Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, December 15, 2010

Aisifuye mvua imemnyea-11

‘Inaonekana jamaa yako sio mtu wa kawaida, na nafikiri huko alipo, yupo hoi kitandani, na tunachotakiwa nikummaliza vinginevyo atakuchezea sana…na inaonekana hayupo mbali nanyi. Lakini huyu jini waliyemuweka hapa kawekwa kulinda mali ya urithi, ina maana hili eneo ni mali ya urithi ambayo ilichukuliwa kwa wenyewe bila ya ridhaa yao, kwahiyo wakaweka haya majini kupalinda…’ Mara alinyamaza ghafla, akatikisha kichwa harakaharaka na kunikodolea macho, huku anatetemeka, na mara akatamka maneno nisiyoyaelewa, halafu akatikisa kichwa haraharaka huku mdomoni anatamka maneno kama `mbruuuuuuuu…’ akatulia huku katoa jicho la uwoga, akaanza kuyumbayumba kama mtu aliyelewa, na akawa anataka kuniambia kitu lakini mdomo haufunguki, lakini baadaye akatamla maneno haya kwa shida


‘Hawa wa-wa-wa merudi te te-te-te-na, ingi-ingi-a ndani ya gari hara-hara-hara-ka…vijana kujeni wamerudi tenaaaaaaa…..’ akadondoka chini!

********

Nikabaki nimeduwaa, nisijue la kufanya , nikatizama huku na kule ili niwaone hawo watu wanaosemwa wamerudi tena, lakini sikuona dalili yoyote ya watu.Nikawa nasita kuingia ndani ya gari, jamaa msaidizi wa yule mganga, akanisukumiza kwa nguvu niingie ndani ya gari, na nilipoingia akafunga mlango wa gari halafu yeye akawageukia vijana wengine ambao walikuwa kama wanatetemeka kwa woga, akachukua chupa iliyojaa maji akawarushia, na wao wakadonoka chini mmoja baada ya mwingine.

Jamaa alipoona kabakia mwenyewe, akatizama huku na kule, ilionekana woga ulishamwingia,akabaki kaduwaa, akachukua chupa nyingine yenye maji akayanywa halafu akayatema hku na kule huku anaongea maneno nisiyoyasikia kwani nilikuwa ndani ya gari, akayatoa maji mengine akawa anayarusha hewani, na mara akaanza kuyumba yumba, akatoa macho kama vile kaona kitu cha kutisha akaanza kuyumbayumba tena, akadondoka chini, naye kimya.

Nikatizama kushoto na kulia , kimya, nikatoka ndani ya gari, nikainua hatua moja, mbili, …mara nikasikia kitu kama uvumi, au upepo ukitoka mbali, na baadaye kukawa kimya. Nikajiuliza nifanye nini, nia yangu nikumfuata yule mtaalamu nimuangalie kuwa kazimia au vipi, kwani yeye ndiye kiongozi na kama kiongozi kashindwa, basi hakuna jinsi, waondoke tu…

Mimi mawazo yangu sikuona nini wanafanya, kwangu niliona kama maigizo fulani,…nikapiga hatua kumwendea yule mtaalamu, lakini kabla sijainua mguui mara nikasikia tena uvumi wa upepo , na sasa ulikuwa mkali kama kimbunga kinachozunguka na kutengeneza duara, ulianza kidogokidogo , halafu ukaja kwa kasi ukileta vumbi na mchanga, nikaona kulikwepa hili vumbi ni bora nirudi niingie ndani ya gari. Nikaingia na kufunga mlango, lakini upepo ule ukawa haukomi,mpaka gari likawa linatingishwa na ule upepo, nikaona hapa sasa hakuna usalama,

Nikaamua kuondoka mahala pale nikaliwasha gari, likawa haliwaki. Gari langu halina tabia hiyo, nikajaribu tena, kimya. Ina maana gari langu limeharibika, haiwezekani, nikawasha tena, kimya. Sijui kwanini wazo hili lilinijia akilini, lakini nilijikuta nikichukua kichupa cha yale mafuta aliyonipa yule mtaalamu nikayatoa na kukifungua kile kichupa, na harufu yay ale mafuta makali ikajaa ndani ya gari. Kwa ukali way ale mafuta, huwa hata mimi yananifanya kichwa kinauma, na mara ghafla upepo ule ukatulia na mara nikasikia sauti kali kama mruzi ambayo sikujua inatokea wapi, ila ulikuwa ukiumiza masikio. Nikawasha gari tena, likakubali, nikarudisha nyuma, nikaliweka sawa huyo nikaondoka zangu.

Niliendesha hadi sehemu mbali na pale nyumbani nikasubiri kidogo , halafu nikapiga simu kwa yule mtaalamu, iliita kwa muda haikup[okelewa, nikapiga tena na tena kimya, na baadaye sana ikapokelewa, na jamaa akaitikia, aliitikia akiwa kama mtu anayetokea usingizini,…!

‘Oooh, jamaa anajifanya mjanja, tutapambana naye hata ikibidi siku nzima ya leo…’ akasema akakata simu.

Nikajiuliza nirudi kule au niondoke niende zangu nyumbani kwa wazazi wangu, na nikiwaambia kuhusu hili najua watapata kisingizio cha kuniambia nyumba hiyo haifai. Hapana lazima nirudi kule nione mwisho wa haya maigizo, lakini kile kimbunga cha ajabu kilikuwa ni nini? Kuna haja ya kujua hili, katika uchunguzi wangu wa mambo haya, ni upepo wa kawaida au kuna nguvu Fulani, lazima nilijue hili, nikawasha gari kurudi kule kwenye nyumba yangu, ambayo sasa nitaiita nyumba ya vituko.

