Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Sunday, December 27, 2009

Tujiheshimu maofisini

Ilikuwa siku yangu ya kwanza, na nilitakiwa kuonana na bwana mkubwa wa kampuni moja ya mtu binafsi. Kama kawaida unapofika sehemu ngeni unajikuta mtu wa kushangaa kila unachokiona ingawaje huenda ulishakutana nacho kabla. Lakini nilichokiona pale kilikuwa kigeni kwangu, kwani huko nilikotoka kuingia ofisi kama hizi za bwana mkubwa ilikuwa ni nadra, kwahiyo yaliyokuwa yakitendeka huko siwezi kuthibitisha kuwa ilikuwa sawa na hhayo niliyoyaona kwenye ofisi hii mpya.


Nilipoingia kwenye ile ofisi nilikaribishwa kiti halafu nikaulizwa kuwa nahitaji chai au kahawa, kwa kujivunga nikasema angalau maji inatosha. Simu ikainuliwa na mara mlango ukafungulia, binti mmoja mrembo niliyekutana naye kabla akaingia akiwa na sinia ndani yake kuna kahawa ya bwana mkubwa na glasi ya maji. Yule binti akatugawia vilivyomo halafu akasogea kule alipokuwa amekaa bwana mkubwa ili kuchukua faili ambalo alihitajika kulipeleka kunakohusika.

Binti yule wakati anasikiliza maagiza ya bwana mkubwa yule, alikuwa amesimama nyuma ya kiti chake, cha ajabu nilichoona ni kuwa binti yule bila kunijali mimi kama mgeni kwa muda ule, alikuwa akimchezea bwana mkubwa yule kwa mikono yake, mkono wake ukawa unamkandakanda yule bwana mkubwa kwenye mabega huku na kule, na hata kuosogeza kifuani , kichwani eeeh, jamani ! Hapa mimi nilishindwa kujizuia nikajikuta ninaguna, na ule mguno ukasikika kwa bwana mkubwa yule, akaniuliza

`Vipi mbona unaguna, kuna la ajabu hapa?’ akauliza kwa mzaha huku anacheka na yeye akiupapasa ule mkono wa binti!

‘Hapana, ila nilikuwa nasafisha koo, na nilipoitazama pete yako ya ndoa nikaiona ni mpya kidogo, umeoa karibuni nini!’ nikasema kiutani

‘Kwani pete ya ndoa ina maana gani ndani ya ofisi, siku hizi, mkeo ni nyumbani, ukiwa ofisini sahau ya mkeo’ maneno yakamtoka yule binti na kuniacha hoi hasa hilo neno, `mkeo ni nyumbani’

‘Ukiolewa utajua umuhimu wa pete ya ndoa’ akasema yule bwana mkubwa huku akijiweka saw kuongea na mimi.

Yule binti akabetua mdomo na kujibaragua huku akilichukua lile faili na alipofika mlangoni akagusa mdomo wake kwa kidole na kumuonyeshea yule bosi kama vile anambusu kwa mbali. Nikajikuta ninacheka , na yule bosi akacheka kwa dharau. Baadae akasema kuwa hii ndio hali ya ofisi zatu, nisione ajabu.

‘Wakati mwingine inasaidia kuondoa uchomvu wa kazi ukiwa na mabinti kama hawo ambao wanajua kuwapetipeti mabosi wao, fikria masaa mengi upo ofisini ni wapi utakutana na mkeo, ni mpaka usiku, sasa…ok, tuendelee’ akasem yule bosi.

Baade nilitoka mle ofisini na wakati napita mezani mwa yule binti nilimkuta amekaa kinamna ambayo nguo zake za ndani zilikuwa zinaonakena, nikaguna ili ashituke ajirekebishe, na badala yake akajifanya hakusikia na kupandisha mguu juu kama vile anakuna vidole vyake vya mguu, sikuamini macho yangu nikabaki mdomo wazi. Hizi ndizo hali zetu za kiofisi kweli, haya ndio maadili mema ya ofisini, au ni tabia ya mtu mwenyewe!

Wafanyakazi wengi muda wao mwingi wanautumia ndani ya maofisini kuliko majumbani mwao, na hali hii inawafanya wazoeane kuliko hata wanavyozoeana na familia zao. Wengine kwa uzaifu wao wa kibinadamu wanavuka mipaka na kuanzisha mahusiano yasiyo rasmi ndani ya maofisini. Hali hii imefanya maumbukizi mengi ya ukimwi yasambae na baya zaidi yavuka mpaka kutoka maofisni na kwenda kwenye majumba yetu!

Swali langu likawa ni kwanini wengine wanavuka mpaka na kuwa vishawishi vya ngono? Je hali hii haivunji heshima kwao? Nasema hivi kwasababu nguo na mikao inayoonekana ndani ya maofisini mwetu inakuwa ni moja ya vyanzo vya ushawishi kama kweli tutakuwa wakweli. Na ukizingatia kuwa wakati mwingine kunaandaliwa tafrija, ambazo ndani yake kunakuwa na vilevi. Kuzoeana kukichanganyika na vishawishi hivi, vya mikao ya hasara, kutaniana, kushikanashikana vinakwenda mbali zaidi ya hapa. Pia vishawishi vya ubosi na ushindani wa mimi nionekane bora vinaingilia kati na hatimaye usaliti wa ndoa na urafiki usio rasmi hujengeka, na matokeo yake ni maambukizi ya ukimwi.

Ninawaoea huruma sana wale akina mama wa watu walio-olewa na kujikuta wanaambukizwa magonjwa na waume zao au hata akina baba ambao ni waaminifu wanakuta wanambukizwa magonjwa na wake zao ambao wamejenga mahusiono yasiyo rasmi kwenye maofisi. Na tumeshuhudia uadui unaojijenga kati ya bosi na wafanyakazi wake kwasababu ya ushindani wa mapenzi. Na hali hii imewafanya wengie hata kupoteza ajira zao, au kusingiziwa mambo yasiyo ya kweli kwasababu ya shindani wa mapenzi!

Tabia ya kila mtu ni mtu mwenyewe, lakini zipo sababu nyingine zinaweza zikamfanya mtu akaingiwa na ibilisi na kujikuta anafanya kile ambacho sio tabia yake, na mojawapo ni hiyo ya kutojiheshimu ndani ya maofisi yetu. Kwani kuna ubaya gani kuvaa kiheshima ndani ya ofisini na kama mna mahusiano yenu basi kayafanyeni nje ya ofisi baadae. Tujue ofisini tunakutana tu, lakini undani wa kila mmoja wetu tunaweza tusiujue vyema, na hili ndilo la kuangali zaidi, kwani wengine wanafanya hivyo ili kutimiza dhamira fulani, tusipoangalia tunaweza tukajikuta tunajianika wenyewe juani, wakati wenzako wanaenda baadae wanachumia kivulini.

From miram3

1 comment :

Anonymous said...

Hata mimi nilitembelea ofisi moja nikakuta binti amekaa, suruali nyuma imeshuka, na kifuani kavaa kifulana kinachoweka maziwa asilimia kubwa wazi, sijui lengo lao ni nini jamani