoma tangazo hilo kuwa jamaa yangu huyu anatafutwa na polisi kwa kumuibia mwajiri wake. Sikuamini kabisaa, mpaka aliponipigia simu mtu ambaye alikuwa karibu naye! Na huyu aliyenipigia simu amemsifia ndugu yetu huyo kuwa kafanya jambo la maana saana, kwani hata kama angefanyakazi hapo hadi akongoloke, asingeweza kuzipata hizo hela, akaongezea kuwa `kachukua jasho lake ambalo alikuwa akinyonywa , miaka nenda rudi.

Nchi yetu hii inapokwenda ni kubaya, kwani makampuni mengi yaliyopo hapa nchini hayana utawala bora, watawala waliopo wanawagawa wafanyakazi kimatabaka, wazungu na Wahindi toka nje wanalipwa zaidi ya huko kwao walipotoka, kila kitu analipiwa, na mshahara wake ni ule wenye sifuri sita kwenda mbele, nyumba analipiwa, watoto wanasomeshwa, analipiwa hadi karatasi ya chooni.

‘Mimi kama ningekuwa raisi ningesema tuwaajiri wazungu tu hapa nchini , kwani ni wachapa kazi,waaminifu….siunaona mwenyewe wanavyojituma…’ hii ni kauli ya meneja wetu wakati anafuatilia vibali vya kumuingiza bwana fedha toka India.

Ni kweli wanachapa kazi, ni kweli ni waaminifu, lakini wanafanya hivyo kwa kuwa wao wana sababu na motisha! Niliwahi kuuliza swali kwa hawa `wakubwa’ kuhusiana na mslahi ya wafanyakazi kuwa je gari lililojazwa robo tanki linaweza kusafiri sawa na lile lilojazwa tanki zima. Bofya hapa! Safari ni moja wengine magari yao `fully tank with reserve’ kwasababu za rangi yao, dini yao, mmmh, mwenzetu nk ,wengine robo tanki na hakuna hata akiba, unategemea huyu mtu ajitume sawasawa na huyo wa fully tank? Jamani hivi kweli hii ni haki, nakumbuka usemi wa mkuu , kwenye blogi yake alisema `mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni…itafika muda watu watadai haki yao, kwani `uvumilivu una mipaka yake, ikizidi sana,,,ndiyo hayo …migomo, maandamano…mwisho wa siku, hakukaliki tena! Wabunge Mpo?...mmh, najua hili haliwagusi sana, kwani nyie ni `matawi ya juu’

Hilo ndio wazo langu la ijumaa ya leo!


Ni mimi: emu-three

7 comments :

Yasinta Ngonyani said...

nanukuu"Nchi yetu hii inapokwenda ni kubaya, kwani makampuni mengi yaliyopo hapa nchini hayana utawala bora, watawala waliopo wanawagawa wafanyakazi kimatabaka, wazungu na Wahindi toka nje wanalipwa zaidi ya huko kwao walipotoka, kila kitu analipiwa, na mshahara wake ni ule wenye sifuri sita kwenda mbele, nyumba analipiwa, watoto wanasomeshwa, analipiwa hadi karatasi ya chooni" mwisho wa kunukuu. Hakika wazo la ijumaa ya leo ni bonge la shule. Tatizo ni kwamba wafanya kazi wanaotoka nje huwa wanalipwa mshahara mkubwa hii yote ni kwasababu, huu ni mtazamo wangu mimi yaani wao huwa hawalipwi shilingi wanalipwa hele ya kikwao ndio hapo inapokuwa tafauti. lakini hata hivi si uungwana kabisa. Pia nadhani Tanzania yetu rushwa zimezidi huwa najiuliza KWANINI MFANYAKAZI ASIPEWE MSHAHAR wa kutosha? nadhani kungekuwa hakuna hizi chai chai....

Anonymous said...

Wee mwana wee temea mate chini usiseme kabisa halituhusu, mimi niliamua kuacha kazi baada ya kumenyeka miaka bila kuthaminiwa. Tena pamoja na kuanza kazi na masters yangu nilikuwa naletewa "mabosi" waliosoma digirii zao za bachelors ulaya na marekani hata kuandika ripoti hawawezi lakini mishahara yao zaidi ya mara mbili ya wa kwangu. Ukifanya kazi hauna cha kupumzika wala overtime.

Nikaona eeh, mtoto mie sina jina la kuonekana kuwa linafaa kuwa bosi, sinywi pombe wala sivuti sigara cha kufia kitu gani? Basi taratibu nikaanza kutafuta scholarship, uzuri grade zangu zote za shule ziko juu hata haikuchukua muda nikapata scholarship ya PhD yangu, hivi niko shule, na nikimaliza hata kama nitarudi nyumbani itakuwa ngumu sana kwenda kunyanyasika huko kwenye ajira ya kuajiriwa, bora nijilimie hata mboga mboga na kufuga kuku kuliko kurudia yale yaliyonikuta. Mwenye kutaka ujuzi wangu kwa wakati huo itabidi anilipe papo kwa papo na kwa maelewano yaani consultancy! Nina uzoefu wa kazi zaidi ya miaka 10, bado mtu unaonekana hujui kitu kisa sivai kimini? Siamini wanachoamini? Siendi kwenye vikao vya happy hours kunywa pombe na kupoteza muda?

