Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, September 22, 2009

Kumuenzi baba wa taifa

Leo tarehe 22nd September 2009, tukiwa ndani ya daladala kulizuka ubishi, wa jinsi ya kumuenzi baba wa taifa. Wengi walidai kuwa hiyo kauli ya `kumuenzi'sasa inatumika kibiashara au kisiasa zaidi, na sio ukweli wa kumuenzi. Mimi nikatafakari je tumuenzi vipi ili ilete maana halisi. Wakati natafakari hili nikajiwa na wazo ambalo niliwahi kulituma kwenye blogi ya michuzi kuhusu: historia na chimbuko la majina

Mimi nilijaribu kujikumbusha hivi baba wa taifa alipofika hapa Dar-es-salaam, alifikia hoteli gani, au kama alifikia kwa mwenyeji fulani, alikuwa ni nani na ilikuwa sehemu gani ya jiji hili. Hili la eneo ndilo nililoliwekea manani kwasababu kadhaa. Mojawapo ya sababu ni uwekaji wa kumbukumbu za maeneo kuhusiana na matukio na majina ya maeneo. Hili lingetusaidia sana hasa kwa vizazi vyetu vijavyo. Kwa mfano Mwalimu Nyerere alipofika hapa Dar alishukia kwa mwenyeji wake, ambaye nafikiri alikuwa na makazi yake. Haya makazi yake yangekuwa historia muhimu kwetu. Nyumba hii ingewekwa kama kumbukumbu kama vile tulivyoweza kuweka kumbukumbu ya nyumba ya mahala kilipozaliwa chama cha TANU. Hii isiishie hapa Dar, hata mikoani, mfano sehemu Wakoloni walipokuwa wakiwanyongea wazee wetu na matukio kama hayo.

Maeneo kama haya na mengine kama tutayaweka vizuri katika hali kama ile(hata kama haitafanana sana) ingesaidia sana sio tu kwa vizazi vijavyo,lakini ingekuwa ni sehemu ya vivutio vya watalii. Watalii wengine wanakuja hapa nchini kupata maelezo ya historia ya nchi yetu, wasomi wanahitaji kumbuklumbu kama hizi, kiasilia na sio kimaandishi tu, wengine hupenda kutalii majumba ya zamani nk. Hili sisi kwa hapa Dar sijaliona zaidi ya Kijiji cha Makumbusho, napo ni vitu vimeletwa , na sio sehemu tukio lilipotokea. Nahisi tumeshindwa kulidumisha toka awali, na matokeo yake baada ya miaka kumi ijayo tutashuhudia magorofa kwa kwenda mbele. Hii ndio itakuwa historia ya Dar.

Nilipoandika habari ile kwa Michuzi nilitegemea nitapata wachangiaji wengi wanaojua nini maana ya majina mengi yaliyotolewa kama majina ya maeneo kadhaa hapa Dar, huenda wanaojua machimbuko haya bado wapo hai, ingekuwa jambo la maana pale tunapoona patakuwa kivutio tujaribu kukumbuka jina hilo lilitokana na nini tukajaribu kulirejesha ile hali ya awali japo hata kwa masanamu. Kwa mfano, `mnazi mmoja' kulikuwa na mnazi mmoja mrefu, kwanini tusipande, au kuweka sanamu ya mnazi. Magomeni mapipa kulikwa na mapipa mengi yaliwekwa pale pembeni ya barabara, yalikuwa ya lami kama sikosei. Mwembe madafu kulikuwa na wauza madafu chini ya mwembe, Mbuyuni kulikuwa na Mbuyu Mkubwa, Mwenge nafikiri ilikuwa sehemu ya kuwashia Mwenge, nk

Maswali yanakuja kwenye majina kama Manzese, Buguruni , Sinza nk, haya majina yalitokana na nini hasa? Huenda tunayachukulia kama majina tu, lakini mengine yana maana nzuri kihistoria na maeneo kama hayo yangeenziwa vizuri, ingeleta taswira ya kihistoria na kitalii. Wengi watauliza `ili iweje' au jibu la haraka ni `kutafuta wawekezaji walifanikishe' hata hili jamani mpaka waje wawekezaji?

Sasa muda wa kumuenzi baba wa Taifa unakaribia,kumbukumbu zake nyingi kama sikosei zimepelekwa Butiama, lakini maisha yake mengi yalikuwa hapa Dar, mbona kumbukumbu zake kimaeneo hatuyaoni zaidi ya `kwa Mwalimu Nyerere'. Ina maana kuanzia alipofika, alifikia huko Msasani, na kuanza shughuli hapohapo? Hapana kuna zaidi ya hayo, hasa kipindi cha kupigania uhuru, wapi alikaa, wapi alifanya shughuli zake, nani alikuwa nao kwangu mimi naona hiyo ingekuwa sehemu mojawapo ya kumuenzi na kumbukumbu hizo zingejengewa ingekuwa kivutio kwa taifa letu. Hatujachelewa, tujaribu kuzitafuta nyendo zake wapi alifikia kwa mara kwanza hapa wengi wanapajua,lakini nina wasiwasi na hili.

Nasema hivi kwasababu yupo mmoja wa waliojadili hili kwenye lile basi alisema eti `kuna historia hazitakiwi kujulikana ukweli wake kwa sababu fulani, ndio maana mengi ya mwanzo ya wazee walioshirikiana na baba wa taifa hayawekwi wazi' Kwanini? nilijiuliza bila jibu. Naomba wenye mawazo zaidi watusaidie kwahili. Au nimekosea?

No comments :