Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, September 25, 2009

Majukumu ya mke kwa mume

Ilikuwa saa nne asubuhi siku moja, sikuweza kwenda kazini, nikawa napitapita kuwaona majirani, niliona heri nimpitie jirani yangu mmoja, kwani huwa hatuonani mara kwa mara. Huwa maeneo ya kwetu tunaamuka asubuhi sana na kurudi usiku kwahiyo mnaweza mkakata hata mwezi hamjaonana na jirani yako. Mke wangu aliniambia jirani yako namuona siku hizi nyumbani naona huenda yupo likizo, nikamwambia itabidi leo nimpitie angalau kumpa salamu.

Nilifika kwake na kugonga geti mara nyingi bila jibu, nikahisi huenda kwasababu yupo mapumziko huenda bado amelala, nikaamua kuondoka lakini kabla sijafika mbali nikasikia geti likifunguliwa, nikarudi na kumkuta jirani yangu yupo mlangoni, alikuwa amevaa zile nguo wanazovaa wapishi mahotelini, na zilikuwa na uchafu wa masizi, na bado mikononi kulioneka maukoko na masizi mengi, nikajua mwenzangu kweli anawajibika.

`Oh jirani za siku tele,ulisafiri nini..' alianza kunisabahi huku akijaribu kujifutafuta na usoni alionyesha kutahayari kidogo.

`Nipo, siunajua tena huku kwetu, kuondoka usiku kurudi usiku' nilisema huku nikiangalia ndani kumtafuta mfanyakazi wao wa nyumbani au mkewe,lakini ilivyoonekana hawakuwepo au wanashughulika uwani. Aligundua natafuta nini , akanieleza kuwa mfanyakazi wao ameondoka na mkewe kaenda kazini, na watoto wameenda shule,kwahiyo yupo peke yake.

`Tunabana matumizi,manake nimepatwa na mtihani, mimi kibarua sina, nimekumbwa na gonjwa la `redundancy' na malipo yalikuwa sio mazuri, nimezunguka huku na huko kutafuta kazi sijafaulu. Bahati nzuri mke wangu anafanya kazi vinginevyo ningeadhirika. Kipato anachopata ni kidogo sana, sio kama mimi nilipokuwa napiga mzigo, sasa hatuwezi kumlipa mfanyakazi,watoto wanataka ada, sisi tunataka tule, kwahiyo na sisi tukaamua kupitisha redundancy kwa mfanyakazi wetu wa nyumbani, na ndugu wote waliokuwa wakitutegemea, lakini bado maisha ni magumu.

Alinieleza mengi, na mwishowe akafikia sehemu ambayo ilinifanya niandike hii habari hapa. Alisema, sasa hivi imembidi afanye kazi zote za nyumbani kwasababu mkewe inambidi aamuke saa kumi na moja kasoro ili awahi kibaruani, sasa majukumu yote ya ndani anaachiwa yeye, ikiwemo, kuhakikisha watoto wameandaliwa vizuri kwa ajili ya kwenda shule, ahakikshe amefanya usafi wa ndani, ikiwemo kupika,kufua, kuosha vyombo.

`Mwanzoni ilibidi nikonde, ilibidi wakati mwingine tugombane na mke wangu, kwasababu kazi zote hizo nilizoea ni kazi za wanawake, lakini siku zilivokwenda nikaona namtesa mke wangu,fikiria mwanzoni ilibidi aamuke saa kumi, ili afanye kazi za ndani ndipo aondoke,na hili likamfanya awe anachelewa kazini, nikaona hapa nisipogangamala, sote tutakuwa nyumbani na hapo kitakachofuatia ni talaka.

`Nikaanza kujizoeza kidogokidogo,kufagia,kufua, kazi ikawa kuosha vyombo,kazi ikawa kuwapikia watoto wakirudi shuleni, lakini baadaye niliona ni vitu vya kawaida. Unajua kazi zote ni kujizoeza,na majukumu haya sio lazima tuyagawe kuwa hili ni la kike au ni la kiume, kama ipo jinsi basi tunaweza kuyagawa hivyo, lakini ikifikia hatua kama hii yangu, bwanae, waache watu waseme, siri ya mtungi aijua kata...'

Hapa nilijikuta nikimpigia mwenzangu makofi, kwasababu nakumbuka kuna kipindi nilikuwa namsaidia mke wangu baadhi ya shughuli watu waakanza kusema huyo kapewa limbwata huyo anakaliwa na mkewe,kumbe sivyo hivyo,ukitafiti kiuandani sana utakuta wengi wetu tunasaidiana na wake zetu `kisiri' tukiogopa kuambiwa `mume bwege' lakini huu uume bwege unatoka wapi,ina maana wazungu wao ni waume bwege,mbona wao kazi zote wanasaidiana.

Inabidi tubadilike kutokana na maisha yanavyokwenda, na sie wenyewe tuangalie majukumu yaliyopo mbele yetu,kama yamewatinga, basi tugawane! Na tusione soo, kwani kazi zote zinafanyika kwa mume na mke, na pale inapobidi majukumu ya mke anaweza akayabeba mume au kinyume chake,na ikifikia hapo tusilalamike kwani mapenzi ya kweli ni kuhurumiana kwa kusaidiana.

Swali langu kwa wanajamii,je kama imetokea mume kakumbwa na gonjwa lililoletwa na wawekezaji la `ridandansi' na bahati nzuri mkeo anafanya kazi, je wewe mume unaweza ukayachukua yale majukumu yote aliyokuwa akifanya mkeo,ikiwemo ,kupika, kuosha vyomboa kufua na kuhakiksha kuwa usafi wote nyumbani upo kama alivyokuwa akifanya mkeo, na mkeo akirudi uhakikishe umempikia, umemwandalia maji ya kuoga nk? Kwasababu sasa wewe huna kazi kipato chako kinamtegemea mkeo, je majukumu haya kama mume anaweza kuyabeba kama alivyokuwa akiyabeba mke, na je mke anaweza kuhimili majukumu yote ya kulea familia nk,nk ? Tuwe wakweli na tutoe hoja za uhakika!

From miram3

No comments :