Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, June 9, 2015

HISTORIA HUJIRUDIA



‘Una watoto wangapi bwana mdogo?’ lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa rafiki yangu, ambaye kwa heshima nilimwita kaka, kwasababu wakati tunasoma wao walikuwa madarasa ya juu.


Nilitabasamu na kabla sijamjibu swali lake, alianza kulalamika kuhusu familia yake, akidai kuwa yeye amebahatika kupata watoto wane, kati ya hao ana mtoto wa kiume mmoja tu. ‘Hiyo yote ni neema ya mungu’ alisema. Kilichomkera kuhusiana na watoto wake ni kuwa na tabia ambayo hakupendezwa nayo.

‘Bwana mdogo, oa uzae, lakini usitegemee heri zote, mimi nimejitahidi kuwasomesha watoto wangu kwenye shule nzuri tu, lakini cha ajabu mabinti zangu wote wamenizalia nyumbani’ Alitingisha kichwa kwa huzuni. Nahisi tatizo hili limemkera sana, na kweli ni kero kwa wazazi wote, kwani kila mmoja anategemea watoto wake wapate elimu, wapate maisha bora na waume au wake bora, na sio kuzalia nyumbani. Utajisikiaje ukiona mtoto wako kapachikwa mimba, na huenda kapata ujauzito huo akiwa bado anasoma?

‘Huyu bwana mdogo wangu, yeye ndio ni mwanaume, lakini hata yeye nasikia ana mtoto nje, nasikia kampa binti wa watu mimba, na sasa anahangaika jinsi ya kutoa matunzo, kwasababu bado hajaweza kuishi na mke. Ataishije na mke wakati bado hajapata kazi ya maana!’ aliendelea kulalamika.

Mimi nilifikiria sana na kumbukumbu za huyu jamaa zilinirejea, kwani namkumbuka sana huyu jamaa ni kati ya wanafunzi, makaka zetu ambao waliitwa `viwembe’ walishapewa adhabu hata kuitiwa wazazi wao kwa tabia za utovu wa nidhamu, walishafumwa mitaani kwa kutembea na watoto wa walimu na watoto wa wafanyakazi wa shule.

Nikacheka kidogo, na kicheko kile hakikumfurahisha jamaa akakuja uso na kusema;

'Unacheka eeh, ngoja na wewe yakukute, na wewe si una zaa...'akasema na mimi nikaendelea kutabsamu na kusema;

‘Bro, unakumbuka enzi zako za shule, nasikia hata ulipoanza kazi, hukuacha ule utundu wako,...unakumbuka bro, kipindi ulipoadhibiwa mbele yetu kwa kutembea na mtoto wa mfanyakazi wa shule’ nilimuuliza kwa mzaha.

‘Achana na hayo bwana mdogo hiyo ni historia, nafikiri wengi tulipitia enzi hizo, lakini baadaye unajirekebisha...nilipooa nikatulia, ...japo mmm mara moja moja, si uajua bwana mdogo, wali wali kila siku...acha hayoo bwana mdogo...’

'Lakini nndugu yangu, mara nyingi haya mambo hujilipizia hapa hapa duniani, unavyofanya kwa wenzako ujue na wewe utafanyiwa hivyo hivyo....si unajua, hayo unayomfanyia mtoto au mke wa mwenzako, ujue yaamuumiza na yeye...sasa unafanyiwa wewe, unaonaje...'nikamwambia, akashika kichwa akasema

'Unajua nina haraka kidogo, kuna mtu nakwenda kukutana naye, tutaongea siku nyingine...'akasema

'Ni yule dada uliyenionyesha siku ile...?' nikamuuliza, akatabasamu, nikasema

'Yale, yale...kumbuka, muda mfupi ulikuwa unalalamika,...'nikasema

'Si unajua bwana....yule mmmh, lakini, naanza kutulia, nampenda sana mke wangu, ....tutaonana siku nyingine..'akasema , na huyoo, akaingia ndani ya gari lake na kuondoka, kwasababu nafikiri ukweli ulimgusa.

