Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, July 4, 2016

Toba ya kweli (kutoka ndani ya shajara yangu)


‘Rafiki yangu, mwezi mtukufu ndio unaisha,...na kiukweli nimejitahidi Ramadhani ya mwaka huu kutimiza karibu kila kitu...leo....'aliniambia rafiki yangu.

'Hongera sana...mashallah...'nikamwambia.

'Unajua ..., nikiwazia hilo, nimekumbuka maisha yangu yaliyopita, ni mwaka jana tu, wakati mwaka ulipokwisha nilifanya jambo baya sana, , ....'alianza kuongea rafiki yangu akiwa kashika shavu hana raha.

'Ndio ndio..nakumbuka mwaka jana uliumwa sana, ukawa kama umechanganyikiwa kwani ilikuwaje...?' nikamuuliza

'Unajua ilikuwa ni siri yangu,kuba sana....'akatulia kwanza

'Lakini sasa naona sio siri tena, japokuwa nimechelewa..'akasema  na mimi nikatulia nikimsikilizia.

'Unajua mwaka jana,  niliamua kujitakasa kweli, kwani maisha yangu yalijaa machafu mengi, utajiri niliokuwa nao haukuwa wa halali, maisha niliyokuwa nikiishi yalijaa dhambi nyingi sana..japokuwa niliweza kuwa tajiri.

Lakini nikuambie kitu, sio matajiri wote wana raha...mimi ni mmojawapo...unajua, ikafika muda nikasema hapana hii sio njia sahihi...nahisi nahitajika kufanya jmbo.’ Jamaa yangu akasema, nikaona nimsubiri aelezee alichokikusudia, lakini akabakia kimia akiwa kashika shavu, na mimi nikaona asiniache hewani nikamwambia.


‘Ni vizuri kama uliamua hivyo, na ulifanya jambo la hekima sana,  na wote ina bidi tuwe na moyo kama wako’ nilimuunga mkono. Aliniangalia kwa muda, kiasi kwamba nilijiuliza ni kipi kibaya nimekitamka. Aligeukia upande wa dirishani kama vile anakwepa kuniangalia machoni

‘Rafiki yangu sio rahisi kihivyo...haikuwa jambo rahisi kama unavyofikiria wewe...kujitakasa, sio kazi rahisi , asikudanganye mtu. Nafsi ina nguvu sana mwilini kwetu....Kwani nilipoamua kufanya hivyo nilikwenda kwa mtu wa imani ninayemuamini sana, nikamuuliza, mkuu wa imani, niambie ili niwe msafi, ili nitubu madhambi yangu, nifanyeje...

'Akaniambia kama ninataka kutubu ukweli, toba ya kweli mungu yupo karibu nasi kuliko kitu kingine, na mola hupokea toba zetu wakati wowote..ninachotakiwa ni kumlilia yeye atanisamehe...' mimi nikamwambia kama ni hilo tu, basi mimi nitamlilia sana,  haina shida. Lakini akaendelea kuniambia, sio hivyo tu kuna madhambi ambayo niliwatendea wenzangu, inabidi hayo sasa , niwaendee wahusika, niwaombe msamaha, niwarejeshee mali zao niliowadhulumu..'akaniambia.

'Mhh, mkuu hilo litakuwa gumu kidogo...'nikasema

'Wewe si unataka kutubu,...madhambi uliyomtendea mola wako atakusamehe kwa upande wake, lakini kuna mja wake uliyemdhulumu, ukamuibia ukamfanyia mabaya, je atajuaje kuwa wewe ndiye uliyemfanyia hivyo,ili akusamehe... je hiyo dhuluma ambayo ni kama donda kwake, itaponaje....'akasema

'Sasa nifanyeje...?' nikamuuliza na yeye akasema

'Kiukweli kuna makosa tunayafahamu kabisa, tulifanya hiki na kile kwa yule na yule, basi muhimu ni wewe uende kwa huyo mtu ukamuombe msamaha, mueleze ukweli ulivyokuwa, na kwa vile nia yako ni njema, atakusamehe tu..ama kwa yale ambayo hatukumbuki, mungu mwenyewe anajua....'akaniambia

Unajua kwa vile niliumwa sana, na dawa peke niliyoambia , ya kuweza kupona maradhi yangu ilikuwa ni toba...angalu hata nipate mtoto.... , basi nikaanza mikakati hiyo ya kutubu, lakini haikuwa kazi rahisi  kutegemeana na makosa yenyewe, lakini nilijitahidi sana, yale ninayoyakumbuka niliyafuatilia, na kuwafuatilia wahusika....