Niliendesha kwa kasi hadi nilipokaribia ile nyumba, na kwa mbali niliona wale jamaa wakikimbia huku na huko, huku wakipiga manyanga, na niliona baadhi ya watu wamekuja kuangalia nini kinaendelea, nafikiri makelele ya manyanga yaliwavuta hawa watu, hata hivyo walikuwa wamesimama kwa mbali wakiangalia nini kinachoendelea. Nikaendesha gari hadi waliposimama hawa watu nisikie wanasema nini.

Nilisimamisha gari mbali kidogo nikaja kwa miguu, na kujichanganya ndani ya kundi hili la watu, na kwa vile wote walikuwa wametekwa kimawazo na kile kinachoendelea kwenye ile nyumba, hakuna aliyenigundua, nikajifanya na mimi nashangaa ni nini wanakiangalia, na hapo nikasikia watu wawili wakiongea

‘Hivi huyu jamaa anayataka maisha yake au kachoka kuishi..’ mtu mmoja akasema

‘Labda hela zinamsumbua, nyumba hii imetelekezwa miaka mingi na mzungu, we fikiria mzungu asiyelogeka aliikimbia,sembuse ngozi hii nyeusi, ambayo ni nyepesi kulogeka…mwache tuone naye ana ubavu gani, nasikia anatoka bara, …wanasema watu wa bara hawaogopi uchawi ..ngoja tuone..’ akawa mmoja anasema huku anasogea kutizama nini kinaendelea kule, na baadaye wakanigundua , wakageuka kuniangalia.

Sikuwajali sana nikawapita na kuelekea kule kwenye nyumba, na nilipofika niliwakuta jamaa wamekaa chini wanakunywa maji, huku wengine wakijifuta majasho, na waliponiona wakatabasamu, na kusema `Kazi imeisha, jamaa kasalimu amri…utasikia kilio tu, najua yupo jirani,na nia yetu ni kumwendea nyumbani kwake, lakini tunahitaji kibali kwa mjumbe, unasemaje Docta…’ Akaniuliza yule Mtaalamu.

‘Hapana, hilo halitawezekana, kibali hicho kitoke kwa jina langu, hapana, …’ kama mumeshindwa basi

‘Nani kakuambia tumeshindwa, kazi imeisha, lakini huyu mtu anaweza akapona na kwenda kutafuta jeshi jipya, na je wakati huo akirudi tunaweza tusiwepo, unajua sisi ni watu wa kuitwa huku na huku, na nia yetu nikulimaliza hili swala kabisa…hili limefungamana na mambo ya kurithi na inavyoonekana kuna kudhulumiana, lakini huyu alienda mbali zaidi ya hayo, kama angesimamia kwenye haki, tungekushauri vingine, lakini kajikita kwenye uchawi, na hili ndio tunataka kuliondoa kabisa’ akasema msaidizi wake.

‘Kibali hatutakichukua kwa jina lako, sisi wenyewe tutakitafuta kwa jinsi yetu, wewe hili halikuhusu, huyu sasa ni adui yetu, sio wako…kwako tumeshamaliza, ila kwa vile tumemtungua lazima atataka kulipiza kisasi, na sisi hatutaki kumpa nafasi hiyo, kwahiyo wewe twende ndani na tukukabidhi nyumba yako, haina matatizo kabisa…’ akasema yule jamaa, na kwa pamoja tukaingia ndani.

Nilikuta nyumba ipo shanghala baghala, na sikumbuki hawa watu kuingia ndani, vyombo, vimedondoka vingine vimevunjikavunjika, baadhi ya viti vimevunjika, na madamu yametapakaa kila kona…palikuwa panatoa harufu ya ajabu ajabu, ikawa inanitia kitu kama kichefuchefu na nikawa naona kizunguzungu, nikatamani nitoke nje, lakini miguu ikawa haina nguvu, nikasema hata mimi ni dakitari, ngoja ninywe vidonge vyangu vya kupambana na hali kama hii, nikapekua kwenye mkobwa wangu wa dharura, kwa shida sana nikaviona, lakini kabla sijavitia mdomoni, nilisijisikia kama nainuliwa juu kwa juu nikapoteza fahamu….

                          ****Vipi tena, yamemkuta nini Doctor, tuendelee kuwemo*******

Ni mimi: emu-three

4 comments :

Anonymous said...

Hapa sasa inatisha, utafikiri unaangalia filamu za kinajeria, ningelikuwa nawajua hawa jamaa wa kinajeria ningekusukia mpango wanunue hivi bisa vyako, kwani hapa bongo sidhani kama wanaweza kuigiza vitu kama hivi, na kama wakiweza sana sana watakulalia, na huenda wameshachomoa baadhi ya visa, ...siunajua bongo hii
Nikupa hongera sana. Kazi nzuri na sijui muda gani unatumia kuandika na kazi zako nyingine, usichoke, ipo siku utatoka wangu!

Jane said...

Nakubaliana na jamaa yangu aliyetangulia hapo juu, M3 kweli wewe ni tajiri basi tu ni milango hajafunguka lakini nasema kwa jina la yesu na ikapate kufunguka sasa. Sasa Doctor mbona nyumba haieleweki???? sema tu kwa vile na we mbishi ningekushauri uachane nayo lakini fuata nini moyo wako unasema maana tulipewa uwezo wa kukanyanga ng'e na nyoka so naamini nawe unaweza ukidhamilia. Kazi nzuri M3. Barikiwa.

Yasinta Ngonyani said...

Haki ya mungu Dakitari huyu ana imani na sio ndogo, Sasa umekatasha pamu bwana wewe leta utamu huo na MMM kipaji unacho HONGERA.

Candy1 said...

Enhe enhe!!! Tuone kama mganga atajiganga...hahaha Kiswahili!