Kiuhalisia, historia hijurudia, na wengine husema maji hufuata mkondo. Wewe chunguza utagundua hili, na kama imetokea kinyume basi ni kudra za mwenyewe muumba. Chunguza watu na tabia zao za ujanani, kama walikuwa wahuni, wanaharibu watoto wa wenzao, ujue na wao hali hiyo italipizwa kwa watoto wao.

Jiulize mzazi wa mtoto uliyetembea naye na kumpa ujauzito alijisikiaje, je na wewe ukitendewa hivyo utajisikiaje? Au ni mkuki kwa nguruwe? Ubaya unalipwa kwa ubaya, ila kama utatubia ukweli wa kutubia huenda ukawa mmoja wa hao ambao wamejaliwa watoto wao wakawa tofauti na tabia zao za ujanani, shukuru sana. Lakini ni wangapi wanakumbuka hilo na kutubia, zaidi ni kujisifia, mimi enzi zangi nilikuwa mkali, hakatishi....

Nakumbuka yupo bosi mmoja ambaye kazi yake ilikuwa kutembea na wafanyakazi wake na alipendelea sana kuwaajiri mabinti wadogo, ilifikia hatua wafanyakazi wake(mabinti) wakawa wanamtania

'Bosi kwanini uvae nguo, wewe ukija ofisini chojoa nguo zako tu...'mfanyakazi mmoja akamtania

'Kwanini unasema hivyo, umekosa adabu siku hizi eeh...' bosi yule alishangaa na kumuuliza binti huyo aliyekuja kumuona ofisini mwake.

'Unajua bosi imeniuma sana, ina maana hata yule binto mdogo uliyemuajiri unatembea naye...'akasema huyo binti akionyesha wivu.

'We nini, nani kakudanganya hayo....'akasema huku akijabarugua kuangalia makaratasi yaliyopo mezani.

Yule mfanyakazi binti akamwambia

'Bosi kwakweli mimi nimekuwa mfanyakazi wako wa siku nyingi, nimekuvumilia sana...na mimi ni mpenzi wako wa siku nyingi, ...'akasema

'Sasa tatizo lako ni nini...?' akauliza bosi

'Siri zako zote nazifahamu, wewe karibu wafanyakazi wote wakike hapa ofisini umetembea nao, ni kweli si kweli...?' akamuuliza

'Sasa yote hayo ya nini, mshahaar nimekuongeza, wataka nini zaidi...?' akauliza

'Tabia hiyo sio nzuri, ndio maana nakuambia ni bora utembee uchi tu...huna haja ya kuvaa nguo...'akasema

'Hebu toka nje ya ofisi yanagu...'. Yule bosi  akamfukuza yule binti ofisini kwake. Alimfukuza kwasababu ukweli ulimchoma. Sasa mtu kama huyu watoto wake wakitendewa hivyo atalalamika? Mtenda naye hutendewa au sio.

Tukubali, na ndio ukweli, wema hauozi, na ukitenda wema utegemee heri njema, ingawaje wema malipo yake yapo mbali na si rahisi kuyaona haraka lakini wema katu hauozi. Na unapotenda wema, unatamani uje upate wema badili, na unaweza hata kukumbushia, lakini ubaya je...

Na ubaya haulipi, tenda uovu wako upewe majina na sifa za kila namna, lakini malipo yake ni dhambi na dhambi hizo utalipwa tu, na baya zaidi huenda malipo yake yakapitia kwenye kizazi chako, au uzeeni mwako.

Utauliza kwanini sasa atende mwingine na dhambi zilipiwe kwa mwingine, usisahahu kuwa wewe ulimtenda binti wa mwenzako na aliyeumia sana kwa muda huo ni mzazi wake sasa na wewe unatakiwa uone uchungu kama aliouona mzazi mwenzako.

 Historia hujirudia, chunguzeni nyendo zenu za wazazi wenu , jirani zenu mtagundua hili. Kama unatabia kama hiyo na unawapenda watoto wako, achana na tabia hizo chafu, jirudi na utubu ili upate kizazi chenye heri!

From miram3

1 comment :

Anonymous said...

Ni kweli ukizini na wewe utaziniwa, kama hutaki basi achana na mchezo huo, kwani ni lazima ufanye mzee, acha na kama huwezi oa, wawili watatu hata ukitaka wanne, kama una ubavu kweli