'Sasa basi, kuna mmoja wa niliyemkosea..huyu ilikuwa vigumu sana kwangu kumwambia na kutubia mbele yake, ..na huyu mtu hutaamini nilikuwa ninalala naye ninaishi naye kila siku..’ Alinigeukia na kunikazia macho, na macho yake yakaanza kulengalenga machozi.

‘Ni nani huyo, mkeo au jirani au mwanao, au, una maana gani’ nilianza kuhisi vibaya, nikijua kuna baya alimfanyia mkewe au hata mtoto wake.

 Alitabasamu na kuangalia pembeni kama awali.

‘Kazi ya kutubu imenichukua mwezi mzima, na kweli nilizamiria nihakikishe nimekamilisha hili, kwasababu nimesota, nimeteseka sana. Magonjwa shida na taabu vilinipeleka kuamini kuwa madhambi yangu ndio chanzo cha yote’ Alisema na hapa nilimuunga mkono kwasababu wengine wangekimbilia kwenye imani za kishirikina na kuteketea zaidi, lakini mwenzetu huyu imani yake imemtuma vyema nilikaa vizuri kusikiliza.

‘Siku nilipoamua kutubia niliamua kwelikweli, nikarejesha mali nilizozipata kiharamu, nikawatembelea wale wote niliowakosea , nikafanya mengi mengi, lakini kila nikilala nilikuwa nikiteseka kuwa kuna dhambi kubwa niliitenda ambayo inahitaji kutubia kwa hali ya juu. ..'akatulia kidogo.

'Utashangaa wengi niliwakosea ilibidi hata kusafiri kuwafuta..., lakini huyu wa karibu yangu, yupo nami kila siku nilishindwa kumwendea, japokuwa  tupo naye tunalala naye lakini nilimuona kama yupo maili nyingi ajabu’ alisema huku kama anacheka lakini uso wake ulionyesha umakini wa anachokiongea.

‘Siku moja nikaamua,  ...'akatulia

'Ooo mke wangu, kuna jambo nataka tuongee faragha....'akatulia

'Ni kweli mke wangu akafika tukaa naye, nikaanza kumuelekezea, alishajua nafanya nini, lakini kwa hili naona hakulitarajia...'akatulia

' Nilimuelezea mke wangu kwa kirefu nini kusudi langu, na yeye ilionekana kunishangaa na kuniona kuwa labda nakaribia kukata roho, lakini nikampa moyo kuwa sio hivyo, ila nimeona kuwa ili tuondakane na taabu tulizo nazo, kuumwa, shida....na anagalau tupate mtoto, hata mmoja, ni vyema nitubu hayo madhambi, na mimi ninahitaji toba, toba ya kweli.

Kiukweli mke wangu alikuwa mcha mungu maana hata yeye hayo yalikuwa yakimuuliza miaka kumi sasaupo naye na hatujajaliwa kupata mtoto, mali tulikuwa nayo lakini hatukuwa na raha nayo, ....unajua,..mali ninayo lakini siwezi kuitumia, nina kisukari, nina presha,....ugonjwa wa moyo...nitaitumiaje hiyo mali, naiangalia tu...'akasema

'Kwakweli Mke wangu akanielewa, na kusema ni sawa, ninavyofanya naye ataniunga mkono..'akatulia , na alitulia hivyo ,ikachukua muda kidogo rafiki huyo kuendelea na stori yake....

