Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, December 17, 2009

Siri si siri tena

Mjadala umezuka, kuhusiana na kupanda kwa nauli za mikoani kila inapofikia kipindi hiki cha December, kisa ni kuwa watu wengi wanasafiri kwenda makwao, shule zimefungwa na maofisi mengine pia hufungwa kwani matajiri wanaenda kutumia makwao.


Mjadala huu ulienda zaidi pale lilipozuka swala la baadhi ya wenzetu ambao huoa mke na kumwacha na wakwe zake huko mikoani na kuonana na mke huyo mwak kwa mwaka, na wengine hujitahidi miezi sita, sita. Swali likazuka hivi hii ndio kusudi la kuoana. Hapa akina mama wengi walipinga na kusema huu ni uonevu.

Akina baba walijitetea mtindo hasa wenzangu na mimi tunaotokea huko mikoa ya Kaskazini, kuwa unapooa, huwa unakabidhiwa kihamba chako, kina migomba, na ng’ombe wa kuwahudumia, sasa kutokana na hali za kimaisha, mtu unaona kuliko kutafuta mfanyakazi wa kuhudumia shamba na ng’ombe ambao ni muhimu kwa ajili ya mbolea ya migomba, na pia mtu wa kuwasaidia wazazi ndio maana kimakubaliano wengi huoana mke abakie na wazee ili wasaidiane na hilo.

‘Huo usemi wa kukubaliana haupo kabisa, kwasababu ukienda kuwauliza akina mama waliotelekezwa huko hakuna hata mmoja atakayekuambia kuwa aliwekwa kwenye hicho kikao akakubaliana kuwa akae na wazee hao, ila ni taratibu zenu mlizoziweka kuwa mke akiolewa kazi yake ni kuishi na wazee na kuhudumia shamba’ alijitetea mwanamke mmoja ambaye alisema anatokea maeneo ya huko.

Wakati mjadala huu unaendelea nikakumbuka kisa kimoja alichonihadithia babu, kilitokana na mjadala wa kutunza siri. Wengi walisema kuwa wanawake wengi hawawezi kutunza siri, kuliko wanaume, na hapa babu akatoa kisa kimoja kilichotokea kwa wanzetu hawa wanao-oa na kuwazuru wake zao mara moja kwa mwaka.

Mwanamama wa watu alijua ndio kawaida pale alipoagana na mume wake kuwa anakwenda Dar, kuhangaika na maisha, naye abakie na wazee na kuhudumia shamba la migomba. Ilimuuma kuwa hata fungate lilikuwa halijaisha, mume wake mpenzi anaondoka, lakini alikuwa hana jinsi waliagana na kuahidiana kuonana pindi.

Baada ya miezi kadhaa akawa anajisikia vibaya, akawa usiku anaona vitu kama manjozi na woga ukawa unamtanda akilini, kitu ambacho hakuwa nacho. Mwanzoni walizani kuwa labda ni dalili za ujauzito, lakini kumbe sio, kwani miezi ilipita bila kuonekana dalili za ujauzito. Hali hii ilimzidi kiasi kwamba akawa anapiga makelele usiku na ilibidi wazazi wafanye kazi ya ziada kuamuka kumsaidia.

Mwaka ukaisha na jamaa akaja nyumbani mwisho wa mwaka , alijitahidi akakaa mwezi mzima, na cha ajabu kipindi chote cha mwezi alichokuwepo haya matatizo hayakuonekana tena, kila mmoja akaona tatizo limekwisha. Mwezi ulipoisha jamaa akaaga, na mwanamama wa watu alikubali shingo upande aendelee na majukumu yake. Na bahati nzuri miezi kadhaa ikapita bila ya kuonekana lile tatizo tena.

Siku moja mwanamama wa watu alishituka usiku, na kujiona akitetemeka mwili mzima, akaanza kuhisi zile dalili za uwoga na kutingishwa kiajabu, akaanza kupiga mikelele. Mbaya zaidi nyumbani hapo walibakia yeye na baba mkwe, mama alikuwa amesafiri kwenda kwao kuhani msiba, na huko alitaraji kukaa wiki mbili. Ikawa mtihani kwa baba mkwe, hakuwa na jinsi ilibidi aamuke na kwenda kumsaidia mwanamama.

