Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, December 3, 2009

Taaluma


 Sio kawaida yangu kukaa vijiweni, kwani vijiwe vinahitaji ushabiki, vijiwe vinahitaji waongeaji na kama sio muongeaji mzuri raha ya kijiwe hutaiona, labda uwe msikilizaji kama mimi. Kwenye kijiwe, mjadala hauhitaji ajenda au mwenyekiti, hoja huanzishwa na wakati mwingine inaweza hoja hiyo ikawa haina maana kabisa, lakini utatokea ubishi hadi wengine kukwidana mashati.


Wengine huita vijiwe ni sehemu ya kupotezea mawazo, wengine wanasema vijiwe ni kwa watu wasio na kazi, lakini wakati mwingine kunaweza kukazuka mjadala ambao unaweza ukasema hawa waliopo hapa ni wasomi, na usidanganyike ukafikiri wote wanakaa kijiweni hawana kazi, au shule haijapnda, wewe unaweza ukaumbuka na shule yako.

‘Hivi niwaulize wenzangu ni taaluma gani yenye soko hapa Tanzania, manake mwanangu anataka kwenda chuo kikuu, na karibu masomo yote kayafaulu?’ Hili lilikuwa swali la jamaa ambaye muda mwingi alikuwa ameinamisha kichwa akionekana mwingi wa mawazo.

Swali kama hili linapotolewa mara nyingi wa kwanza kujibu ni wale jamaa waongeaji saana, na majibu yao wengine yanaweza yakawa yakukatisha tamaa. Majibu yao yanakuja hata bila kufikiri, kwani mmoja wapo alijibu kwa haraka, ‘mwambia akasomee mambo ya siasa, huwaoni wanasiasa walivyonenepeana, manake huko kula kuko nje-nje’.

Jibu hili mimi nililichukulia vinginevyo, kwani akili yangu ikawa inatafakari zaidi, kuhusiana na elimu.Kwakweli, katika maisha yetu, elimu ni lazima na ni zaidi ya wajibu, ili uweze kupambanua mazingira yanakuzunguka. Elimu ni pana, na huwezi kusema mimi nimesoma kwahiyo najua kila kitu, haiwezekani.

Kwa minajili hii ndio maana wenzetu waliotumia muda wao mwingi katika kutafakari na kupambanua haya mazingira wakagundua utofauti, na utofauti huu ukawekwa katika nyanja ambazo tunaziita taaluma.

‘Mimi nakushauri mwanao akasomee udakitari, kwasababu kama mwanao ameweza kufaulu masomo yote, basi anaakili sana, na udakitari unahitaji watu wenye akili sana’Mjadala ukawa unaendela, na mimi kichwani nikaendeleza wimbi la kufikiri. Ni kweli hizi taaluma zinazidiana katika utashi wa kufikiri, wa akili kichwani? Kama ni hivyo basi kumbe kuna watu wenye akili nyingi na wengine akili zao ni ndogo. Sasa kama ni hivyo kwanini watu wapoteze muda kusoma vitu ambavyo pengine kwa akili zao hawataviweza? Na utagunduaje kuwa mimi au yule akili yake ni ya namna gani?‘Wewe bwana unachemsha, sio kweli kama Nyanja nyingine hazihitaji watu wenye akili nyingi, taaluma zote katika ulinganifu ni sawa, ila kwa akili za kibinadamu kila mmoja ana upendeleo wake na haya huja kutokana na ulivyolelewa, jinsi maeneo uliyoishi, au jinsi ulivyoona kipi kinalipa, na walimu gani uliokutana nao ukapenda masomo yao. Kwani kama taaluma nyingine hazihitaji akili kwanini huyo dakitari akashindwa kuwa mwanasiasa?’

Hoja hii ilinifanya nigeuka kumwangalia huyu aliyeitoa. Huyu alikuwa taksi dreva, ambaye alivalia suti yake safi na tai shingoni utafikiri yupo ofisini. Na hoja zikaendelea kutolewa, na mmojawapo akauliza kwanini basi nchi kama yetu kuna wasomo wengi, lakini pamoja na taaluma zao walizozisomea bado makampuni yanakufa, bado tu nchi yetu ni masikini bado tunaajiri wataalamu toka nje.

Mmojawapo akajibu akasema, hii inatokana na watu kuingilia taaluma ambazo huenda hawakauzisomea, au walizisoma tu ili kupata ajira. Akachukulia mfano wa taaluma ya uhasibu kuwa miaka ya nyuma ilikuwa ni taaluma adimu, na ukijiriwa kutokana na taaluma hiyo wewe umeukata, lakini sasa hivi kila mmoja ni mhasibu, hata yule ambaye hajausomea anaweza kujifanya anaujua. Hapa kwa vile ni taaluma yangu nikasogelea karibu nisikie zaidi.

‘Watu wengi wameingilia taaluma za watu hata bila kwenda shule, hata bila kuzisomea, ndio maana mambo mengi yanakwenda ndivyo sivyo na matokeo yake wale wanaoangalia matokeo ya taaluma hizi kwa mfanao waajiri wanafikia kuziponda baadhi ya vitengo katika maofisi yao na kuviona vitengo hivyo havina umuhimu, lakini sio kweli kama kampuni, kila kitengo kina umuhimu wake, kama zilivyo taaluma, kila taaluma ina umihimu wake, kinachotakiwa ni wao kuhakikisha vitengo hivyo vinashikwa na watu walioisomea taaluma hiyo, na sio kwa maneno ni kwa vitendo, na kila mtu afanyekazi kutokana na taaluma aliyoisomea .

 Siku hizi waongeaji ni wengi kuliko watendaji, na waongeaji sana ndio wanafanikiwa kwasababu ya midomo yao, ndio maana makampuni yanakufa, kwasababu watendaji wazuri hawapati nafasi, kwasababu kila mmoja ni muongeaji sasa ni nani atatenda. Na huyu mtendaji hawezi kuonekana kwasababu muda mwingi yupo katika kutenda yanayompasa katika taaluma yake, wakati wengine wanapoteza muda katika vikao, mijadala muda ambao sio muafaka.

Niliangalia saa yangu nikaona muda umekwenda sana, lakini niligundua kumbe vijiwe ni sehemu nzuri ya kupoteza muda na ikiwa hoja inayoongelewa unaipenda.

Wewe unasemaje ni ipi taaluma ina umuhimu kwa kijana wako ambaye masomo yote anayaweza, ili aweze kufaidika katika maisha yake ya baadaye?
From miram3

1 comment :

Anonymous said...

Mimi napenda mwanawangu awe raisi, sijui taaluma yake inaitwaje