Baadaye ghafla akanigeukia na kuanza kuongea sasa akiwa kama ananinong’oneza

'Mke wangu, kote nimeshajitahidi kutubu, karibu wote ninaowakumbuka niliowatendea mabayanimewaomba msamaha, na wale wakuwarejeshea mali zao nimefanya hivyo,..mali hazina thamani kwetu, zipo, si unaona mwenyewe, hatuna raha kabisa...kwahiyo sikuona ugumu wa kuzitoa hizo mali...'nikamuelezea mke wangu

‘Lakini kuna tatizo moja,....pamoja na kuishi vyema kwetu mimi na wewe , nakiri kwako, kuwa kuna mabaya nilikukosea. nataka kutubu mbele yako...'nikasema na mke wangu akashutuka, na kuniuliza

'Yapi hayo mume wangu, maana siku zote tunaishi vyema, umenietendea mema mengi kama mume wangu, ..mimi nakuamini kabisa....'akasema mke wangu

'Nilianza kumuelezea mke wangu maovu niliyomfanyia yeye....'akatulia

'Unajua ni maovu gani niliyomtendea mke wangu...?’ akaniuliza, na kabla sijamjibu akawa anaendelea na maongezi yake.

 ‘ Ovu kubwa kwa mkeo si kumwibia hela zake, ni kuvunja amri ya ndoa, au si ndio hivyo....'akasema na mimi nikatikisa kichwa

'Sikuweza kuzunguka huku na kule nikamuelezea kinagaubagaa kuwa mimi mumewe nilikuwa nikitembea na mdogo wake....na mke wangu alishituka na kukaa chini, aliposikia hivyo. nikaona hapo sasa  nimeua mtu kwa presha, lakini nikaona nimalize yote kuwa sio mdogo wake tu hata rafiki yake mpendwa , shoga yake mkuu, ambaye walikuwa rafiki pete na kidole..na mfanyakazii wa ndani, hapo mke wangu hakuweza kuvumilia akasema `stoop, please, stooop’

‘Nilipiga magoti mbele yake, nakumuomba anisamehe, kwani nataka kuwa msafi na sitarejea tena madhambi yangu. Mke wangu alitulia kimya na baadaye akatamka neno ambalo sikulitegemea kwa muda ule...unajua alisema nini....?' akaniuliza na mimi nikakaa kimia,

Rafiki yangu akaendelea kusema;

 `Alisema kuwa kanisamehe ...nimekusamehe mume wangu, na naomba tusahau yaliyopita na tuwe pamoja, lakini na mimi pia nataka kutubia kwako...’akasema mke wangu.

`Kweli eeh mke wangu mbona itakuwa jambo jema’ nilimuambia mke wangu nikiwa na furaha tele moyoni, na. Mke wangu kwanza akaanza kulia, baadaye akatulia akasema;

'Mume wangu hili niliapa kuwa sitakuambia, niliona iwe siri ya moyo wangu, lakini kwa vile wewe umeanza, na kiukweli nimeona dhamira ya kweli moyoni mwako, ...sioni kwanini nisikuambie,..'akasema

'Niambie mke wangu, usiwe na shaka, mimi nitakusamehe, na huenda mola akatusaidia tukaondokana na mashaka haya..'nikamwambia...

Mke wangu akaniniuliza swali kwa mashaka,

'Je kweli una uhakika,..utaweza kunisamehe....?' nikamwambia kama yeye kanisamehe kwanini mimi nishindwe kufanya hivyo.

Basi akasema

'Mume wangu unakumbuka ile mimba iliyoharibika miaka kumi iliyopita,...?’ akaniambia

'Naikumbuka sana...ni mapenzi ya mungu ... naikumbuka sana, najua ilikuwa sio riziki yetu hayo tumuachie muumba...'. nikamjibu mke wangu

'Ni kweli na mimi nasema hivyo hivyo, hayo tumuachie muumba lakini tusimwachie hivihivi, bila ya toba ya kweli....'akasemma mke wangu na kuanza kulia na kunipigia magoti, huku akisema anaomba msamaha kwa kosa alilolifanya, na hapa nilibaki nimeduwaa, sikuelewa anamaanisha nini.