Hali hii ilitokea muda mbaya, na ilikuwa haikutarajiwa tena, kwani wengi walihisi hilo tatizo limekwisha, kwahiyo baba mkwe kwa uchomvu wa kazi za mchana kutwa alipooga alilala na shuka tu, na kelele alipozisikia mwamzoni alihisi ni mwizi, alitoka na shuka lake akachukua panga mbio kuelekea banda kubwa anapolala mkwewe. Na ghafula akavaana na mkwewe ambaye alikuwa akitoka .

mbio kukimbia, ikawa shike ni kushike, na ukumbuke pia mwanamama naye kwa uchomvu naye alalala na khanga moja, na kwa vile ilikuwa kipindi cha joto wengi hufanya hivyo.

Kukuru kakara za kumshika mwanamama zikapamba moto, kwani hali hii ikimtokea hukimbia kuelekea asipopajua, huwa kama amepagawa. Kukurukakara hizi, zilikuwa pevu hadi wote wakajikuta si shuka wala khanga zilizobakia mwilini, na hapo shetani akacheza karata yake ili kufanikisha lengo lake, kilichotokea ni aibu kusimulia. Ugonjwa uliisha na uukwe kwa muda huo ukaisha!

Baada ya mwezi hivi mume wa mwanamama akaja bila kutegemewa, na mwanamama aibu na fadhaa vilikuwa bado vimemtanda kichwani, akawa hana raha. Mume mtu aliiona ile hali ni lile tatizo la huo ugonjwa usiojulikana, akajaribu kumliwaza na kwa kipindi hicho mume wake alipokuwepo nyumbani na ucheshi wa mume wake ukamfanya asahau aibu aliyoifanya na baba mkwe wake.

Hali ya baba mkwe ilikuwa kama jinamizi, ilibidi atunge safari ya uongo na huko alikaa hadi mwanae alipoondoka kurejea Dar, na aliporudi alimkalisha kitako mwanamama, mkwewe na kumwambia anaomba sana iwe siri, `siuoliona mwenyewe, ni shetani alituingilia, mimi nilikuwa sina jinsi kama ulivyo wewe, naomba iwe siri’

Dalili za ujauzito zikaanza kuonekana kwa mwanamama, na hauchihauchi miezi tisa ikafika, na mtoto akazaliwa. Sura kama babu yake.

Katika hali ya kimisha, ikatokea kutokuelewana kwa wanandoa hawa, na kisa kilianza mke alipodai na yeye akaishi Dar, kwasababu kuna hisia kuwa mume wake ana kimada huko Dar, ugomvi ukazua matatizo mengina, ikafikia mwanamama kugoma kuhudumia shamba, akidai kazi zinakuwa nyingi, ahudumie mtoto, wazazi shamba hataweza, na jamaa kazi anayofanya hailipi kutafuta mfanyakazi. Jamaa ikabidi atumie rungu lake la uanaume, `kama hutaki ondoka kwenu’

‘Niende kwetu sio, ndio nitaondoka kwetu, siwezi kuwa mtumwa mie, wewe ustarehe na kimada wako huko Dar, mie ni mtumwa wa kazi , kwakweli siwezi tena’ Mke alijitetea

‘Nishakuambia kama huwezi njia ipo nyeupe, mimi kama nina kimada inakuhusu nini wewe’ Mume akaja juu ni kutoa kipigo.

‘Mimi sikubali, hivi wewe unanifikiriaje mimi, nikae huku mwaka mzima, nini maana ya ndoa..’ Mke alijitahidi kujitetea, lakini haikusaidia.

‘Wewe ni mtu wa huku shamba nimekuoa ili unisaidie kwa hili, kama huwezi sema, kwani wake wapo wengi…’

‘Sawa, kaoe hawo vimada wako, ndio maana mnazalishiwa na wakwe zenu, mtu mwenyewe huna kizazi, mpaka usaidiwe na baba yako, au hujui nini, mtoto huyo si wa kwako…’ maneno hayo yalimtoka mwanamama kwa hasira kasahau siri sierini, na kwa hasira akafungasha mizigo yake. Na jamaa aliposikia hivyo aliishiwa nguvu, hakuamini hayo maneno, mpaka alipofika kwa dakitari kupimwa na kweli alionekana ana matatizo ya uzazi, yanahitaji utibabu wa hali ya juu.

Kilichotokea ni siri, lakini siri ikawa imevuja, siri ikawa si siri tena. Halahala kwa wanandoa, jiulizeni nini hasa kusudio la ndoa. Tunakubali jukumu la wazee ni letu sote, lakini pia tuangalie kusudio hasa la kuoana ni nini. Hebu tulijadili hili kwa mapana.

From miram3

2 comments :

Anonymous said...

Pia busara haina tajiri wala masikini.

Anonymous said...

Ndoa zina mitihani yake, lakini wanaojua nini maana ya ndoa wanapeta tu