Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, February 26, 2010

Imekula kwetu

 ‘Ondekeni wote upande huu, sogeeni kule…’ amri zilikuwa zikitolewa mara kwa mara, na watu bila kubisha waliondoka huku, wakasogea pale, na kila mara amri hizo zikitolewa, mheshimiwa hakimu, mtu aliyevaa suti kali na juu ya hiyo suti kavalia joho lenye mistari mekundu hupita na kuingia chumba cha mahakama.Hapa ni mahakama ya kazi, na kweli kulikuwa na kazi, kwani watu walivyojaa, ilionyesha kweli kuna kazi ya ziada. Hali hii ya kuinuliwa iliendelea mara kwa mara hadi muda wa kesi yetu ulipofika. Tukajikongoja hadi ndani ya mahakama, na kuwakuta watu wengi wakiwa wamekalia mabenchi na wengine wakiwa wamesimama, wote hawa walikuja kusikiliza maamuzi ya kesi zao. Kiroho pupa!


Nilijaribu kupitisha macho yangu huku na huko nikiwaangalia watu mbalimbali waliokuwemo humo ndani, wengi walikuwa wamechoka, na kuchakaa. Kuchoka huko na kuchakaa sio kwasababu ya umri, yawezekana ikawa hivyo kwa baadhi yao, lakini dhahiri,ilionyesha kuwa ni sababu ya hali ngumu za kimaisha. Wewe fikiria kwa mfano kesi yetu inakaribia miaka kumi inapigwa tarehe, na mtu kama huyo awe anasota na maisha ya mitaani, akihangaika na hili au lile bila ajira maalumu, atakuwa katika hali gani! Fikiria hela gani aliyolipwa na muajiri ambayo angeanzishia hata kigenge cha nyanya, hela hiyo ni kama tiketi ya kumsaidia kurahisisha kifo chake. Ni lazima atachakaa hata kabla ya umri wake.

‘Kesi namba kadhaa, ya mwajiri(jina) na mfanyakazi (marehemu mwenyekiti wetu)akiwakilisha wafanyakazi wenzake 33..’ alianza hakimu, pamoja na mengine alisoma vipengele kadhaa, na kusema yeye atakachofanya ni kusoma hukumu, na sio kusoma mapitio yote ya kesi. Lakini kwa vipengele alivyovisoma ilionyesha wazi kuwa hakuna kitu. Nikatafakari na kuwaza juu ya wote waliokuwepo hapo nini hatima yao. Ukumbuke kuwa kila mmoja hapo amebeba sio familia yake tu, bali wapo tegemezi kibao, na huenda walichokuwa wakitegemea kama tonge la mwisho la maisha yao ni kupata chochote kwenye kesi hiyo, kwasababu kesi ilishaenda vizuri mwanzoni.

‘Hoja Ya wafanyakazi kuwa wamechelewesha kufikisha maombi yao ya kusikilizwa upya kesi ndani ya wakati haina miguu, kwa sababu wao wanauzoefu kwa vile kesi yao imeshasikilizwa mara nyingi, kwahiyo jopo la majaji limetuplia mbali maombi ya kesi hiyo…’ akasema hakimu na mengineyo. Wote tukaguna na kuinamisha kichwa chini, nahisi kwa muwakilishi wa muajiri aliyekuwepo pale mbele atakuwa akitabasamu, na kusema `imekula kwao hao, walie tu’

Kweli `imekula kwetu’ hatuna jinsi, tulijisemea kimoyomoyo na kuinuka kwenye yale mabenchi, na baadaye tuliamua kumwendea katibu wa chama cha wafanyakazi. Yeye alisikitika na kusema hata yeye ameona ajabu kwanini katika siku 45, wakili wetu wakati huo hakuweza kupeleka maombi yetu mahakamani! Nakupunguka kipindi hicho wakili huyo alikuwa akidai kuwa kabanwa na kazi nyingi, mara kasafiri na hatimaye siku zikapita! Je tumlaumu nani, na baya zaidi wakili huyo hatupo naye duniani. Chakusema kwasasa ni kuwa kesi imekula kwetu.