‘Mume wangu, ile mimba niliamua kuitoa baada ya kushindwa kuvumilia kwani damu ya rafiki yako ni kali kila mtoto aliyemzaa alikuwa kifanana na yeye..nilijua hata mimi nitakaye mzaa atakuwa akifanana na yeye...'akasema

'Unasema nini..?' nikamuuliza kwa mshangao, lakini kwa vile nilishasema nitamsamehe, nikajikausha na yeye akaendelea kusema

'Rafiki yako, anapendwa sana na wakina mama....na mimi shetani alinipanda, kwa vile ...nikaona nijaribu nione,..mtoto akizaliwa si wetu itakuwa siri yangu, kwanza tumekaa muda hatupati mtoto,...lakini bahati mbaya ilivyo, wenzangu waliotangulia kutembea naye, kila mtoto aliyezaliwa alikuwa anafanana naye...'akatulia

'Hadi hapa ninavyokuambia wenzangu watatu wameshatalikiw na waume zao, na wengine....mmh,..'akasita kuendelea na mimi nikasema kwa hasira

'Eti nini ni nani huyo shetani..?' nikamuuliza kwa hasira na mke akatoa macho ya kushangaa baada ya kuniona nilivyobadilika ghafla...lakini baadaye nikajirudi kujifanya nipo sawa, lakini moyoni we acha tu...

'Ni huyu  rafiki yako jirani yetu hapo, mwenye sura kama ya mzungu, unasikia sifa zake jinsi gani anavyotembea na wake za watu na kila aliyetembea naye kampa ujauzito na watoto waliozaliwa wanafanana naye kila kitu. ..'mke wangu aalianiambia sasa akijiamini

Hapo ndio nikaelewa kumbe Mke wangu aliamua kuitoa hiyo mimba wakati mimi nikijua ni mimba yangu na kipindi hicho tulihangaika sana na hiyo mimba, mke wangu alikuwa akiumwa usiku na mchana, siku alipoanza kuhisi ana mimba hadi lipotoka...basi ilipokaribia miezi kama minne, au mitano, tatizo likaanza

'Siki ile usiku,..nakumbuka  ilikuwa ni usiku, mke akazidiwa ikabidi tumpeleke mke wangu hospitali kumbe ni dawa aliyopewa ya kuharibu hiyo mimba, ilikuwa inafanya kazi, na tulipofika akawa anavuja damu sana, ...akaingizwa chumba cha wagonjwa mahututi, baada ya kitambo kidogo, docta akaniita na kuniambia

'Tumeweza kumuokoa mke wako lakini hatukuweza kumuokoa mtoto, mimba imeharibika..'akasema docta.

Basi mimi nilijipa moyo kuwa, kama mimba hiyo imeharibika basi mungu atajalia nyingine, lakini haikuwahi kutokea, miaka na miaka ikapita, lakini mimi sikukata tamaa nikajua ipo siku, ..sasa mke wangu ndio anasema

'Mume wangu unisamehe sana, maana katika kuharibika kwa ile mimba hata kizazi kiliharibika, docta alisema haikuwa na jinsi,....na hilo sikuwahi kukuambia,nilimuomba docta asikuambie,nikamuahidi pesa nyingi, na kweli akalificha kabisa hilo..'akasema,

'Ina maana wewe huna kizazi, ina maana hata yote haya ninayoyafanya ya kutubu hayatasaidia kitu, hatutaweza kupata mtoto nikasema kwa uchungu na hasira...' Kiukweli sikuweza kuvumilia nikaondoka hapo nyumbani, ..sikurejea siku hiyo, wala karibuni, niliishia kwenye nyumba yangu nyingine kwa mwezi mzima,....nikawa hivyo hivyo mwaka ukapita.

Nikawa sina mahusiano na mke wangu, sikuweza kuvumilia, sikuweza kumsamehe, akaanza kuumwa sikuweza hata kwenda kumuona....' hapoa akatulia kwa uchungu

'Unajua inaniuma sana...lakini hebu niambie mtu kama huyu ningewezaje kumsamehe hebu fikiria hapo, kuombeleza kwangu kote na toba zote hizo nia mojawapo ni ili mungu atujalie tupate mtoto, natupone maradhi hayo ya kisukari na presha... fikiria na huyu rafiki yetu tumfanye nini, maana amekuwa nyoka, lakini niliahidi siku nikikutana naye ama zangu ama zake nitamfanyia kitu kibaya, hatanisahau...'akasema akisikitika.

