Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, December 14, 2009

Tutakwenda wengi

‘Tutakwenda wengi’ huu ni usemi ambao alipenda kuusema rafiki yangu mmoja tukiwa tunafanya kazi sote sehemu za bandarini. Usemi huu ulitamkwa tena na jamaa mmoja tukiwa kwenye mazishi ya kijana mmoja ambaye alioa karibuni tu, hutaamini ndoa yao ilikuwa haijafikisha hata miezi sita.


Katiba msiba huo fununu na minong’ono iliyokuwepo ni kuwa kijana huyo alikuwa ameondoka na sababu kifo chake ni ugonjwa unaojulikana sana. Cha ajabu kijana yule hakuwa na dalili mbaya sana, na afya yake ilikuwa ya kawaida tu, licha ya kuumwaumwa mara kwa mara.vipimo vyake vya mwisho vilionyesha kuwa kijana huyo alikuwa na ugonjwa huo siku nyingi, lakini yeye mwenyewe alikuwa hajijui. Siku zikifika lazima kuwe na sababu ya kuondokea.

Kilichohuzunisha wengi ni binti wa watu ambaye aliolewa toka kijijini, binti ambaye hakuwa na dosari za tabia mbaya. Hatuwezi kusema kuwa ugonjwa huo ni lazima upatikane kutokana na tabia mbaya, lakini ni pale moja anapokuwa nao akamwambukiza mwingine ambaye hana tabia yoyote inayomfanya aupate. Wapo ambao kwakeli zinaa kwao ni kama starehe zao, hawa wakiupata hatuwezi kushangaa, lakini binti kama yule ilikuwa sikitiko la kila mtu.

Ndoa ya vijana hawa ilikuwa ya kipekee, walifungia ndani ya mweli wakaenda kula fungate yao huko kisiwa cha marashi ya karafuu, waliporejea hawakukaa muda wakanda ndege kurejea Ulaya, sio tukabaki na gumzo la mitaani. Gumzo hilo lilitokana na binti huyo alivyoolewa na kumuacha mpenzi wake ambaye walishafikia hadi uchumba na posa ilikuwa njiani, lakini siku mshenga alipopeleka mahari akakutana na taarifa kuwa binti ameondoka kwenda Dar, na huko anatarajia kuolewa na kijana wa mzito fulani.

Rafiki yake huyo alipopewa taarifa akaanguka na tangu siku hiyo akawa haongei na watu , hali na baya zaidi akawa amejenga uahasama na mabinti wote wa pale kijijini kuwa wanawake sio waaminifu.

Kijana wetu toka Marekani, alisomea Ulaya na baadaye akawa anafanya kazi Marekani, alirejea likizo na kukutana na wazazi wake, ambao walimshauri aoe mtoto wa Kitanzania, kuliko kuoa wazungu aliowazoea. Kijana hakuwa na pingamizi akawaambia wazazi wake kwavile hana rafiki yoyote wa kike hapa nchini angeomba wazazi wake wamtafutie. Hili likawa ndio lengo la wazazi na kama ujuavyo wazazi wetu wa siku nyingi wakitaka kumuoaza kijana wao hupekua nasaba ya binti, tabia na kuangalia kuwa hakuna magonjwa ya kurithi ili mwana wao apate mwenza wa uhakika.

Walipofika kijijini kwao wakasikia sifa ya binti mrembo ambaye amekataa posa za matajiri wengi, ingawaje inasadikika kuwa anarafiki yake aliyesoma naye ambaye huenda akamuoa. Wazazi wale hawakuchelewa wakawaendea wazazi wa yule binti, na kwa vile familia hizi zilikuwa zikijuana pingamizi halikuwepo na kwavile binti anaolewa kwenye familia ya kitajiri, basi ikawa heri kwao na kubwa ziadi binti yao anaolewa na msomi wan chi za nje, msomi wa Ulaya na Marekani, msomi ambaye pia anafanya kazi nchi za nchi.

Binti akapewa taarifa na aliposikia sifa za familia yenyewe na kijana anayetaka kumuoa, akawa kabisa amemsahau rafiki yake ambaye walishapeana ahadi za kuoana pindi. Hata hivyo hakujali kwasababu uchumba wao ulikuwa haujafika kwa wazazi wa pande zote , akaona hilo kwake sio pingamizi, kinachotakiwa ni kumjua huyu kijana mpya toka Ulaya. Na kweli alipomuona akagwaya, huyo ndiyo kijana aliyemtaka, mtanashati, msomi, na tajiri.

Ndoa ikapangwa na harusi ikafanyika. Baada ya miezi kadhaa tukasikia wanandoa hawa wamerejea, na wanafanya kazi hapa nchini. Lakini fununu zikaenea kuwa kijana mwanaume hali ya afya yake sio nzuri sana, kwani haishi kuumwa umwa. Unajua tena wabongo kwa uzushi wengi hatukujali fununu hizi , kwani wao ni nani wasiumwe, hata kama wametokea Ulaya, lakini mwili ni mwili tu.

Ghafla taarifa zikajakuwa kijana katutoka. Hamna jinsi Mola ndiye muumba na ndiye mwenye mamlaka yake.

`Jamani sasa hivi , hali ilivyo, `tutakwenda wengi’ jamaa mmoja akawa anatupa za leo-leo, na ni mmoja kutoka katika familia ya wafiwa. Kijana wetu hatukujua kabisa kuwa anaumwa huu ugonjwa, hata yeye mwenyewe alikuwa hajijui., Ukimuona alivyo `handsome’, pesa, kisomo, ni nani angemkataa’ aliendelea kusema.

‘Lakini hili liwe somo kwetu kuwa ni vyema kabla ya ndoa wanandoa wote wapimwe kwanza kuangalia afya zao, kwasababu hivi sasa ukimwi hauna dalili mbaya kama zamani. Inatakiwa wafungaji ndoa wahakikishe kuwa wanandoa wanakuja na vipimo vya afya zao kabla hawajafungisha ndoa, ili kutokuwepo na maambukizi’ mmoja aliongezea.

‘Kweli tusipoangalia tutakwenda wengi’ mwingine akasema.

From miram3

1 comment :

Anonymous said...

Mimi nashangaa mtaoanaje bila kupima, lakini tatizo watu wanapimana kabla ya kuoana, sasa wapime nini tena