Wakati tunatoka kuelekea kwa katibu nikamkumbuka mwenyekiti wetu, kuwa kwa muda kama huu tungelikuwa naye, lakini sasa ni marehemu.Nilimkumbuka jinsi gani alivyokuwa akihangaika na kujituma kuifuatilia hii kesi yetu. Hadi hatua za mwisho, akiwa amechoka, amekonda na maisha yakiwa magumu kwake na kwetu, lakini aliweza kuja kwetu kutupa moyo. Huyu ndiye kiongozi shujaa, kiongozi aliyejali matakwa ya wenzake, hata kama yeye alikuwa akiumia, Alijua wazi kuwa hakuwa akiwatetea wafanyakazi wenzake tu, bali alikuwa akiwatetea wao na walio nyuma yao. Mungu amlaze mahala pema peponi , na wengine waliotangulia mbele za haki, kwani sio yeye tu, wapo wafanyakazi wengine wameshafariki, na kushindwa kabisa kuipata haki yao ambayo imeshaota mbawa.

Kwa muajiri kwake ni kicheko, kwani nakumbuka siku wanatugaia barua zetu, wakati tumegoma kukubaliana na matakwa yao, yenye masharti ya kututega, alituaga kwa kebehi kuwa, hata kama tutashitaki, lakini hatutamuweza. Alisema kesi kama hiyo kwa uzoefu wake itachukua muda mrefu na hiyo ni faida kwao, kwani hata kama tungeshinda, hiyo hela itakuwa imeshazalisha na kufidia hiyo ‘hasara’, lakini aliendelea kusema kuwa `Kwa uzoefu wake ni nadra kwa wafanyakazi kushinda. Simtaona, fikiria mkikaa zaidi ya mika mitano nyumbani mtapata wapi hela za kumlipa wakili, mtakuwa mumeshaishiwa…kwaherini ‘ alisema.

Swala la kujiuliza je ili wafanyakazi waweze kupata haki zao vyema ifanyike nini? Je mikataba ya ajira, ambayo baaaye huja kuvunjwa na waajiri, ina maana gani, kwani hatima ya siku kwao hubakia kicheko cha dharau! Ni nani wa kuwalinda wafanyakazi wan chi ambao kila siku huangukia pua kwa kukubali mikataba yenye mitego, inayotungwa na waajiri. Rejea maelezo yetu ya utumwa wa nguvu kazi


Vipo vyama vya wafanyakazi, lakini nguvu zao huwa pale mkiwa bado waajiriwa, mnapokuwa nje ya kazi, nguvu yao huwa ndogo, ingawaje bado wana haki ya kuwatetea, lakini asiyekuwepo na lake halipo. Tukumbuke pia wao kama vyama vya kutetea wafanyakazi wana matatizo mengi ya wafanyakazi na sheria za ajira hazipo wazi, kwani wa-ajiri, na wenye makampuni mara nyingi huwa hawakubaliani na vyama vya wafanyakazi, na wengine huvipinga waziwazi. Hata wakikubaliana navyo bado yeye kama muajiri ana nguvu ya ziada, pesa. Pesa huongea na pesa inarahisisha mambo ya kufuatilia. Hata kama una haki kama huna pesa, utaipata haki yako kweli? Kuna gharama za usafiri, gharama za makabrasha, nk.

Kwa ujumla, kama muajiri akikutema, iwe ni kwa haki au kwa batili ujue wewe mfanyakazi huna chako, utaambulia mshahara mmoja, na kusubiri `enisisiefu' yako, na ukijitia unajua sana ukafungua kesi hatima yake,ndiyo hiyo `imekula kwako'.

From miram3

1 comment :

Anonymous said...

Sie nyie tu, hata sisi wa Taa ya Nescori!