'Je uliwahi kumfanyia huichi kibaya,kwni hamkuwahi kukutana naye...?' nikamuuliza

'Mhh...alihama mji na sijui yupo wapi kwa sasa...'akasema

'Je mke wako,...ilikuwaje....?' nikamuuliza

'Mhh we acha tu.....'akasema, na mimi nikamuuliza;

‘Je rafiki yangu wewe ulipotubu kwa mkeo si mkeo yeye alikusamehe?’

‘Ndio lakini alinisamehe kwasababu labda kwa vile naye alikuwa na mabaya yake na alitafuta njia hiyo kuniambia...lakini sikuweza kumasamehe...sasa mwezi huu nilimlilia sana mungu anisamehe kwa hilo...maana nikiri nilifanya kosa kubwa sana...’ alisema kwa uchungu

'Basi hujachelewa nenda kamuomba msamaha...mrejeane...'nikasema

'Mhh, natamani ingelikuwa ni hivyo, lakini nimeshachelewa...'akasema

'Kwanini..?' nikamuuliza

'Mke wangu haypo tena duniani ....'alisema kwa masikitiko makubwa sana...

Ndugu zanguni,..hapa inatosha, nia ni kuufikisha huu ujumbe wa toba...ni kweli kuna madhambi mengi tumeyafanya, tumewafanyia wengine , na ndani ya mwezi huu tulitubia sana, hatukuwa tunaimba tu hizo duwa, najua zilitoka moyoni.

Kiukweli wengi wetu , tulitubia kwa mola, lakini sikumbuki, labda mimi sijui, wangapi walikwenda kwa wenzao waliowakosea wakawaomba msamaha, wakarejesha mali za watu.walizozidhulumu,....na wengine waliowakosea hawapo mbali kabisa na wao ni wanandoa wenzao....sijui labda wapo walitubua hivyo..labda, lakini mimi sijui...

Na ni ukweli usiopingika mwezi wa toba, mwenzi wa Baraka nyingi unakwisha, hebu tujaribu kujichuja mangapi mema tulifanya, mangapi tulitubia, na tukaapa kwenye kuitikia duwa za maombi yetu kuwa tumetubu ukweli wa kutubu kuwa hatutarejea tena, tukaomba maghafira, ....ili tuweze kuwa wacha mungu wa kweli..je tutafanya hivyo.

Labda wengi wetu tunaabudu tu kipindi cha Ramadhani, na mungu wetu yupo kipindi hiki tu cha RAMADHANI, haya ramadhani inaondoka,.turejee kwenye madhambi yetu,...inasikitisha sana, ..

‘Kwenye tukio hili, tumeona machungu ya toba, fikiria uchungu ulioupata ulipotendewa ubaya,, ulipoambiwa ukweli kuwa ulifanyia mabaya haya na haya...ujue kabisa uchungu huo upo kwe wenzako pia, uliowatendea ubaya, ... usione kuwa ni rahisi walivyokuambia kuwa wamekusamehe, imewauma kama ulivyoumia wewe. Basi kama kweli tumetubia, tukaomba masamaha, yabidi tukubali ukweli, na tuwe wepesi kusamehe...ili tusiumizane

Na hebu fikiria mola wetu tunamkosea mara ngapi, lakini yeye bado anatusamehe..

Tumuombe mola, toba tulizozifanya kwenye mwezi huu ziwe toba za kweli, na tumuombe mola, tusirejee kwenye machafu tena, kwenye madhambi tena, ....iwe ni shule kwetu na tuwe kwelii tumfuzu,....Oooh ,mola tumetubu na hatutajea tena kwenye maasi, ...Aaamin.

From miram3

1 comment :

Anonymous said...

Hiyo ni ngumu, fikiria mwenyewe, umetembea na mke wa mtu unaweza kwenda kumwambia mumewe. Kama unataka kifi sema, zingatia kuwa huenda jamaa hilo linatoka kanda ya ziwa