Katika kitabu nilichokuwa nakitunga nyuma kidogo kilianza hivi:
Ingawaje nilijitahidi kujizuia kama wasemavyo watu ‘jikaze kiume’, lakini akili na mawazo yangu yote hayakuweza kuhimili yale yaliyonisibu. Mawazo yangu yote yalikuwa yakitafakari tukio zima na jinsi lilivyotokea, yote ilikuwa kama ndoto. Licha ya kuwa kimwili nilionekana nipo, lakini akili na mwili havikuwepo. Nilijikuta nikishikwa begani na mikono iliyokakamaa na yenye nguvu huku sauti kali ya kiasikari ikiniamurisha nisimame.
`Nisimame niende wapi’ nilijiuliza akilini.
Nilijizoazoa huku nikichelea kudondoka kwa kosa nguvu za miguu, na bila kutegemea niligeuza kichwa upande ule wa wawatazamaji na macho yangu yalitua pale ilipokaa familia yangu. Nilijaribu kukodoa macho ili niwaone vizuri, kwani kiwingu kizito kilishaanza kutanda machoni. Wote walijaa simazi na kilichonigusa zaidi ni mtoto wangu mdogo ambaye alionekana akiniangalia bila kupepesa macho, sijui alikuwa akifikiria nini.
‘Twende hukuu wewe…’ Sauti iliamurisha na sikujua ‘huku’ ilikuwa na maana gani, kwani kilichoamuliwa pale mahakama hakikutua akilini, sikuwepo kifikira, lakini lakini hisia na nini kilichonileta hapo zilinituma kuwa kwa vile leo ilikuwa siku ya kusikiliza kama ninaweza kupewa dhamana au la, basi huenda dhamana imekataliwa. Ndivyo hali ilivyoonyesha na ndio habari zenyewe. Nilijua sio rahisi kupewa dhamana ingawaje ilikuwa ni haki yangu.
Nilijaribu kugeuza macho yangu tena ili niwaone wanafamilia lakini kilichokuwa mbele yangu ilikuwa uwingu wa wandishi wa habari wakichukua picha zangu, na wengine wakijaribu kuniuliza hili na lile, lakini sikuweza kuwajibu, nisingeweza kuwajibu kwani tukio zima lilitokea haraka na ili niweze kujieleza vyema ilihitaji muda wa kutafakari. Ilihitajika nguvu ya ziada kujitetea na nguvu ya ziada zaidi kuishawishi jamii inielewe kuwa yaliyotokea sivyo ilivyo.
Wakati natembea kutoka kwenye chumba cha mahakama, huku nikisindikizwa na askari wawili mawazo nayo yalianza kutafakari yote yaliyonikuta, huku nikiwa siamini kuwa hayo yote yalinisibu mimi.
NB Ni kisa cha kupambana na maisha,hasa unapotaka maisha yako yabadilike haraka kutoka hali duni kwenda matawi ya juu. Ili ufike kileleni kuna vikwazo, kuna njama, kuna uhalifu nk, na wengine huamua kutumia udhaifi wa wengine kudandia juu, na hawa ni wengi wa matajiri tulio nao . Vyovyote iwavyo, tajiri na utajiri wake,masikini na watoto wake, na yote tunayafanya, ya heri na dhuluma, hutendeka ndani ya maisha yetu,ndio maana tunasema, YOTE MAISHA.
From miram3
No comments :
Post a Comment