Yaani wee acha tu hapa nikimaliza tu Phd yangu ikitoka kazi nchi yoyote duniani nakwenda lakini sio kufanya kazi tena Tanzania kwenye ubaguzi wa kila aina. Mbaya zaidi hata hao mabosi wangu wenyewe mbali na kulipwa mishahara mikubwa kwa kuchat kwenye social network (Ndicho wanachokijua, kazi zote wanakusukumizia wewe wa chini yake ufanye) kutwa kutengeneza madili ya wizi kupitia vijikampuni feki wanavyovipa contract za ajabu ajabu kutokana na authorities walizonazo. Na hao mabosi wao wakubwa hawawezi kufanya kitu kwa sababu wanawaamini au wanakula pamoja hata sijui maana na wao kama ulivyosema mikataba wanayopewa wakiwa Tanzania hakuna pengine duniani, yaani mtu analipiwa shule ya wanawe tena international school, analipiwa nyumba, umeme, mlinzi, genereta, gari anapewa na mafuta juu, na bado anapewa living allowance kila mwezi tofauti na mshahara wake, hiyo living allowance sawa na mshahara wa mkurugenzi wa Tanzania!

Tanzania nakupenda lakini sina hamu!

Aliyetendwa akakimbia!

Mija Shija Sayi said...

Yote yana mwisho na wa mwisho huo hauko mbali.

Uvumilivu una mipaka yake!

Faith S Hilary said...

Inasikitisha sana kwa kweli...sasa na yeye hizo millioni haziishi? Mmmh...wazo zuri ila linazua maswali mengi kama dada Yasinta hapo juu...vitu vingine havieleweki kabisa yaani/ haviingii akilini ila ni kweli, ni vitu vinavyotokea.

Simon Kitururu said...

Duh!

Mzee wa Changamoto said...

Ni zaidi ya wazo. Naamini ni TAFAKARISHI YA IJUMAA.
Nakumbuka wakati naangalia DVD moja kwa ajili ya shule inayoitwa EMPIRES OF AIR, mwisho kuna mzee mmoja alisema "mtoto mmoja aliulizwa ni kipi anapenda kati ya Radio na Tv, akasema RADIO. Baba yake kwa mshangao akamuuliza kwanini Radio? Mtoto akajibu 'picha ninazoziona ninaposikiliza Radio ni nzuri zaidi ya zile ninazoonyeshwa kwenye Tv".
UWEZO wa kujenga taswira unao,
UWEZO wa kuhusisha matukio unao,
UWEZO wa kufunza kwa matukio unao,
UWEZO wa kuonya na kuburudisha unao,
UWEZO wa kumfikirisha kila anayesoma na kutafakari UNAO.
UNANOA AKILI ZA KILA MWENYE AKILI ZA KUFIKA HAPA, KUSOMA NA KUTAFAKARI.

ASANTE

emuthree said...

Nashukuruni sana kwa kuchangia mada hii. Nimeguswa sana na ushauri wenu. Ninachoweza kusema ni kuwa , `siri ya mtungi aijua kata'...kama hujawahi kuishi maisha ya dhiki, kama hujawahi `kusota' kwa hawa `matajiri' kama ...! Basi picha ndiyo hiyo.
Ni kweli , ili ushinde majaribu, ni vyema upambane nayo, hasa kwa elimu. Huyu jamaa yangu na mimi tulikuwa naye msitari wa mbele kusoma. Lakini ilifika mahala `tukagonga ukuta' kwasababu ya `kazi' kila kazi wewe...unafanya hadi nyingine unakwenda nazo nyumbani, mwisho wa siku..`hamfanyi kazi nyie, kazi kudai maslahi...wavivu wakubwa nk'
Tatizo jingine likawa `gharama' ili usome ulitakiwa ujigharamie, kwa muda wako. Je mshahara kama huo ungeugawaje, na kwa muda upi, labda wakati wa likizo yako? Kodi ya nyumba inakusubiri na ukumbuke ukianza kazi basi, `jamii' iliyokusaidia kukusomesha inakusubiri, ulipie fadhila!...hili tutakuja kuliona kwenye visa vinavyokuja...tuombeane uzima!
Ndugu zanguni, unaposikia kuwa `tanzania...nina maaana watanzania ni miongoni mwa `best wa umasikini' duniani , usifikiri ni kwasababu ni `wajinga' hawataki kujituma, hawataki kusoma...Ni kweli wapo wenye nafasi hiyo lakini wanaichezea, ...ila kuna hali ipo inayohitaji `msukumo'
Nashukuruni na nawaomba mzidi kutupa ushauri kama huo, maoni, hasa wale waliosota na baadaye wakagundua njia, kama anyn..alivyojielezea hapo, huenda `tunateleza' au tumefungwa macho na masikio, sasa `nyie' ambao mumeliona hili, ni wajibu wenu kutuasa.
Shukurani .
nb. Mzee wa changamoto, umenipa changamoto kweli. Dada Yasinta ni kweli wanalipwa kwa dolari hiyo ni tofauti na bado wanalipwa kitu kinachoitwa `allowance' kama alivyofafanua;Anyn wa February 25, 2011 4:01 PM! Dada Candy, milioni zitaishaje, kwa tajiri au kwa mlipwaji, kwa tajiri haziishi kwasababu anazalisha na ana bahati kuwa kawapata `cheap-labour' kuacha hawo `matawi ya juu' kwahiyo mwisho wa siku ana faida!
Na kweli `yote ya mwisho kama alivyosema Da-mija!
`Duh', mkuu nimekupata!